Saturday, August 9, 2014

Kardinali Filoni, kumwakilisha Papa Francisko nchini Iraq, ili kuonesha mshikamano wake wa dhati!

Baba Mtakatifu Francisko, huku akiwa ameguswa kwa namna ya pekee kabisa na mahangaiko pamoja na mateso ya Wakristo pamoja na watu mbali mbali wanaolazimika kuyakimbia makazi yao huko Iraq kutokana na madhulumu, vita na nyanyaso za kidini, amemteua Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu kumwakilisha nchini Iraq, kama kielelezo cha mshikamano wa dhati katika maisha ya kiroho na Wakristo pamoja na wote wanaoteseka nchini Iraq kutokana na vita inayoendelea huko.

Huu ni mshikamano wa Mama Kanisa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake au kutokana na sababu mbali mbali! Kardinali Filoni anasema kwamba, Baba Mtakatifu ameonesha imani kwake binafsi, lakini zaidi anaguswa na mahangaiko ya wananchi wa Iraq ambao kwa sasa wanakabiliwa na hali ngumu sana ya maisha kutokana na vita inayoendelea nchini humo.

Watu wengi wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao na kwa sasa wanaishi kama wakimbizi hata katika nchi yao wenyewe. Kardinali Filoni anasema, akiwa nchini Iraq atazungumza na viongozi wa Makanisa, ili kuangalia ni mambo yepi wanayoweza kutenda kwa pamoja. Hali ni ngumu hata namna ya kufika nchini humo, lakini hakuna sababu ya kuwa na woga wala wasiwasi, Kanisa litafanya kile kinachowezekana.

Kardinali Filoni anasema, hii si mara ya kwanza kwa Wakristo nchini Iraq kulazimika kuyakimbia makazi yao. Mateso na mahangaiko ya Wakristo huko Iraq yanafahamika kihistoria na kwamba, hii ni Jumuiya ambayo imeendelea kubeba ndani mwake Msalaba na kuifuata ile Njia ya Msalaba.

Hija yake nchini Iraq anasema Kardinali Filoni inapania kuonesha mshikamano wa Baba Mtakatifu Franciko kwa Wakristo huko Iraq, ambaye anaendelea kuwasindikiza katika mateso na mahangaiko yao kwa njia ya sala na sadaka yake takatifu. Kardinali Filoni anasema, atawasilisha ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa Wakristo wa Iraq.

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Filoni kutokana na uzoefu wake mkubwa huko Mashariki ya Kati, kwani amewahi kuwa Balozi wa Vatican nchini Jordan na Iraq kwa muda wa miaka saba. Ni kiongozi aliyeonja adha ya vita wakati wa utawala wa Rais Saddam Hussein, lakini akabaki, akiwa ameshikamana kwa dhati na wananchi wa Iraq katika kipindi hiki kigumu.

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment