Papa
atoboa siri ya Rozari
l Alipigwa
risasi Siku ya Bikira Maria wa Fatima
l Aliitolea Tanzania kwa Bikira Maria
VATICAN
CITY
BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa
Pili,ametoboa siri ya yeye kuhimiza matumizi ya Sala ya Rozari Takatifu ya
Bikira Maria.
Akizungumza kwa waamini wa waliokusanyika katika Viwanja vya
Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro hivi karibuni, Baba Mtakatifu aliwahimiza
Wakatoliki na watu wengine wanaosali Sala ya Rozari Takatifu, kuwa rozali
inajumuisha njia bora za kukuza majitoleo ya kutafakari uso wa Kristo.
“Sababu muhimu ya kupendekeza tena kusali Rozari, ni ukweli
kwamba inajumuisha njia bora za kukuza majitoleo ya kutafakari uso wa Kristo
miongoni mwa waamini, jambo nililoliomba kufuatia Jubilei Kuu ya mwaka 2000,”
alisema Baba Mtakatifu.
Akaongeza, “Bikira Maria ni mfano mkubwa wa tafakari ya
Kikristo,” alieleza Papa akikumbuka maudhui ya barua yake ya kitume “Rosarium
Virginis Mariae.”
“Tangu kuchukuliwa mimba kwa Kristo mpaka ufufuko na kupaa
kwake mbinguni, Mama yake aliendelea kuelekeza moyo wake usio na doa kwa Mwanae
wa Kimungu: tafakari ya ajabu, inayopenya mioyo, ya huzuni na yenye kung’ara,”
alisisitiza.
“Ni katika mtazamo huu wa
Ki-Maria, uliojaa imani na upendo, Mkristo na Jumuiya ya Kanisa, hufanya sala yao wakati wanaposali Rozari,” alisema Papa.
Alisema, hiyo ndiyo sababu ya yeye kupendekeza kuongezwa kwa
Mafumbo ya Nuru katika Rozari, yanayohusu maisha na kazi za Yesu.
Katika KIONGOZI toleo lililopita, tuliripoti kuwa katika
Maadhimisho ya Miaka 24 ya Upapa, Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili,
alitangaza Mwaka wa Rozari na kupendekeza Mafumbo ya Nuru kuongezwa katika sala
hiyo.
Historia ya maisha ya Papa Yohane Paulo wa Pili inaonyesha
wazi Ibada kubwa aliyonayo yeye binafsi kwa Mama Bikira Maria. Tangu
aliposimikwa kuwa Baba Mtakatifu ,aliutolea utume wake chini ya maombezi ya
Bikira Maria,ndiyo maana hata nembo yake ina herufi’M’ ikimanisha ‘Matoleo
maalumu kwa Bikira Maria’.
Katika tukio lisilo la
kawaida la jaribio la kumuua,lililofanyika Mei 13 mwaka 1981 na Mehmet Ali Agea
(23) raia wa Uturuki,jaribio hilo lilifanyika katika sikukuu ya Bikira Maria wa
Fatima ,na kuokoka kwake yeye alikuelezea ni kutokana na maombezi ya Bikira
Maria.
Katika ziara zake katika nchi mbalimbali duniani,Papa amekuwa
akisisitiza Ibada kwa Bikira Maria kwa kugawa zawadi ya rozali kwa kila
anayekutana naye;na kumtaka asali Rozali.
Akiwa nchini Tanzania katika ziara yake ya Kichunguji mnamo Septemba 1990,Baba
Mtakatifu mara tu baada ya kuwasili nchini alielekea katika Kanisa la Mtakatifu
Yosefu lililopo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam,ambapo aliongoza
sala ya Rozali kuiombea nchi hiyo Amani
na Utulivu.
Katika Barua ya Kitume inayoitwa Rosarium Virginis
Mariae (Rozari ya Bikira Maria), Papa anatoa Sala ya Bikira Maria kama
tafakari juu ya mafumbo ya maisha na kazi ya Kristo iwapo itasaliwa kwa uchaji
na si kwa midomo tu.
Katika kuelezea uamuzi wake wa kuongeza mafumbo matano ya
nuru katika Rozari ya sasa, Papa alisema kuwa, Rozari ya Bikira Maria ni kama
ufupisho kamili wa Injili uliolenga kutafakari sura ya Kristo kupitia macho ya
Maria na kurudiarudia Sala ya Salamu Maria.
Alisema hadi sasa mafumbo 15 ya Rozari yaani, ya Furaha,
Uchungu na Utukufu, yamekosa nyakati mahususi katika maisha ya Kristo
hadharani.
Kwa sababu hiyo, Baba Mtakatifu alipendekeza kuingiza Mafumbo
ya Huduma ya Kristo ya hadharani kati ya Ubatizo wake na mateso yake.
Katika Kifungu cha 21 cha barua hiyo, Papa anatilia mkazo juu
ya Mafumbo ya Nuru ya maisha ya
hadharani ya Yesu na kufafanua fumbo ambalo Mkristo hutafakari katika kifungu
cha matini.
Anayataja matini hayo kuwa ni Ubatizo wa Yesu, Kujidhihirisha
kwake katika Harusi ya Kana, Utangazaji wake wa Ufalme wa Mungu, Mwito wake kwa
uongofu, kugeuka kwake sura na kuweka Sakramenti ya Ekaristi kama kielelezo cha
Fumbo la Pasaka.
Akizungumza hivi karibuni, Baba Mtakatifu alisema, “Kama
kila sala ya dhati, Rozari haituondoi kutoka uhalisia wa mambo, ila hutusaidia
kuiishi sala hiyo tukiwa tumeunganika na Kristo kwa ndani, huku tukitoa
ushuhuda kwa upendo.”
Papa Yohane Paulo wa Pili, pia aliwakumbusha waamini, kama
alivyofanya katika barua yake ya kitume, kwamba amani na familia ni malengo
mawili ya msingi ya kusali Rozari.
Kwa namna ya pekee, Papa alitoa wito wa kuwaombea watu wa
Urusi ambao katika siku hizi za hivi karibuni, wamekuwa katika mateso makali
wakati wa mgogoro wa utekaji nyara katika jumba la maigizo jijini Moscow.
Mgogoro huo uliisha Jumamosi ya Novemba 26, mwaka huu, baada
ya makomandoo wa Jeshi la Urusi kuwaokoa mateka ambapo watekaji nyara wote 50
waliuawa pamoja na mateka 117.
“Wakati tunawaombea wahanga wa kisa hicho
cha maumivu, tumwombe Bikira Mtakatifu ili matukio kama
haya yasiweze kurudiwa,” alisema Papa.
No comments:
Post a Comment