Thursday, June 26, 2014

Vatican imetoa Hati ya kufanyia kazi Sinodi maalum juu ya familia



Alhamisi hii Juni 26, 2014, Vatican ilitoa muhtasari wa hati ya kufanyia kazi Sinodi Maalum ya Maaskofu, iliyotangazwa na Baba Mtakatifu Novemba 2013 juu ya “changamoto za Kichungaji ndani ya Familia katika mtazamo wa Uinjilishaji mpya , itakayo fanyika OKtoba mwaka huu. Sinodi hii ya mwezi Oktoba,inalenga kutoa mapendekezo yatakayofanyiwa kazi pia katika Mkutano mwingine wa Sinodi ya kawaida ya Maaskofu ya mwaka 2015. Hati hii imetolewa na Ofisi ya Kardinali Lorenzo Baldisseri ambayo itafanya mapitio ya majibu katika aswali 39 yaliyofanyiwa uchunguzi katika hati ya kisairia.

Hivyo hati ni matokeo ya utafiti uliofanywa katika makanisa kadhaa Katoliki juu ya changamoto zinazokabili familia kwa wakati huu na msaada unaoweza kusaidia kupunguza makali ya matatizo katika familia. Kiini cha majadiliano ya Maaskofu kwa mujibu wa hati inaonyesha maeneo muhimu yatakayofanyiwa kazi na sinodi katiak mtazamo wa Unjilishaji ndani ya familia na hasa kazi za kichungaji kwa familia mbele ya changamoto mpya, elimu ya maisha na imani.

inatazamiwa muhtasari wa majibu ya maswali juu ya masuala ya ndoa, familia na, maudhui yake yatatolewa chini ya Mada Mbiu: “Changamoto za Kichungaji kwa familia katika mazingira ya Uinjilishaji. Hii ni sinodi maalum itakayo jaribu kutoa majibu katika haja za kidharura lwa ajili ya kusalimisha hadhi na uwepo wa familia. Kazi yake msingi itakuwa ni kutathmini na kuchunguza habari zilizopatikana kutoka katika Makanisa kadhaa maalum, na kutoa mwongozo wa kichungaji, utakao jadiliwa pia katika Sinodi ya kawaida ya Oktoba ya mwaka 2015, chini ya Mada: Yesu Kristo ataonyesha siri na wito wa familia.

Hati hii ya kufanyia kazi , imegwanyika katika vifungu vitatu vikuu, kwanza ikiwa uinjilishaji ndani ya familia. Majadiliano ya mababa wa Sinodi, yatalenga zaidi katika mwanga wa Ukweli wa Biblia kwenye asili ya tangu kuumbwa kwa mwanadamu, kwamba Mungu alimuumba mwanamme na akaumba mwanamke na wote, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, na Mungu aliwabariki kwamba watakaa pamoja na wataongezeka kwa kuzaa watoto . na hivyo binadamu anakuwa ni msaidizi wa Mungu katika kuyapokea , kuyatetea na kueneza maisha.

Mababa wa Sinodi watafanya rejea katika nyaraka mbalimbali za Kanisa juu ya Mada hii ya familia, kama waraka Humanae Vitae wa Papa Paulo VI. Pia hati ya kufanyia kazi, inatambua ukosefu wa elimu miongoni mwa waamini, hasa kutokana na mafunzo duni kwa Mapadre juu ya familia na hivyo wengi wao hawajui jinsi ya kukabiliana vikwazo na changamoto zinazojitokeza kwa katika njia ya haki, kwa familia yenye ndoa , hasa kuhusiana na nyanja ya kujamiiana na uzazi. Mafundisho ya Kanisa juu ya somo hili yanapaswa kukubaliwa kwa uaminifu, na hivyo ni kusema ndiyo, katika kazi za kutetea na kulinda hadhi ya maisha ya binadamu, wakati wa upinzani dhidi ya mafundisho juu ya kudhibiti uzazi, talaka au mahusiano kabla ya ndoa.

Hati inazamisha kwa kina sababu msingi katika matatizo yaliyopo kwenye familia za ndoa leo hii kwamba, ni pamoja na mazingira ya kukua kwa mapenzi ya ubinafsi, mali, utamaduni wa talaka katika jamii ya kisasa. Hivyo, kuna haja ya kutafuta njia mpya, lugha mpya ya kufikisha mafundisho ya Kanisa katika eneo hilo, kuwaunda vyema mapadre katika kazi zao cha kichungaji kwa ajili ya familia. Sehemu hii ya kwanza hasa inalenga katika umuhimu wa maandalizi mazuri kwa wanaotarajia kufunga ndoa, uendelezaji wa ucha Mungu ndani ya familia na roho wa kweli wa kitume katika familia.

Sehemu ya pili ya hati hii ya kufanyia kazi, "Instrumentum laboris", uchungaji wa familia katika uso wa changamoto mpya" - baada ya kusema umuhimu wa maandalizi ya ndoa, uendelezaji wa ucha Mungu maarufu na msaada wa familia na roho wa kweli wa kitume kwa familia.

Pia Mababa wa Sinodi watatafakari pia juu ya changamoto ya kichungaji leo hii, katika muono wa hali halisi kwamba . kuna hali nyingi muhimu zinazopambana na uso wa familia leo, ikiwemo : kushuka kwa heshima ya baba katika familia, utengano unaotokana na ukosefu wa kuzingatia maagano ya ndoa na hivyo kudai talaka kwa sababu tu ya kuchokana, vurugu na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto, tamaa ya fedha inayo ingiza watoto katika biashara ya ukahaba, madawa ya kulevya, ulevi, mapenzi ya mchezo wa kamari, madawa ya kulevya na mitandao ya kijamii yenye kuchochea wanandoa kutalakiana na kadhalika. Pia matokeo ya wanandoa iwe wote au mmoja wao kwa kubaki kwa muda mrefu kazini, uhaba wa kazi, ukosefu wa pumziko ya Jumapili na mengine mengi yanayozuia nafasi ya kuwa pamoja kama familia.

Na Kanisa, kwa hiyo, linatarajiwa kutoa msaada wake halisi wa maelekezo katika kukabiliana na changamoto hizi. Sababu nyingine muhimu ni uhamiaji, kwa ambayo inasisitiza juu ya haja ya kuwezesha kuungana kwa familia; umaskini; ulaji; vita; utofauti wa ibada kati ya wanandoa hivyo ugumu wa kuelimisha watoto wao; mbinu na za kuzuia magonjwa , hasa UKIMWI. Pia jinsi ya kukabiliana na kashfa ya ngono kwa wafanyakazi wa Kanisa, picha za aibu kwa watoto , upayukaji wa Mapadre wanaoshindwa na maisha ya useja na hivyo kuchukua mtazamo mwingine wa maisha ya ndoa, pia athari za wazazi waliotalakiana au malezi ya mzazi mmoja.

Katika hati hii ya kufanyia kazi , inaonyesha kwamba Kanisa si hakimu wa mabaya yanayofanyika lakini mama ambaye daima yu karibu na hushauri watoto wake kubainisha yaliyo mema na mabaya na kama ni jambo la hatari kuishi bila huduma ya sakramenti , kwa kuwa ni kujiweka mbali maisha ya Kikristo na uhusiano na Mungu.

Sehemu ya tatu ya hati – NI “Uwazi katika maisha na wajibu wa elimu" - mada ambayo katika mafundisho ya Kanisa, hasa juu ya uwazi na maisha kwa upande wa mume na mke, yanaguswa kidogo sana katika mtazamo wake chanya. Awali ilionekana kama ni kuingilia ndoa na kama kikwazo katika uhuru na ufahamu wa wana ndoa. Hivyo, Mababa wa Sinodi kwa sasa wana kazi ya kuchambua kwa kina hoja nyingi zenye kutatiza kama uzazi wa mpango na ukweli wa njia asili za kusimamisha uzazi, kuheshimu utu na mazingira ya kibinadamu katika uhusiano wake wa kimapenzi kati ya mume na mke.

Pia Maaskofu watajadili na kutolea maamuzi ya pamoja juu ya njia za kuzuia dhidi ya UKIMWI. Kanisa linahitaji kutoa maelezo thabiti juu ya msimamo wake, pia kujibu baadhi ya maswali yanayo jitokeza mara kwa mara katika vyombo vya habari juu ya masuala ya "kitalaamu yanayohusiana na ambukizo la maradhi haya ya ukimwi.

Aidha Mababa wa Sinodi Maalum, watazungumzia umuhimu na thamani ya wajibu wa wasimamizi wa ubatizo au kipaimara katika safari ya imani kwa watoto na vijana, na wakati maalum wa lkutoa msaada kichungaji unao hitajika kwa ajili ya ndoa mchanganyiko na kukosekana kwa usawa wa ibada.

Hati ya kufanyia kazi , inamalizia kwa maombi ya Papa Francisko ,aliyoyatoa wakati wa sala ya malaika wa Bwana , tarehe 29 Desemba, 2013, ambayo ilikuwa ni Sikukuu ya Familia Takatifu ya Nazareti, ambamo pia alitangaza uwepo wa sinodi Maalum kwa ajili ya familia mwezi Oktoba 2014, ambayo itaongozwa na Mada: "Changamoto ya Kichungaji , kwa familia katika mazingira ya uinjilishaji.

Sinodi hii inatajwa kuwa Sinodi maalum kwa kua inafanyika katika misingi ya dharura ya kutoa majibu ya haraka kwa kanisa juu ya changamoto za leo zinazo pambana na familia za Kikristo na kanisa kwa ujumla. Matokeo ya inodi hii maalum ya Oktoba 2014, yatatumika katika kuandaa hati nyingine ya kufanyia kazi Mkutano wa Sinodi ya kawaida ya mwaka 2015, ambayo itakayoongozwa na Mada: Yesu Kristu ataonyesha siri ya fumbo la familia na miito katika familia.

Habari kwa hisani ya radio vatican


No comments:

Post a Comment