Saturday, August 9, 2014

Tarehe 10 Agosti, 2014 ni siku ya kuombea amani, umoja na mshikamano wa kitaifa Korea!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni linayaalika Makanisa wanachama kushikamana kwa njia ya sala, ili kuombea, amani, umoja na mshikamano kati ya Korea ya Kusini na Korea ya Kaskazini, Jumapili tarehe 10 Agosti 2014.

Huu ni mwendelezo wa Mapokeo kwa ajili ya kuomba umoja na mshikamano wa kitaifa kila Jumapili ya Mwaka kabla ya tarehe 15 Agosti, Siku ambayo Korea ya Kusini na Korea ya Kaskazini zinasherehekea Siku kuu ya Ukombozi.

Itakumbukwa kwamba, Korea ilijipatia uhuru wake kutoka kwa Mjapani kunako tarehe 15 Agosti 1945, lakini hii pia ndiyo siku iliyoisambaratisha Korea na kujikuta imegawanyika sehemu kuu mbili, yaani Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini. Kusali kwa ajili ya kuombea amani na mshikamano wa kitaifa ni kielelezo cha hali ya juu kinachoweza kuoneshwa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni.

Huu ni mwendelezo wa maazimio ya mkutano mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni uliofanyika mjini Busan, Korea ya Kusini, ili kuendelea kuunga mkono hija ya maisha ya kiroho inayofanywa na Korea hizi mbili katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maisha.

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment