NANI MWABUDU SANAMU ?
SWALA
LA SANAMU
Kati ya maswala yanayowakera sana wenzetu Waislamu, na hata baadhi ya
Wakristo wa madhehebu mbalimbali, mojawapo ni lile la sanamu na picha takatifu
zinazotumiwa na Wakatoliki na Wakristo wengine toka karne za kwanza za Kanisa.
Tunawapa pole kwa kero hizo, lakini wasiwe na wasiwasi: hatumlazimishi mtu
yeyote afanye hivyo. Lakini upande wetu tunawaomba wasituhukumu harakaharaka
wakisema, eti, tunaabudu sanamu; sisi tunajua sababu tulizonazo za kutumia vitu
hivyo bila ya kuviabudu, na tuna hakika ya kumpendeza Mwenyezi Mungu. Ukipenda,
nitakueleza kidogo kuhusu jambo hilo, ingawa si la kwanza katika dini yetu.
Yaliyo muhimu kwetu ni imani kwa Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, halafu
tumaini na upendo kwake na kwa jirani yeyote.
Tukizungumzia
sanamu ni kwa sababu tunashambuliwa sana kuhusu jambo hilo, ambalo wengi
wanaliona kuwa ni thibitisho kuwa, eti, Kanisa Katoliki limepotoka kabisa; hivyo,
eti, ni lazima kuliacha na kufuata dini au madhehebu tofauti. Kumbe kuliasi hilo
Kanisa pekee la Yesu Kristo ni kupotea kabisa kwa kutoroka kundi lake na
wachungaji aliowakabidhi kondoo zake.
Toka mwanzo wa maelezo yetu haya tunatamka juu ya imani yetu yale
aliyoyasema mtume Paulo alipolaumiwa kwa kula nyama iliyotolewa kwanza sadaka
kwa miungu ya bandia; jibu lake na letu ni hili, “Kwa habari ya kuvila vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; twajua ya
kuwa sanamu si kitu katika ulimwengu, na ya kuwa hakuna Mungu ila mmoja tu”
(1Kor. 8:4). Tunawaomba wote wapokee
tamko letu hilo; sisi sio wajinga kiasi hicho, hata tukamlinganisha Mungu pekee
na kiumbe chake chochote, hasa kama tulikitengeneza wenyewe.
Wengi wanaotushambulia wanatumia Biblia, hasa kitabu cha Kutoka (20:3-6),
tunaposoma: “Usiwe na miungu mingine
ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho
juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.
Usivisujudie wala kuvitumikia. Kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye
wivu: nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha
wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu”.
Baada ya kusoma maneno hayo, watu hao wanaanza kusisitiza: “ Umesikia? Hilo ni
neno la Mungu! Nyinyi Wakatoliki mmepotoka kabisa! Mapadri wenu wanawadanganya”.
Kweli, mtu asiyejua Biblia na namna ya kuitumia anaweza akashtushwa sana
na maneno hayo hata akadhani kwamba eti, Kanisa linapotosha watu. Lakini
anayejua Biblia vizuri hawezi kamwe kuridhika na dondoo lake moja, kama kwamba
lingekuwa neno pekee la Mungu kuhusu jambo fulani. Biblia imejaa maneno ya kila
aina, na mengine yanaonekana kupingana yenyewe kwa yenyewe. Kanisa tu, ambalo
ndilo “nguzo na msingi wa kweli”
(1Tim. 3:15), linaweza kutueleza
maneno ya Biblia yana maana gani, na kati ya hayo lipi ni muhimu zaidi kuhusu
swala fulani, kwa mfano swala la sanamu.
KATAZO
LA SANAMU LILIVYOTUNZWA CHINI YA SANAMU
Ni afadhali jue kwamba maneno hayo ya Kutoka pamoja na ya amri nyingine
za Mungu yaliandikwa juu ya mbao mbili za mawe ambazo ziliitwa Ushuhuda na
kuwekwa ndani ya sanduku maalumu lililoitwa sanduku la Agano na lililofunikwa
kwa dhahabu. Bila ya shaka hilo si ajabu. Lakini nadhani utashangaa kusoma
katika kitabu hichohicho cha Kutoka (25:16-22)
kwamba Mungu mwenyewe aliagiza zichongwe sanamu juu ya hilo sanduku la Agano: “Kisha
tia ndani ya sanduku huo Ushuhuda nitakaokupa. Nawe fanya kiti cha rehema cha
dhahabu safi; urefu wake utakuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja
na nusu. Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu: uyafanye ya kazi ya kufua,
katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. Weka kerubi moja mwisho
mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili. Fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na
kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku. Na hayo makerubi yatainua mabawa
yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao
zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema.
Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku; kisha utie huo Ushuhuda nitakaokupa
ndani ya sanduku. Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu
ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la
Ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli”.
Ukiwa umesikiliza vizuri, ni kwamba hilo katazo la sanamu lilitunzwa
chini ya sanamu mbili zilizoagizwa na Mungu mwenyewe! Tena, ni kwamba Mwenyezi
Mungu aliahidi kuwa ndipo atakapowatokea Waisraeli na kuzidi kusema nao. Ndiyo
sababu kwa Waisraeli kiti hicho kati ya makerubi kilikuwa mahali patakatifu
kuliko popote duniani. Kumbe hayo makerubi yalikuwa miungu ya makabila ya jirani,
hasa ya Babeli, huko Iraq! Lakini aliyeagiza hayo makerubi yachongwe ni Mwenyezi
Mungu, si binadamu. Hivyo ni dhahiri kuwa katazo la sanamu si la moja kwa moja,
la sivyo Mungu angekuwa anajipinga kwa kuamuru kitu alichokikataza. Lakini sisi
sote tunajua Mwenyezi Mungu hawezi kamwe akajipinga. Kwa hiyo katazo la sanamu
alilotoa, maana yake ni hiyo inayofundishwa na Kanisa Katoliki.
Zaidi ya makerubi hayo yaliyochongwa juu ya sanduku la agano, mengine
mengi yalikuwemo mwenye mapazia ya hekalu, kutokana na agizo la Mungu: “Kisha
fanya hiyo Maskani iwe na mapazia kumi: ifanye ya nguo ya kitani nzuri ya
kusokota, pamoja na nyuzi za rangi ya samawi, na ya zambarau, na nyekundu,
pamoja na makerubi; kazi ya fundi stadi…”(Kut.
26:1-31).
Kutokana na agizo hilo, Bezaleli “akafanya
kiti cha rehema cha dhahabu safi: urefu wake ulikuwa dhiraa mbili na nusu, na
upana wake ulikuwa dhiraa moja na nusu. Kisha akafanya makerubi mawili ya
dhahabu: akayafanya ya kazi ya kufua, yawe katika miisho miwili ya kiti cha
rehema; kerubi moja mwisho huu, na kerubi moja mwisho huu; alifanya hayo
makerubi mawili ya kitu kimoja na hicho kiti cha rehema katika miisho yake
miwili. Na hayo makerubi yakanyosha mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha
rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zilikuwa zaelekeana hili na hili; nyuso za
hayo makerubi zilikuwa zikielekea kiti cha rehema” (Kut. 37:7-9).
Hapo baadaye Solomoni pia alipamba patakatifu pa patakatifu, yaani
undani wa hekalu, kwa makerubi na mengineyo, tunavyosoma katika kitabu cha
kwanza cha Wafalme (6:23-35): “Akafanya
ndani ya chumba cha ndani makerubi mawili ya mzeituni, kwenda juu mikono kumi…
Akayaweka hayo makerubi katika nyumba ya ndani; na mabawa ya makerubi
yakanyoshwa… Akayafunika makerubi kwa dhahabu. Akazinakshi kuta zote za nyumba
kwa nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, pande za ndani na
nje… Akafanya milango miwili ya mzeituni; akanakshi juu yake nakshi za
makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, akaifunika kwa dhahabu; akatia
dhahabu juu ya makerubi, na juu ya mitende. Ndivyo alivyoyafanyia maingilio ya
hekalu miimo ya mzeituni… akanakshi juu yake makerubi…”.
Hivyo ni wazi kwamba tangu mwanzo katazo la sanamu halikuwa la moja kwa
moja. Hata manabii waliopinga vikali ibada za sanamu za kipagani hawakusema
lolote dhidi ya hayo makerubi na michoro ya kupamba hekalu la Mungu wa kweli.
KUABUDU
MIUNGU KATIKA AGANO JIPYA
Sasa tuingie katika Agano Jipya. Injili haituletei neno lolote la Yesu
dhidi ya sanamu. Kinyume chake, katika kueleza atakavyowaokoa watu,
alijifananisha na sanamu ya nyoka ya shaba. Musa aliinua sanamu hiyo jangwani
kwa ajili ya watu walioumwa na nyoka hai kusudi wakiitazama wapone tu; basi,
Yesu alisema: “Na kama vile Musa
alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa,
ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye” (Yoh.
3:l4-15).
Hata alipotaja amri za Mungu, Yesu hakuzitaja zile za kwanza zikiwa ni
pamoja na katazo la sanamu, bali alianza na Usiue: “Wazijua amri: Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye,
Waheshimu baba yako na mama yako” (Mk.
10:19). Ni kwamba mkazo wa Yesu ni mwingine, yaani amri kuu ya upendo. Mtume
Paulo alieleza mkazo huo katika barua yake kwa Waroma (13:8-10):
“Msiwiwe na mtu chochote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye
mwenzake ameitimiza sheria. Maana kule kusema: Usizini, usiue, usiibe, usitamani,
na ikiwapo amri nyingine yoyote, inajumlishwa katika neno hili, ya kwamba:
Mpende jirani yako kama nafsi yako. Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi
pendo ndilo utimilifu wa sheria”.
Siku nyingine Yesu alionyeshwa pesa yenye picha na jina la mtawala, kama
ilivyo desturi hata leo, akauliza, “Ni
ya nani sanamu hii, na anwani hii?” (Math.
22:20); akajibiwa kuwa ni ya mfalme Kaisari. Basi, Yesu alituangalisha
tusiabudu sanamu za namna hiyo akisema, “Hamwezi
kumtumikia Mungu na mali” (Lk. 16:13).
Yaani mali zinaweza zikashika nafasi ya Mungu katika maisha yetu hata
tukaziabudu. Unaweza ukamkuta mtu ambaye anapinga sana sanamu na picha takatifu,
kumbe anatamani sana pesa! Kadiri ya Biblia huyo anaabudu sanamu, yaani pesa.
Anajali twiga zake kuliko binadamu mwenzake anayeweza kuhitaji msaada.
Kwa msingi huo mtume Paulo alisema wazi kufanya hivyo ndio kuabudu
sanamu: “Maana neno hili mnalijua
hakika, ya kwamba hakuna mwasherati, wala mchafu, wala mwenye tamaa, ndiye
mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu” (Ef.
5:5). Ndiyo sababu alionya: “Basi,
vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi: uasherati, uchafu, tamaa mbaya,
mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu” (Kol.
3:5). Barua ya kwanza kwa Timotheo
(6:9-10) inafafanua: “Hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa
nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na
uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo
wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na imani, na kujichoma kwa maumivu
mengi”.
Kadiri ya mtume Paulo, wengine tena wanaabudu tumbo lao, tunavyosoma
katika Wafilipi (3:19): “mwisho
wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao
mambo ya duniani”. Wataalamu wanaeleza kwa namna mbalimbali maana ya
maneno hayo, wengine wakidai kuwa tumbo linamaanisha ulafi, wengine wanasema
linamaanisha tamaa zote za mwili kama vile uzinzi, wengine tena wanaeleza kuwa
maneno hayo ya mtume Paulo yanazidi kuwapinga wale waliosisitiza masharti ya
Kiyahudi kuhusu vyakula, wakifanya maswala ya tumbo kuwa ndiyo dini. Kwa
vyovyote ni kwamba watu hao walijali mno mambo ya mwili, hata kuliko Mungu
mwenyewe. Bila ya shaka watu wa namna hiyo wapo leo pia. Kulaumu picha takatifu
hakutawasaidia kitu. Afadhali waache kuabudu tumbo.
Mfano mwingine ni ule wa mtume Yohane ambaye mwishoni mwa maisha yake
alisumbuliwa sana na baadhi ya wanafunzi wake ambao walileta matata na hatimaye
mafarakano katika jumuia za Kikristo. Barua zote tatu alizoziandika zinakabili
watu hao kwa ukali. Ya kwanza inamalizika kwa maneno yafuatayo: “Watoto
wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu” (1Yoh.
5:21). Ukisoma barua nzima utatambua kwamba haizungumzii kamwe sanamu, ila
mafundisho ya kizushi na utovu wa upendo katika jumuia. Kwa hiyo ni wazi kuwa
maneno hayo ya mwisho hayalengi sanamu zenyewe, ila yanasisitiza yale
yaliyotangulia (1Yoh. 5:20): “Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupatia
akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli. Nasi tumo ndani yake yeye aliye wa
kweli, yaani ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na
uzima wa milele”. Kwa sababu hiyo kupotosha ukweli wa imani hata
kusambaratisha Kanisa ni sawa na kuasi kabisa dini ya Kikristo na kuabudu miungu
mingine. Hata hilo ni la kuzingatiwa sana: unaweza ukamkuta mtu anapinga sana
sanamu na picha takatifu, kumbe analeta mafarakano katika Kanisa akidai wengine
wafuate msimamo wake! Mtu wa namna hiyo anayaamini maoni yake tu, hawezi
kusikiliza wengine, wala hajali umoja wa Kanisa . Kadiri ya Biblia huyo anaabudu
sanamu, yaani anajiabudu pamoja na akili yake. Anajali kiburi chake kuliko
ustawi wa Mwili wa Kristo.
Kabla ya Yohane, Mtume Paulo alionya wanafunzi wake hasa wa Korintho
kuhusu shida hiyohiyo: “Basi ndugu,
nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala
pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja. Kwa maana,
ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya
kwamba iko fitina kwenu. Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu
husema, ‘Mimi ni wa Paulo’, na, ‘Mimi ni wa Apolo’, na, ‘Mimi ni wa
Kefa’, na, ‘Mimi ni wa Kristo’. Je, Kristo amegawanyika? Je, Paulo
alisulubiwa kwa ajili yenu? Au je, mlibatizwa kwa jina la Paulo?” (1Kor. 1:10-13). Mwelekeo huo wa kujivunia mhubiri huyu au huyu
unajitokeza siku hizi katika kusambaza picha zake katika kuwaalika watu
wahudhurie mikutano ya Injili: pengine walewale wanaokataa picha za Yesu na za
watakatifu wake wanaeneza kila mahali zile za mhubiri wanayempenda. Barua hiyo
ya Paulo inaendelea kutuuliza: “Je,
Paulo alisulubiwa kwa ajili yenu? Au je, mlibatizwa kwa jina la Paulo?”.
Nasi tunajiuliza, Je, hao Wakristo wanajiona wameokolewa na mhubiri huyo hata
wapendelee picha yake kuliko ya Yesu? Kuna msingi fulani wa kujiuliza hivyo,
yaani kwamba mara nyingi hao wanajali mhubiri wao kuliko umoja wa Kanisa, lililo
Mwili wa Kristo: “Je, Kristo
amegawanyika?”. Si ajabu kwamba katika madhehebu hayo yanayopinga sanamu
mafarakano hayana mwisho kamwe. Kila kikundi kinang’ang’ania misimamo ya
fulani dhidi ya ile ya wengine wowote hata kusababisha farakano. Hiyo inaweza
kutokea ingawa wahusika wanajidai kuwa hawamfuati Paulo wala Apolo wala Kefa,
ila Kristo, wakisema, “Mimi ni wa
Kristo”.
Hata upande wa siasa mtu anaweza akajikuta akiabudu miungu mingine. Hasa
kitabu cha Ufunuo kinatuangalisha na ibada kwa mtawala wa nchi anayedai kushika
nafasi ya Mungu na kutoa sheria kinyume cha Mungu. Yohane aliandika kitabu hicho
akiwa uhamishoni katika kisiwa cha Patmos, kinachokabili nchi ambayo siku hizi
inaitwa Uturuki. Zamani zake sehemu hiyo ilikuwa tu mkoa wa Dola la Roma. Ndio
mkoa wa Asia ambapo ibada kwa mfalme mkuu wa Roma ilistawi mapema na kwa nguvu
zaidi kuanzia kipindi cha utawala wa Augustus, ambaye chini yake Yesu alizaliwa.
Katika Ufunuo sura ya 2 na ya 3 tunasoma barua saba kwa kanisa la Efeso, mji
mkuu wa mkoa, na kwa makanisa ya miji sita ya kandokando. Miji hiyo yote,
isipokuwa Thiatira, ilikuwa na mahekalu ya kumuabudia mfalme. Hasa huko Efeso
mfalme Domitianus (aliyetawala miaka 81-96 B.K., yaani miaka hiyohiyo Ufunuo
ulipoandikwa) alijijengea hekalu kubwa akidai kuabudiwa na raia zake. Vilevile
alisimamisha sanamu zake katika sehemu zote za Dola la Roma. Kutokana na hali
hiyo ya hatari kwa imani ya Wakristo wanaomwamini Mungu mmoja tu, na Bwana mmoja,
Yesu Kristo, basi Yohane aliandika kitabu cha Ufunuo ili kuwahimiza waamini
wapinge madai ya serikali ya kuwataka raia sio tu watii sheria halali, bali pia
wawape viongozi wake heshima ile anayostahili Mungu tu. Vilevile Yohane
aliwahimiza wapinge dini inayotetea ibada za namna hiyo. Hao ndio wanyama wale
wawili wanaozungumziwa katika sura ya 13: yaani serikali ovu na dini inayoitetea.
Ingawa siku hizi hakuna mfalme wala rais anayedai kujengewa mahekalu ili
aabudiwe, ni kishawishi cha watawala wengi kutaka kushika nafasi ya Mungu kwa
kupanga wenyewe maadili ya wananchi, hata kuwalazimisha watende kinyume cha
dhamiri na dini zao. Matokeo yake ni kwamba waamini wengi wanadhulumiwa, kuteswa
na hata kuuawa. Vilevile ni kishawishi cha viongozi wengi wa dini kutetea
watawala hata wanapotenda maovu. Viongozi hao wanaweza wakawadai waumini wao
watii bila ya kujiuliza kama ni sawa au sivyo. Vilevile ni kishawishi cha
wananchi wengi kufuata mkondo na hivyo kushika sheria za serikali hata
zikipingana na zile za Mungu; na pia kuheshimu nchi yao kuliko inavyofaa, hata
kudharau nchi nyingine; tena kuwaamini mno viongozi wao na vyama vyao hata
kufumba macho mbele ya makosa wanayoyafanya. Hizo zote ni namna za kuabudu
viumbe badala ya Mungu tu.
UJENZI
WA MAKANISA NA MATUMIZI YA SANAMU
Tukirudia sanamu zenyewe, Agano Jipya halisemi kuwa Wakristo wa kwanza
walizitumia, lakini hiyo si hoja, kwa sababu vilevile hawakuwa na mahali maalumu
pa ibada. Hata hivyo siku hizi hakuna anayepinga ujenzi wa makanisa kwa ajili
hiyo akitoa hoja ya kwamba Biblia haizungumzii mahali pa namna hiyo, bali
inasema Mitume na wanafunzi wao walikuwa wakisali pamoja na Wayahudi katika
hekalu pekee la Yerusalemu na katika masinagogi ya kila mji na kijiji, halafu
walikutana kuadhimisha ekaristi katika nyumba za kawaida. Kwa mfano, Matendo ya
Mitume (2:46) yanasema: “Sikuzote
kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, na
kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe”.
Kumbe ukirudi nyuma, unakuta kwamba Wakristo waliopinga sanamu katika
karne ya pili, kwa mfano Minucius Felix kule Afrika Kaskazini, waliweza kupinga
pia ujenzi wa makanisa wakitumia maneno ya Yesu kwa mwanamke Msamaria (Yoh.
4:21): “Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima
huu, wala kule Yerusalemu”. Walisahau kuwa Yesu alikuwa akihiji mara
nyingi Yerusalemu hekaluni. Kama kawaida, hata katika swala hilo kutegemea
mstari mmoja tu wa Biblia ni hatari kubwa ya kuipotosha yote.
Mmojawapo kati ya hao waliopinga majengo ya ibada kwa msingi huo ni
Origenes. Huyohuyo anakumbukwa sana katika historia ya Kanisa kwa utaalamu wake
wa Biblia, lakini pia kwa tendo alilofanya la kujihasi ili atimize namna yake
neno la Yesu kuhusu matowashi, yaani wanaume wasioweza kuungana na wanawake: “Wako
matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi
waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa
matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na
alipokee” (Math. 19:12). Basi, huyo
Origenes alijikata sehemu za siri ili kulipokea neno hilo alivyolielewa; ila
baadaye akajilaumu. Hata hivyo, mpaka leo kuna watu wanaoendelea kusoma Biblia
namna hiyo kwa kuzingatia dondoo hili au hili linavyoonekana mara moja,
wakipuuzia mapokeo ya Kanisa, na hivyo wanaingia hasara kubwa.
Basi, upinzani wa watu hao tuliowataja na wa serikali pia haukufaulu
kuzuia Wakristo wasiendelee kujenga na kupamba makanisa waliyoyahitaji. Kuanzia
mwaka 205 tuna ushahidi wa maandishi kuhusu mahali pa namna hiyo. Ni vilevile
kuhusu picha takatifu. Tunazikuta katika mahandaki ya Roma ambapo Wakristo
mashujaa wa karne tatu za kwanza walikusanyika kwa ibada ili kukwepa askari
wasiwakamate na kuwatesa. Humo tunakuta kwa mfano mchoro wa njiwa kwa maana ya
Roho Mtakatifu, na wa mchungaji mwenye kubeba kondoo mabegani kwa maana ya Yesu
Mchungaji Mwema. Matumizi ya picha yanashuhudiwa vilevile na kitabu cha mwaka
150 hivi kuhusu maisha ya mtume Yohane, na maandishi ya Tertullianus aliyeishi
Afrika Kaskazini kwenye mwaka 200, halafu na historia ya Kanisa iliyoandikwa na
Eusebius wa Caesarea mara baada ya uhuru wa dini kutangazwa na Dola la Roma
(313). Wakristo wakaendelea kutumia hizo picha za Yesu na za watakatifu bila ya
upinzani wowote mpaka Mohamed alipoanzisha Uislamu. Baada tu ya umma wake kuenea
na kuja kutawala nchi mbalimbali za Kikristo, wakazuka Wakristo walioanza
kuzionea aibu picha hizo kutokana na lawama na hoja za Waislamu. Ulikuwa mwaka
724 hivi; mara hata mfalme Leo III aliyetawala Dola la Roma la Mashariki akaanza
kuzipinga na kuzikataza na kuziteketeza. Ndio mwanzo wa mabishano makali
yaliyosababisha hata umwagaji damu hadi mwaka 843 ambapo Wakristo waliotetea
picha takatifu walipata ushindi wa kudumu na kuruhusiwa na serikali.
MUNGU
AMEONEKANA KWETU
Hapo katikati ulifanyika Mtaguso Mkuu wa Pili wa Nisea (787) ambapo
maaskofu walichukua uamuzi wa moja kwa moja kuhusu swala hilo wakieleza sababu
gani kuanzia Agano Jipya sanamu zinakubalika. Kwa kifupi ni kwamba Yesu sio tu
Neno wa Baba bali ni pia sura yake: katika yeye Mungu ametutokea wazi, tofauti
na ilivyokuwa katika Agano la Kale, ambapo Musa aliwaambia Waisraeli: “Bwana
alisema nanyi kutoka kati ya moto; mkasikia sauti ya maneno, lakini hamkuona
umbo lolote; sauti tu” (Kumb. 4:12). Ndiyo sababu hao walikatazwa wasiwe na sanamu: kwa kuwa zamani
hizo hawakujaliwa kumuona Mungu.
Kumbe mtume Yohane aliweza kuanza kwa kishindo barua yake ya kwanza kwa
kushuhudia juu ya Neno la uzima “lililokuwako
tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na
mikono yetu ikalipapasa” (1Yoh. 1:1).
Yesu ni “mng’ao wa utukufu” wa
Mungu “na chapa ya nafsi yake” (Eb.
1:2), “ni mfano wa Mungu asiyeonekana” (Kol. 1:15); “katika yeye
unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili” (Kol. 2:9), hata aliweza kusema: “Aliyeniona mimi amemwona Baba” (Yoh. 14:9). Ukristo ni ufunuo wa Neno na wa sura ya Mungu katika
Kristo. Mwenyewe ni picha ya Mungu isiyofanywa na mikono ya binadamu na
iliyoonyeshwa katika hekalu la mwili wake.
Kuanzia hapo imani inatokezwa na kutangazwa si kwa maneno tu, bali pia
kwa picha ambazo ni mafundisho kwa njia ya macho na ushahidi wa ukweli wa
umwilisho wa Mwana wa Mungu. Bila ya shaka ni lazima tuangalie kwamba picha
tunazozichora zilete ujumbe sahihi kadiri ya imani, kama vile ni lazima tuwe
macho ili mahubiri na mafundisho tunayoyatoa yasipotoshe ukweli wa ufunuo wa
Mungu. Mtaguso wa Pili wa Vatikano umeagiza: “Maaskofu wasikubali kamwe
matumizi ya sanaa yanayopingana na imani na maadili na uchaji wa Kikristo katika
nyumba ya Mungu na mahali pengine patakatifu. Pia wakatae yale yanayovunja
heshima halisi ya kidini kwa sababu ni batili au kwa sababu hayatoi vielelezo
halisi vya mambo matakatifu”.
Tunapaswa kuchambua picha, si kuzikataa jumla kama kitu kiovu. Hasa kwa
wasiojua kusoma zinachangia sana imani na upendo kwa Bwana Yesu wakitambua
upendo wake katika madonda na damu yake wanavyoona vimechorwa kwa usanii mkubwa.
Mbele ya msalaba wengi wanaongoka na kuachana na dhambi zao. Wengine wanaponywa
kimwili pia, kutokana na imani yao kwa Yesu iliyochochewa na picha yake. Bila ya
shaka picha si mwenyewe, lakini inamwakilisha na kumfanya akumbukwe: hiyo ni
kweli sio tu kuhusu picha zinazopigwa na kamera, bali pia kuhusu michoro na
sanaa nyingine inayofaulu kutufikirisha juu ya mtu fulani.
VIWAKILISHI
VYA MTU
Agano Jipya linatusimulia jinsi watu wadogo walivyoweza kufaidika kiroho
na kimwili na vitu vilivyosaidia imani yao, kama vile vazi la Yesu, kivuli cha
Petro na leso na nguo za Paulo. Vitu hivyo vilipata nguvu kwa sababu ya
kumwakilisha mmiliki wao. Tusome habari hizo za ajabu: “Tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka
kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake. Kwa maana
alisema moyoni mwake, ‘Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona’. Yesu
akageuka, akamwona, akamwambia, ‘Jipe moyo mkuu, binti yangu, imani yako
imekuponya’. Yule mwanamke akapona tangu saa ile” (Math.
9:20-22). Kilichomponya ni imani yake, lakini hiyo ilisaidiwa na tendo la
kugusa pindo la vazi la Yesu. Ilitokea vilevile kwa wengine wengi walioletwa
kwake hawawezi; “nao wakamsihi waguse
hata pindo la vazi lake tu. Na wote waliogusa wakaponywa kabisa” (Math
14:36). Ilitokea vilevile kwa
mitume wake: “hata ikawa katika njia
kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro akija,
ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao… nao wote wakaponywa” (Mdo.
5:15-16). “Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata
wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao
yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka” (Mdo.
19:11-12). Bila ya shaka vitu hivyo vyote havikuwa Yesu wala mitume wake
wenyewe, lakini viliwawakilisha na kuwasaidia hao wagonjwa wawe na imani kwao.
Si tofauti kwa picha na sanamu zetu: si Yesu wala si watakatifu wake wenyewe,
lakini zinaweza kutusaidia tuwakumbuke na kujisikia tunaungana nao kwa njia hiyo.
Sisi tunadhani kwamba waamini, baada ya kuelezwa vizuri na wachungaji wao, wana
akili na imani ya kutosha hata waweze kuhusianisha picha na mtu bila ya
kuwachanganya wala kudhani eti picha ndio mtu mwenyewe!
Kwa vile ufunuo umekusudiwa kwa watu wote bila ya kujali uwezo wa akili
yao, Mwenyezi Mungu alipojifunua alitumia alama na njia za kila aina, kama vile
moto, njiwa pamoja na sauti. Naye Yesu alitumia vitu kama vile mate, matope n.k.
katika kuwaponya watu akatuachia sakramenti saba ambazo zote ni alama wazi
ambazo kwa kuonekana na kusilikana kwao zinamaanisha na kutuletea neema za fumbo.
Basi, ni dhahiri kuwa anatutaka sisi pia tutumie njia zote za maarifa: kusikia,
kuona, kugusa n.k. ili yeye ajulikane na kutukuzwa. Upande mmoja tusidhani
kwamba tutamjua na kumjulisha kwa njia za maarifa na vionjo vyetu tu: muhimu
zaidi ni akili na hasa imani. Upande mwingine tusiingie kosa la kudhani
tunatakiwa kutumia akili au imani tu, hata kukataa matumizi ya vitu na milango
ya fahamu. Yesu alisifu imani ya yule mwanamke ingawa yeye aliona haimtoshi
kumuamini bila ya kugusa pia pindo la vazi lake. Anayetakiwa kumjua na
kumkaribia Mungu katika ibada na maisha ni binadamu nafsi nzima: yaani mwili kwa
kutumia vionjo vyake na njia zake za maarifa, akili kwa kuchanganua, kuchambua
na hata kusanii taarifa zinazomfikia, ikiongozwa daima na imani kwa ujumbe wa
Mungu.
Ni mang’amuzi ya siku nyingi kwamba ibada kadhaa zinavutia sana
waamini kwa vile zina kielelezo cha sanamu na picha zinazowasaidia kutafakari
mafumbo ya wokovu, kwa mfano ibada ya Ijumaa Kuu. Tazama pia upendo na huruma
ambavyo vinaamshwa na ibada ya Njia ya Msalaba! Na tazama vinavyozidi kuongezeka
kila kituo hadi msalabani na kaburini. Kweli, unaweza ukawasimulia watu mateso
ya Yesu na kusababisha uchungu na majuto. Lakini wakiona picha za filamu juu ya
mateso hayohayo, zikiwachorea mazingira yale yalivyokuwa, wengi wataguswa zaidi
hata kulia machozi, hata kama wanajua kuwa ni igizo tu. Kumuona Yesu amefungwa
kamba nene akiwa mikononi mwa wakatili ambao wanampiga mijeledi na kutiririsha
damu yake: ni picha ambazo hazisahauliki kwa urahisi na zinasaidia kufikiria
tukio ambalo hawakulishuhudia wenyewe. Pasipo msaada huo, kila mmoja anajichorea
akilini kadiri ya ujuzi na uwezo wake. Kumbe wasanii wamejaliwa na Mungu kipaji
cha kutuchorea kwa ufanisi mkubwa mambo yoyote, hata ya imani, na kama talanta
nyingine zozote wanapaswa kukifanyia kazi kwa faida ya wote. Biblia inasifu
ufundi waliojaliwa wale waliochaguliwa kuchonga makerubi : “Basi,
Bezaleli na Oholiabu watatenda kazi, na kila mtu mwenye moyo wa hekima, ambaye
Bwana amemtia akili na hekima ili ajue kufanya kazi hiyo yote kwa huo utumishi
wa mahali patakatifu, kama hayo yote Bwana aliyoyaagiza” (Kut.
36:1). Ukurasa wa kwanza wa Biblia unamfananisha Mungu na msanii ambaye
anatazama kila kazi ya mikono yake na kuridhika nayo. Alipomuumba mtu, kiumbe
chake bora duniani, alimshirikisha usanii wake kama kipaji cha pekee cha
kutokeza zaidi uzuri wa viumbe vyake. Msanii anahisi uzuri kuliko watu wengine,
na pia anaweza kuutokeza kwa kiasi fulani katika mashairi, michoro n.k. Kwa haki
sanaa mbalimbali zinahesabika kati ya kazi za heshima zaidi kwa binadamu, kwa
kuwa zinatokeza uwezo wake wa kufurahia uzuri. Kanisa pia toka zamani
limeheshimu kipaji hicho na kukikaribisha katika ibada zake, kuanzia muziki
mtakatifu. Katika historia yote, sehemu kubwa ya sanaa zote zinazohifadhiwa na
Umoja wa Mataifa ni sanaa za Kikatoliki. Kanisa linaukabidhi usanii kazi ya
kufanya ulimwengu wa roho uvutie zaidi kwa kutokeza uzuri wa mafumbo ya imani
pia katika rangi, sauti na kadhalika. Lakini watu wote jumla wanahitaji daima
kuchota katika sanaa mwanga fulani kuhusu maisha yao ambao unaelekeza kwa Mungu.
Uzuri unatia pia tumaini kati ya mabaya mengi yanayokera duniani.
Ushirikiano wa imani na sanaa uliwahi na bado unaweza kutokeza uzuri wa
kazi ya Mungu unaong’aa hasa katika Yesu na watakatifu wake. Kwa watu wote
uzuri wa namna hiyo ni njia ya kupenya mafumbo ya imani na ni mvuto wa kuinuka
juu kuliko mambo ya dunia hii. Tufikirie tu uzuri wa muziki wa dini unaotokeza
kwa namna bora yaliyomo katika maneno ya Zaburi fulani hata kutufanya tuyaonje
na kuyafurahia kwa dhati kabisa. Vilevile hatuwezi kuikataa amani inayotuingia
moyoni mahali penye picha nzuri za imani, tofauti kabisa na karaha na vishawishi
vinavyotupata kwenye picha zisizofaa.
Katika ulimwengu wa leo tunapatwa na mafuriko ya picha za kila aina,
nyingi zikiwa chafu na katili, nazo zinavuta hasa watoto na vijana kutenda vile
walivyoona. Ikiwa shetani anazitumia sana hizo picha kwa kutupotosha, kwa nini
sisi tusitumie njia hiyohiyo kuenezea usafi na wema? Tunapovaa au kubandika
mahali picha takatifu huwa tunaungama na pia kutangaza imani yetu kwa njia yake.
Wafanyabiashara wanajua vizuri jambo hilo, hata wakamwaga pesa nyingi ili picha
ya bidhaa yao ionekane popote pamoja na jina lake. Na kweli wateja wanakimbilia
hasa bidhaa zilizotangazwa zaidi. Basi, nasi tutangaze popote imani yetu hata
kwa njia hiyo.
Tena, hizo ishara za imani zinatudai tuishi kwa uadilifu tusije
tukaaibisha dini yetu na kujiaibisha mbele ya wale wanaoziona tumezivaa au
kuzibandika kwetu. Hivyo pia zinachangia utume wetu kwa kutuhimiza tuwe na
mwenendo mwema. Lakini hata kabla ya hiyo, picha takatifu zinaamsha ndani mwetu
hamu ya kulingana na Yesu au mfuasi wake aliyechorwa ndani yake. Ni kama
unapoona picha ya baba wa taifa, marehemu mwalimu Nyerere, na papohapo
unakumbuka uaminifu wake na ujumbe wake wa amani na haki ambao unakudai
usipotoke.
HESHIMA
KWA SANAMU NA PICHA TAKATIFU
Pamoja na kukataa jumla matumizi ya picha takatifu katika makanisa,
wengi wanasema linawakwaza hasa tendo la kuziheshimu. Kumbe labda hawashangai
jinsi kinavyoheshimika kitabu cha Neno la Mungu, kwa kukijaladia vizuri,
kukishika kwa uangalifu mkubwa, kukishangilia, kukibusu na hata kukifukizia
ubani. Kwetu ni wazi kabisa kwamba heshima tunayoitoa hailengi ubao, madini au
chochote kile kilichotumika kutengenezea picha au sanamu, wala karatasi na wino
vilivyotumika kuandikia kitabu hicho, bali yule aliyechorwa au anayesema nasi
kwa vitu hivyo. Hilo ni jambo la kawaida katika maisha ya binadamu, ambaye
anatunza kwa makini picha za watu anaowapenda, na vitu vyao, si kutokana na
thamani ya vitu hivyo, bali kutokana na jinsi anavyothamini watu hao. Ukichukua
picha ya marehemu wake, kwa mfano, na kuichana kwa dharau, utaona
atakavyosikitika. Ni vilevile ukichana kitambaa chenye rangi za taifa:
utalaumiwa na kuhukumiwa kwa kuikosea heshima nchi na watu wake. Tunasoma
historia ya mtawa Stefano ambaye alithubutu kumuendea huyo mfalme Leo
mwanzilishi wa mapambano dhidi ya picha takatifu akamuonyesha pesa yenye sura
yake, akimuuliza: “Sura hii ni ya nani?”. Mfalme akamjibu: “Mbona ni sura
yangu!” Hapo mtawa akaitupa ile pesa chini akaikanyagakanyaga. Mara akakamatwa
akahukumiwa kifo kwa sababu ya kukanyaga sura ya mfalme. Lakini wakati wa
kupelekwa akamuambia mfalme: “Tazama! Kama mimi nitaadhibiwa hivi kwa sababu
tu sikuheshimu sura yako katika pesa, na wewe ni kiumbe tu utakayekufa,
watastahili adhabu gani watu kama wewe wanaoteketeza picha za Yesu, Mwana wa
Mungu?”. Ingawa huyo mtawa shujaa akauawa, ukweli alioutoa kwa maneno yake
unabaki palepale hata leo.
Heshima inaweza kutolewa kwa namna mbalimbali, kadiri ya utamaduni wa
mahali: sehemu nyingine watu wanaheshimiana kwa kupiga goti, kwingine kwa
kuinama au kuinamisha kichwa, kwingine kwa kubusiana mikono au nyuso, na
kadhalika. Ni kweli kwamba baadhi ya heshima hizo tunazitumia kwa Mungu pia,
lakini nadhani kila mtu anaelewa kuwa tukimpa Mungu ni kwa dhati kuliko
tunapompa kiumbe chake. Hata katika Biblia tunaona matendo hayo yalivyotumika
kwa watu wa Mungu, kwa mfano mfalme Daudi: “Ahimaasi
aliinua sauti yake, akamwambia mfalme, ‘Amani!’ Akainama mbele ya mfalme
kifudifudi, akasema, ‘Ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyewatoa watu hao
walioiinua mikono yao juu ya bwana wangu, mfalme’” (2 Samweli 18:28). Mfalme Daudi hakukataa kusujudiwa, kwa sababu huyo
Ahimaasi alipofanya hivyo alimhimidi Mungu aliyemuokoa, na hivyo alimkiri Mungu
wake kuwa mkuu kabisa. Hata nabii Nathani alimuinamia mfalme Daudi: “Walimwambia
mfalme wakasema, ‘Tazama, Nathani, nabii’. Naye alipoingia ndani mbele ya
mfalme, akamsujudia kifudifudi” (1Fal.
1:23). Nabii wa Mungu hakuona ni kosa kumsujudia mfalme aliyeteuliwa na
Mungu aongoze kwa niaba yake taifa la Israeli.
Tukiendelea
kusoma tunakuta nabii Eliya alivyopokea kwa wema wajumbe wa mfalme Ahazia
waliomuinamia, tofauti na waliotangulia kumuendea ambao hawakumheshimu vya
kutosha wakateketezwa kwa moto kutoka mbinguni: “Yule
akida wa hamsini wa tatu akapanda, akaenda akapiga magoti mbele ya Eliya,
akamsihi sana, akamwambia, ‘Ee mtu wa Mungu, nakusihi, roho yangu na roho za
watumishi wako hawa hamsini ziwe na thamani machoni pako’” (2 Fal. 1:13). Eliya, mtetezi mkuu wa upekee wa Mungu, hakulaumu hilo
tendo la kumpigia magoti na kumsihi yeye binadamu, kwa msingi wa kuwa aliitwa
mtu wa Mungu, yaani akida alimtofautisha na Mungu na kumheshimu kwa kuwa ni
nabii wake.
Ni
kweli kwamba watu wengine wa Mungu na malaika walikataa kupigiwa magoti, lakini
Biblia inaonyesha wazi ni kwa sababu gani, yaani kwa kuwa waliopiga magoti
walitaka kuwaabudu kama Mungu au miungu. Kwa mfano, tunasoma katika Matendo
14:11-15: “Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema
kwa Kilikaonia, ‘Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu’. Wakamwita
Barnaba, Zeu, na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji. Kuhani wa Zeu
ambaye hekalu lake lilikuwa mbele ya mji, akaleta ng’ombe na taji za maua hata
malangoni, akitaka kutoa dhabihu pamoja na makutano. Walakini mitume Barnaba na
Paulo, walipopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika
makutano, wakipiga kelele, wakisema, ‘Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi
nasi tu wanadamu hali moja na ninyi’”. Kwa msingi huohuo Yesu alikataa
kumsujudia shetani: “Ibilisi alimchukua
mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake,
akamwambia, ‘Hata yote nitakupa, ukianguka kunisujudia’. Ndipo Yesu
alipomwambia, ‘Nenda zako, shetani! Kwa maana imeandikwa: Msujudie Bwana Mungu
wako, umwabudu yeye peke yake’” (Math.
4:8-10). Lakini Yesu hakusita kupiga magoti mbele ya mitume wake, wakiwa ni
pamoja na Yuda msaliti, ili awaoshe miguu kama kwamba ni mtumwa wao: “Alitia
maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile
kitambaa alichojifunga” (Yoh. 13:5).
Tendo lilelile moja linaweza kuwa na maana mbili, moja mbaya moja bora kabisa.
Inategemea nia ya mtu.
Ndivyo
ilivyo pia kuhusu vitendo vyetu vya heshima kwa picha na sanamu takatifu: sisi
hatuna nia yoyote ya kuziabudu. Ila tunamuabudu Yesu aliyechorwa kwa kuwa ni
Mwana wa Mungu, na tunawaheshimu kiasi chao watakatifu wake kwa sababu ni watu
wa Mungu na kwa sababu Mungu mwenyewe anawaheshimu, alivyosema Yesu: “Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu
atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu” (Yoh.
12:26).
Zingatia
kuwa picha zetu zote ni za viumbe halisi, sio za miungu ya bandia kama
ilivyokuwa kwa wapagani wa zamani za Agano la Kale na za Agano Jipya walioabudu
sanamu za wanyama na za vingine visivyowahi kuwepo nje ya ubunifu wao. Sisi
tunamchora Yesu na watakatifu wake, hasa mama yake: hao wote waliishi kweli
duniani wakatuachia mifano bora ya uadilifu, nasi tunawaheshimu kwa sababu
hiyohiyo tu, yaani kwa jinsi walivyompenda na kumtumikia Mungu. Ni watu halisi,
tena bora, walio hai kwa Mungu na wanaostahili heshima zote.
Kumhusu
Yesu tumeandikiwa na mtume Paulo: “Iweni
na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu, ambaye
yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu
kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa
namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama
mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa
hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;
ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na
vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu
wa Mungu Baba” (Fil. 2:5-11).
Amina: kwa jina la Yesu kila goti lipigwe! Lakini, ebu, jina ni kitu gani?
Ni kiwakilishi tu cha mtu mwenyewe. Ukiliheshimu jina la Yesu, heshima
inamuendea yeye, si herufi zinazounda jina hilo. Basi, hata picha yake inaweza
kuwa kiwakilishi chake, hivi kwamba heshima unayokipatia inamuendea Yesu
mwenyewe. Ndiyo sababu jina hilo linaweza likatamkwa kwa namna mbalimbali kadiri
ya lugha, bila ya kupotewa na maana yake ya kumwakilisha mwana wa Maria wa
Nazareti: unaweza kumuita Jesus kwa Kiingereza, Isa kwa Kiarabu, n.k., mradi
umkiri kuwa ndiye Bwana wa vyote. Kumbe unaweza ukamkuta mtu anayesisitiza
kwamba si sahihi kumuita Yesu “Kristu”, wakidai matamshi ya kufaa ni “Kristo”.
Yaani kuishia na o badala ya u! Tukitaka kuzingatia matamshi asili ya Kigiriki
tunatakiwa kutamka Kristos, au sanasana Kristosi. Na tukifanya hivyo, kwa nini
tusitamke vizuri pia jina la Yesu, kwa Kiyahudi Yeshuah ? Ni afadhali
tukubaliane kwamba matamshi si muhimu zaidi, yanaweza kubadilika kadiri ya
mahali. Nikitamka Kristu siendi motoni kwa hiyo, na nikitamka Kristo siendi
mbinguni kwa hiyo.
Unajua,
katika maisha ya Yesu wengi hawakumuelewa, hasa wale wasiotaka kumuelewa. Hivyo
si ajabu kukuta hata leo wabishi waliojipa kazi ya kukosoa wote na kusahihisha
yote, hata kuhusu mambo madogomadogo. Mtu akipenda anaweza akatusahihisha wote
tunaposema kuwa jua limezuka au limepanda au limetua, akisisitiza kwamba jua
halisogei popote, bali dunia inazunguka kandokando yake. Lakini atasaidia nini?
Mbona siku hizi karibu wote wanajua kuwa ndivyo ilivyo? Tuachane na kiburi!
Tusidhani kuwa sisi peke yetu tunaelewa jografia, na wengine wote ni wajinga
kiasi hicho.
KUABUDU MSALABA
Haya
tuliyoyasema yanafaa kuhusu neno moja la liturujia ya Ijumaa Kuu ambalo
linaeleweka vibaya na kupingwa sana na baadhi ya wenzetu, yaani ‘kuabudu
msalaba’. Wanalielewa kama kwamba ni ibada kwa mbao zake. Basi, tunaposema
“kuabudu msalaba”, tunaomba wenzetu hao watuelewe tunataka kusema nini.
Nichukue mfano wa mtume Paulo aliyeandika: “Yeye
aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana” (1Kor.
1:31), yaani asionee fahari kitu kingine chochote. Hata hivyo alipowaandikia
Wagalatia mwenyewe alitamka (6:14): “Lakini
mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu chochote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu
Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulubishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu”.
Ni
wazi kuwa Paulo hakutaka kusema anazionea fahari mbao za msalaba tu, bali fumbo
la msalaba ambalo tumekombolewa. Fumbo hilo limebadilisha kabisa ulimwengu,
likidai tubadili pia mawazo na matendo yetu yote tukabebe misalaba yetu nyuma ya
Yesu: “Mtu yeyote akitaka kunifuata na
ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate” (Mk. 8:34). Tukimzungumzia Kristo jumla tu, tunaweza tukamuelewa kama
mtukufu tu, mbali na ulimwengu na mateso yake, na hivyo kutufanya tukwepe hali
halisi ya ulimwengu huu wa mateso. Ndiyo sababu Paulo alisisitiza kwamba “sisi
tunamhubiri Kristo, aliyesulubiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni
upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na
hekima ya Mungu” (1Kor. 1:23-24).
Kwa hiyo tunapaswa kukubali kwanza mpango wa Mungu aliyetaka Mwanae ateswe
msalabani ili abebe laana ya dhambi zetu na kuifutilia mbali, halafu sisi
tufuate nyayo zake. Mtume alilionea fahari fumbo hilo, ingawa alijua fika kuwa
Kumbukumbu la Torati (21:22-23)
linasema: “Akiwa mtu ametenda dhambi ipasayo kufa, akauawa, nawe utamtundika juu
ya mti, mzoga wake usikae usiku kucha juu ya mti; lazima utamzika siku iyo hiyo,
kwani aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu”.
Sisi
pia tusione msalaba kama adhabu ya aibu, bali tuupende na kuuonea fahari. Si
mbao za msalaba ambazo hatujui zilikwenda kwishia wapi, bali fumbo hilo la
upendo wa Mungu lililotukomboa, na hasa yule aliyesulubiwa kwa ajili yetu. “Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi
tunaookolewa ni nguvu ya Mungu” (1
Kor. 1:18). Ndiye tunayemuabudu. Kama tulivyokwishaeleza, tunapopiga goti
mbele ya sanamu ya Yesu msulubiwa na kuibusu, heshima hizo zinamuendea yeye kama
shukrani ndogo kwa upendo wake mkuu. Naye anazipokea kama alivyozipokea heshima
alizopewa na watu wa zamani zake, ingawa wengine walinung’unika. Tunasoma, kwa
mfano, habari za mwanamke ambaye alimpaka mafuta Yesu akasifiwa naye kwa
kumuonyesha hivyo heshima yake: “Amin,
nawaambieni: Kila patakapohubiriwa Injili hii katika ulimwengu wote, tendo hilo
alilolitenda huyu litatajwa pia kwa kumbukumbu lake” (Math. 26:13). Kumbe baadhi ya wanafunzi na wengineo walinung’unika
sana, hata ilimpasa Yesu kuwakemea: “Mwacheni;
mbona mnamtaabisha? Amenitendea kazi njema” (Mk. 14:6). Angalia usirudie leo kosa walilolifanya hao kwa kumlaumu
bure huyo mwanamke kwa jinsi alivyomheshimu Yesu tofauti na mitazamo yao.
Unaweza ukamlaumu mtu anayemheshimu Yesu kwa kubusu sanamu yake kwa imani na
upendo, ukijidai wewe tu una imani na unajua namna ya kufaa ya kumheshimu. Kumbe
Yesu ameridhika kabisa na heshima zake.
Hata
siku nyingine wanafunzi walionywa na Yesu alipoona wanataka kuwazuia watu
wasimheshimu walivyotumwa na moyo wao, yaani kwa kumuomba awabariki watoto
waliomletea. “Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, ‘Waacheni watoto wadogo
waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin,
nawaambieni: Yeyote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia
kabisa’” (Mk. 10:14-15). Ndio,
ndugu, tunahitaji kuongoka na kuwa kama watoto ili tuingie katika ufalme wa
Mungu. Badala ya kuwahukumu watu wenye moyo wa kitoto mbele ya picha takatifu,
tujitahidi kuachana na kiburi na tabia ya kuhukumu bure. Mungu tu anajua mioyo
ya watu. Tusiwapime kulingana na namna ambayo sisi tunajua Biblia. Hata zamani
za Yesu waliojidai waadilifu kwa kujua na kushika sheria ya Musa walidharau sana
wenzao wasiokuwa na elimu hiyo. Kumbe ndio walioshindwa kumuamini na kumfuata
Yesu. Sikiliza maneno yao: “Ni nani katika wakuu amwaminiye, au katika Mafarisayo? Lakini
makutano hawa wasioifahamu torati wamelaaniwa” (Yoh.
7:48-49). Yesu aliwahi kuwaonya: “Mwayachunguza
Maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na
hayo ndiyo yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima”
(Yoh. 5:39-40). Namna yao ya kuelewa
Biblia, pamoja na kuwafanya wahukumu wenzao, iliwasogeza mbali na Yesu mwenyewe,
hasa baada ya kumuona amefia msalabani! “Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu
tunaookolewa ni nguvu ya Mungu” (1Kor.
1:18).
No comments:
Post a Comment