Saturday, May 31, 2014

Ujumbe wa Siku ya 48 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2014

Mama Kanisa tarehe Mosi Juni, 2014 anaadhimisha Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni sanjari na Siku ya 48 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni, inayoongozwa na kauli mbiu “Mawasiliano katika huduma ya kweli ya utamaduni wa kukutana”. RealAudioMP3

Baba Mtakatifu anasema kwamba, watu wanaishi katika ulimwengu ambao ni kama kijiji kwani watu wanakaribiana sana, na njia za mawasiliano ya jamii zimeboreka zaidi katika ulimwengu wa utandawazi kiasi kwamba, kuna mwingiliano mkubwa wa watu.

Lakini jambo la kusikitisha anasema Baba Mtakatifu ni kuona kwamba, bado kuna migawanyiko katika Familia ya binadamu, kuna pengo kubwa kati ya matajiri na maskini kiasi kwamba, tofauti hizi kubwa ambazo zinapaswa kuonekana kuwa kashfa katika maisha ya binadamu, zimeanza kuzoeleka na kuwa ni jambo la kawaida kabisa. Dunia inaendelea kuteseka kutokana na utengano, umaskini, vita na kinzani zinazojikita katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na hata wakati mwingine kidini!

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, njia za mawasiliano ya kijamii zinaweza kuwajengea watu ari ya umoja na mshikamano katika familia ya binadamu, ili kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Mawasiliano yanaweza kusaidia kubomoa kuta za utengano kwa kujenga utamaduni wa kusikilizana na kujifunza kutoka kwa wengine, ili hatimaye, kukuza majadiliano yanayowawezesha watu kufahamiana na kuheshimiana. Utamaduni wa kukutana unadai watu kuwa tayari si tu kutoa bali pia kupokea. Njia za mawasiliano ya kijamii ambazo zimeboreska kwa kiasi kikubwa kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia zinaweza kuwa ni msaada mkubwa unaotoa fursa ya watu kukutana na kwamba, njia za mawasiliano kwa hakika ni zawadi kutoka kwa Mungu.

Baba Mtakatifu anatambua matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika njia za mawasiliano ya kijamii hasa kutokana na kiasi kikubwa cha habari kinachotolewa na watu kushindwa kupata fursa ya kucheua na kutolea maamuzi. Baadhi ya habari zina utata na zinajikita katika masuala ya kisiasa na kiuchumi. Njia za mawasiliano ya kijamii zina mchango mkubwa katika kukuza ufahamu wa watu au kuwavuruga; kuwaunganisha au kuwatenganisha.

Ikumbukwe kwamba, kuna watu ambao kutokana na sababu mbali mbali hawana nafasi katika matumizi ya mitandao ya kijamii, changamoto ya kutambua kwamba, mawasiliano ni jambo la kibinadamu na wala si tu katika maendeleo ya digitali, jambo linalohitaji ukimya, usikivu, uvumilivu kutokana na tamaduni pamoja na mapokeo mbali mbali. Waamini wajifunze kuthamini na kuenzi tunu msingi za maisha ya binadamu zinazopata chimbuko lake katika Ukristo, hasa kuhusiana na utu na heshima ya binadamu; asili ya ndoa na familia, tofauti kati ya dini na siasa pamoja na mshikamano unaoongozwa na kanuni ya auni.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, utamaduni wa kukutana unajikita katika dhana ya mtu kumtambua jirani yake katika mazingira yanayoundwa na ulimwengu wa digitali kwa kuwa Wasamaria wema, ili kushiriki katika shida na mahangaiko ya wengine, kwani wote ni watoto wa Mungu. Nguvu ya mawasiliano inajidhihirisha katika ujirani.

Mawasiliano yanayojikita katika kuwavuruga na kuwachanganya wengine kama inavyojionesha kwenye mfano wa Msamaria mwema, kwa baadhi ya watu ndani ya jamii kutoguswa na mahangaiko ya jirani zao kwa sababu mbali mbali kuna hatari kwamba, watu wakashindwa kuwaona jirani zao! Haitoshi kila wakati watu kuwa wameunganika kwenye mitandao, lakini wanapaswa kukutana kweli kweli kwa kupenda na kupendwa pamoja na kufarijiwa.

Kwa bahati mbaya mikakati ya vyombo vya mawasiliano havipanii sana kuonesha uzuri, wema na ukweli katika mawasiliano, changamoto kwa vyombo hivi kuonesha ubinadamu na huruma ili kuwaunganisha watu na wala si waya na kwamba wadau wa njia za mawasiliano wanaweza kuwa ni msaada na rejea kwa wengine, watu wanaoaminiwa katika mawasiliano. Ushuhuda wa Kikristo katika mitandao ya kijamii ni muhimu sana ili kuwafikia hata wale walioko pembezoni mwa jamii!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna umati mkubwa wa watu wanaoishi pembezoni mwa jamii, hawa ndio wanaopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na kwamba, mchakato huu unaweza kukolezwa kwa njia ya mitandao ya kijamii; hawa ni watu wenye madonda wanaohitaji, faraja na matumaini. Kwa njia ya njia za mawasiliano ya kijamii ujumbe wa Kikristo unaweza kufika hata miisho ya dunia. Makanisa na mitandao ya kijamii, iendelee kuwa wazi ili watu waweze kuingia na kujichotea utajiri wa Neno la Mungu.

Mawasiliano ya kijamii iwe ni fursa ya kuelezea wito wa kimissionari unaofumbatwa na Mama Kanisa, ili kuwasaidia watu kutambua uzuri wa imani pamoja na kukutana na Yesu Kristo. Hata katika uwanja wa mawasiliano ya jamii, Kanisa halina budi kusaidia kuleta joto na kuamsha ari miongoni mwa watu, kwa kuonesha uwepo katika kutafuta ukweli na maana ya maisha ya mwanadamu. Kanisa halina budi kujenga utamaduni wa majadiliano, ili kuwafahamu watu, kujua matumaini na mashaka yao, ili hatimaye, kuwapekea Injili, Yesu Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, akateswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Watu wawe makini na matukio mbali mbali yanayowazunguka hasa katika maisha yao ya kiroho. Majadiliano ya kweli yanajikita katika kuaminiana na kuthaminiana katika mchakato wa kushirikishana mawazo kwani hakuna mtu anayeweza kujidai kwamba mawazo yake ndiyo ya kweli tu!

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa siku ya 48 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa kuwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwangalia Msamaria mwema, ili aweze kuwa ni mfano bora wa kuiga katika kuganga madonda ya watu na kuufurahisha moyo. Watu waguswe na mwanga wa upendo na huruma, ili kwa pamoja waweze kuwa kweli ni raia wa ulimwengu wa digitali.

Kanisa halina budi kuwepo katika mitandao ya kijamii ili kushiriki katika mchakato wa majadiliano na watu wa dunia ya sasa ili waweze kukutana na Yesu. Kanisa lijitahidi kuwa ni mwenza wa safari katika maisha ya mwanadamu. Mabadiliko na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika njia za mawasiliano ya jamii ni changamoto kubwa inayopaswa kufanyiwa kazi na Kanisa kwa kuwa na nguvu mpya ili kuwashirikisha wengine uzuri wa Mungu.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.



No comments:

Post a Comment