Wednesday, July 23, 2014

Silaha na nishati ya nyuklia bado ni tishio kwa usalama wa binadamu!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC linaendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kusitisha utengenezaji, ulimbikizaji na matumaini ya silaha za kinyuklia ili kuiokoa dunia kutokana na hofu ya maafa makubwa yanayoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya silaha za kinyuklia. RealAudio
MP3

Ushuhuda unaoendelea kutolewa na wahanga wa mashambulizi ya silaha za kinyuklia Nagasaki na Hiroshima kunako mwaka 1945 na kuvuja kwa mtambo wa nyuklia wa Fukushima kunako mwaka 2011 unaoendelea kuongeza hofu na wasi wasi kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linayataka Makanisa wanachama kuendesha kampeni dhidi ya utengenezaji wa silaha za kinyuklia inayoongozwa na kauli mbiu “Ulimwengu pasi na silaha za Kinyuklia”. Makanisa yanapaswa kupambanua kwa kina na mapana, kimaadili na kitaalimungu athari za matumizi ya silaha na nishati za kinyuklia.

Waoneshe ushuhuda unaotolewa na wadau mbali mbali kuhusiana na matumizi ya nishati ya kinyuklia pamoja na kuendelea kutoa ushawishi wa kuridhia upigaji rufuku wa utengenezaji, matumizi na ulimbikizaji wa silaha za kinyuklia duniani. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linayahimiza Makanisa wanachama kufanya mabadiliko ya ndani katika maisha yao, kwa kutumia nishati rafiki ili kulinda na kutunza mazingira.

Baraza la Makanisa ulimwenguni linabainisha kwamba, matumizi ya nishati ya kinyuklia ni hatari kwa usalama na maisha pamoja na maendeleo ya binadamu. Serikali mbali mbali zinazoendeleza sera ya matumizi ya nishati ya kinyuklia zinahatarisha ustawi wa wengi kwa kutumia rasilimali fedha ya umma kwa ajili ya kuendeleza sekta binafsi.

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment