Sunday, June 1, 2014

Ni kiongozi asiyetaka makuu!


Kardinali George Pell, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya uchumi mjini Vatican, akihojiwa na gazeti moja kutoka Hispania anasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anaishi maisha ya kawaida pasi na makuu kama kielelezo cha kumwilisha ufukara katika maisha na utume wake kiasi kwamba amevunjilia mbali kuta za utengano zilizokuwepo kabla ili kukutana, kuonana na kuzungumza na watu!

Kardinali Pell anasema, kuna baadhi ya vyombo vya upashanaji habari ambavyo vinajadili juu juu kuhusu mafundisho tanzu ya Baba Mtakatifu Francisko katika ulimwengu mamboleo: masuala kama uchu wa mali na madaraka; utamaduni wa kifo unaokumbatia sera za utoaji mimba; umuhimu wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kwa baadhi ya vyombo vya habari kwao hii si habari inayouzika na matokeo yake wanataka kupindisha habari kuhusu mafundisho ya kweli ya Papa Francisko, kwa ajili ya mafao yao binafsi.

Hii ni changamoto kubwa kwa vyombo vya upashanaji habari kujitahidi kuingia katika kiini cha Mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko, kwa kutambua kwamba, ni kiongozi anayependa kutolea ushuhuda wa kweli za Kiinjili si tu kwa maneno bali hata katika mtindo wa maisha yake! Ni kiongozi anayetangaza Injili ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji. Ni Mtawa aliyefundwa katika maisha na kanuni za Wayesuit wa zama hizo ndiyo maana anajisadaka bila hata kujihurumia. Kwake hakuna mapumziko wala kuponda mali! Kazi hadi kieleweke!

Kardinali Pell anasema kwamba, Baba Mtakatifu katika mikakati ya utekelezaji wa dhamana yake anakazia umuhimu wa umoja na mshikamano katika kupanga, kuamua na kutekeleza vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa, ndiyo maana ameamua kuunda Tume ya Makardinali kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaomsaidia kufanya marekebisho katika Sekretarieti ya Vatican. Anaendelea kutekeleza changamoto zilizotolewa na Makardinali wakati wa mikutano yao elekezi kabla ya uchaguzi wa Papa Francisko.

Kardinali George Pell anasema, Baba Mtakatifu anataka kuona masuala ya ukweli, uwazi, uadilifu na weledi yanafanyiwa kazi katika huduma mbali mbali zinazotolewa na Kanisa. Sekretarieti ya Uchumi inaundwa na Makardinali wanane na waamini walei saba, wote wakiwa na kura sawa katika maamuzi yanayotolewa na Sekretarieti hii. 

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment