Ukristo
BWANA YESU |
Dini hiyo, iliyotokana na ile ya Wayahudi, inayolenga kuenea kwa binadamu wote, na kwa sasa ni kuu kuliko zote duniani, ikiwa na wafuasi zaidi ya bilioni mbili.
Kitabu chake kitakatifu kinajulikana kama Biblia. Ndani yake inategemea hasa Injili na vitabu vingine vya Agano Jipya.
Yaliyomo |
[hariri] Asili
Chimbuko la Ukristo ni kuwepo kwa mtu aliyezaliwa takriban miaka 2000 iliyopita huko Mashariki ya Kati, katika kijiji cha Bethlehemu kilichopo hadi hivi leo kwenye mipaka ya Palestina, naye alikuwa akiitwa Yesu wa Nazareti au mwana wa Yosefu mchonga samani; mama yake akifahamika kwa jina la Bikira Maria.[hariri] Masiya Yesu
Ukristo ni matokeo ya utume wa Yesu, uliopokewa na waliomwamini kuwa ndiye Masiya, yaani Mpakwamafuta (Kristo kwa Kigiriki), mkombozi aliyetimiliza ahadi za Mungu kwa uzao wa Abrahamu.Utabiri wa kuja kwake ulianzia katika bustani ya Edeni pale Mungu alipomwambia mwanamke "uzao wako utamponda kichwa" nyoka, yaani shetani.
Musa, mwanamapinduzi aliyewakomboa watu wa Israeli kutoka utumwani Misri takribani miaka 1250 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu, ndiye nabii wa kwanza kutabiri wazi ujio wa Masiya au Kristo (Kumbukumbu la Torati 18:15-22, hususan mstari 18: "Nitawainulia nabii kama wewe kutoka miongoni mwa ndugu zenu; na nitatia neno langu kinywani mwake na atasema nao yote niliyomwamuru."
Kuja kwake kulitimia katika Agano Jipya, ambalo ni ukamilifu wa yote yaliyotabiriwa katika Agano la Kale. Kwani Musa alitumwa kuanzisha Agano la Kale kama maandalizi ya Agano Jipya, akikabidhi mifumo mingi ya nje na ndani kwa watawala na waamuzi waliomfuatia watakaoshikilia Agano la kusubiri Masiya wakishirikiana na manabii na makuhani.
Yesu alizaliwa miaka kama 1800 baada ya Abrahamu. Vitabu vya Injili vinaeleza matukio na mafundisho ya Yesu ambayo ndiyo mwongozo wa imani hiyo. Maisha na kazi ya Yesu yameibua mambo mengi katika historia. Ndiyo sababu kalenda iliyoenea duniani huhesabu miaka kutoka ujio wake; huu ni mchango mmojawapo wa Ukristo.
[hariri] Mafundisho ya msingi ya Yesu
Yesu alifanya ishara za kustaajabisha, au miujiza. Matokeo ni kwamba, watu wengi wakamwamini. Nikodemu, mshiriki mmojawapo wa baraza la Sanhedrini, ambayo ilikuwa pia mahakama kuu ya Kiyahudi, alivutiwa na kutaka kujua zaidi kuhusu siri ya miujiza hiyo na ujumbe kutoka kwa Mungu; kwani yeye alihamasika kuona ishara zile kutoka kwa Mungu. Yesu akamjibu kwamba hakika mtu hawezi kuingia ufalme wa Mungu asipozaliwa mara ya pili kwa maji na Roho. Pia akajieleza kuwa mpatanishi wa ulimwengu wa dhambi na Mungu na kwamba kila anayemgeukia kwa imani hatapotea, bali atarithi uzima wa milele: Kristo ni mfano wa nyoka wa shaba aliyetengenezwa na Musa. (Yohana 2:23-3:21; Hesabu 21:9).Akiwa akitembea kando ya Ziwa la Galilaya, Yesu alikuta umati wa watu umekusanyika. Basi akapanda mashua na kuenda mbali kidogo na ufuoni, akaanza kuwafundisha kuhusu Ufalme wa Mbingu kupitia mfululizo wa mifano. Mmojawapo ni hili lifuatalo: Ufalme wa Mbingu ni kama punje ya haradali ambayo mtu anaipanda. Ingawa ni mbegu ndogo sana inakua na kuwa mti wa mboga kubwa kuliko yote. Inakua mti ambao ndege wanauendea, wakipata makao katika matawi yake. (Mathayo 13:1-52; Marko 4:1-34; Luka 8:4-18; Zaburi 78:2; Isaya 6:9,10).
[hariri] Maana ya Kristo
Mtume Paulo anazungumza hivi kuhusu Kristo:Walakini iko hekima tusemayo kati ya wakamilifu; ila si hekima ya dunia hii, wala ya hao wanaotawala dunia hii, wanaobatilika; bali twanena hekima ya Mungu katika siri; ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliazimu tangu milele, kwa utukufu wetu; ambayo wenye kutawala dunia hii hawaijui hata moja; maana kama wangalijua, wasingalimsulubisha Bwana wa utukufu; Lakini, kama ilivyo andikwa:
Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu, mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.
Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho, maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuaye ila Roho wa Mungu. Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua yaliyokirimiwa na Mungu. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamnu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni. Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu, Maana,
Ni nani aliyefahamu nia ya Bwana, amwelimishe?
Lakini sisi tunayo nia ya Kristo. (1 Wakorintho 2:6-16).
[hariri] Kanisa siku za mwanzo
Jumuia ya Wakristo inaitwa Kanisa, lililotajwa na Yesu katika Mathayo 16:18:-Wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu, nitalijenga kanisa langu. Wala milango ya kuzimu haitalishinda.
Ujio wa Roho Mtakatifu
Mara baada ya Yesu kwenda zake katika tukio linalotajwa kupaa kwake mbinguni, wafuasi wake wakarudi Yerusalemu, yapata mwendo wa sabato, na walipoingia huko, wakapanda ghorofani walipokuwa wakikaa Petro na wenzake. Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwapo wote mahali pamoja. Ukaja upepo toka juu kama upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukatokea na ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa na roho mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyo wajalia. (Matendo ya Mitume 1:12-14, 2:1-4).
Hii ilifuatiwa na Petro na wenzake kuanza kuhububiri ufufuko wa Bwana Yesu na hatimaye kugusa wengi. (Matendo ya Mitume 2: 37-40).
Ustawi wa Jumuia ya kwanza ya wafuasi wa Kristo
Na watu walipokuwa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika na matendo mengine; wengi wakaona ishara nyingi basi nao wakauza mali zao, na vitu walivyokuwa navyo, na kugawia watu wote kama kila mtu alivyokuwa na haja. Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakila pamoja na kushiriki kwa moyo mweupe.
Hivyo ndivyo jumuia ilivyozaliwa na kufahamika kama Kanisa. (Matendo ya Mitume 2:42-47).
Kukutanika na kushiriki mafumbo makuu, kushukuru na kusifu, pamoja na uwepo wa karama za Roho Mtakatifu, hufanya Kanisa liwe hai.
Mitume wa Yesu walienea toka Yerusalemu hata Lida, Yafa, Kaisaria, Damasko n.k. na kuanzisha jumuia nyingi. Nazo jumuia kwa bidii za waamini wa mwanzo zikafika Foinike, Kipro, Antiokia, ambako waliitwa Wakristo kwa mara ya kwanza, kutokana na waamini wa mataifa mengine kuwazidi wale wenye asili ya Kiyahudi (Matendo 11:1-23).
Imani na desturi za mikusanyiko hiyo zilitapakaa na hivyo kuanza kusuguana na mapokeo ya jamii mbalimbali zilipopenya. Hii inatokana na ukweli kwamba watu wengi wa siku zile tayari walikuwa na imani zao walizokuwa wakizitunza. Basi ukaja wakati ambao Wakristo wakaanza kukosoana kuhusu dhamira zao na huduma. Ndiyo asili ya nyaraka mbalimbali ambazo zinaunda sehemu muhimu wa Agano Jipya.
[hariri] Mafundisho toka Kanisa la Mitume
Viungo ni vingi, ila mwili ni mmojaMtume Paulo anazungumza hivi:
Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja. (1 Wakorintho 12:12-13). Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha. Je, wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri? Takeni sana karama zilizo kuu. Hivyo nawaonyesha njia iliyo bora. (1 Wakorintho 12:28-31).
Juu ya Wafu, Ufufuko wa Miili na Utukufu Wake
Mtume Paulo anazungumza hivi kuhusu wafu, ufufuko wa miili ya utukufu na roho kwa Kanisa la Korintho:
Lakini labda mtu atasema, 'Wafufuliwaje wafu?' Nao huja kwa mwili gani? Ewe mpumbavu ! uipandayo haihuiki, isipokufa; nayo uipandayo, huupandi mwili ule utakaokuwa, ile chembe tupu, ikiwa ni ngano au nyingineyo; lakini mungu huipa mwili kama apendavyo, na kila mbegu na mwili wake. Nyama yote si nyama moja; ila nyingine ni ya wanadamu, nyingine ya hayawani, mingine ya ndege, nyingine ya samaki. Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani; lakini fahari yake ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali. Kuna fahari moja ya Jua, na fahari nyingine ya Mwezi, na fahari nyingine ya Nyota; maana iko tofauti ya fahari hata kati ya nyota na nyota. Kadhalika na ufufuo wa Wafu. Hupandwa katika uharibifu; hufufuliwa katika kutoharibika; hupandwa katika aibu; hufufuliwa katika fahari; hupandwa katika udhaifu; hufufuliwa katika nguvu; hupandwa mwili wa asili; hufufuliwa mwili wa Roho. Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko. Ndivyo ilivyoandikwa: mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni Roho yenye kuhuisha. Lakini hautangulii ule wa Roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho. Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili ni atoka mbinguni. Kama ilivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni. Na kama tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye wa mbinguni. Ndugu zangu, nisemayo ni haya, ya kuwa nyama na damu haziwezi kuurithi ufalme wa mungu; wala uharibifu kurithi kutokuharibika. Angalieni, nawaambia ninyi siri: Hatutalala sote, lakini sote tutabadilika, kwa dakika moja, kufumba na kufumbua,wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu,nasi tutabadilika. Maana Sharti uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa. Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo ndipo litakapokuwa lile neno lililioandikwa:Hivyo imani katika ufufuko una sura isiyo ya kimaada, tena una fahari kama mambo ya mbingu yenye kudumu zaidi na milele yake.
Mauti imemezwa kwa kushinda. Ku wapi, ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, ewe mauti, uchungu wako?
Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati. Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana Wetu Yesu Kristo! (1 Wakorintho 15:35-57).
Wajibu wa Wakristo
Mtume Paulo anasema hivi kwa Wafilipi:
Basi wapendwa wangu, kama vile mlivyotii siku zote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kutimiza kusudi lake jema. Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano, mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na hila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu, mkishika neno la uzima; nipate sababu ya kuona fahari katika Kristo, ya kuwa sikupiga mbio bure wala sikujitaabisha bure. Naam, hata nikimiminwa juu ya dhabihu na ibada ya imani yenu, nafurahi; tena nafurahi pamoja nanyi nyote. Nanyi vivyo hivyo furahini tena furahini pamoja nami. (Wafilipi 2:12-18).
[hariri] Mafarakano makuu kati ya Wakristo
Katika historia ndefu ya Ukristo, yalitokea mafarakano mengi, waamini wa Yesu wakizidi kutofautiana. Makundi makubwa zaidi ni: Kanisa Katoliki, Makanisa ya Waorthodoksi na madhehebu ya Uprotestanti.[hariri] Wakatoliki
Zaidi ya nusu ya Wakristo wote wanashikamana katika imani na sakramenti chini ya maaskofu wenye ushirika kamili na yule wa Roma, ambaye kwa kawaida anaitwa papa. Kati yao umoja unazingatiwa sana.[hariri] Waorthodoksi na Waorthodoksi wa Mashariki
Wakristo wengi walioishi upande wa mashariki wa Dola la Kirumi na ng'ambo ya mipaka yake walitengana na Wakatoliki hasa katika karne V na karne XI. Hata hivyo msimamo wao wa imani si tofauti sana, kwa kuwa wanachanga mapokeo ya awali ya Kanisa la Mitume na la Mababu.[hariri] Waprotestanti
Utitiri wa madhehebu ya Kiprotestanti ndio wenye tofauti kubwa zaidi kati yao wenyewe na kati yao na Wakristo waliotajwa kwanza. Hiyo ilitokana na msimamo wa msingi wa kutaka kila mmoja aweze kutafsiri Biblia alivyoielewa, bila ya kutegemea mapokeo wala mamlaka ya Kanisa.[hariri] Kanisa leo
Kutokana na historia ya Kanisa kuwa na mchanganyiko wa mazuri na mabaya, wengine wanahisi kuwa halina maana sana. Hali hii inajionyesha hasa pale ambapo waamini wengi wameacha kwenda kanisani isipokuwa siku ya Krismasi na Pasaka au kwenye harusi na misiba.Pia kutokana na mgawanyiko wa madhehebu, kumekuwa na mkanganyiko kuhusu kazi ya Kanisa la leo.
Wakatoliki, Waorthodoksi, Waanglikana, Wamethodisti, Walutheri na wengineo wanafuatilia desturi kama walivyozipokea. Mtiririko wa ibada zao huandikwa na hujulikana kama Liturugia.
Madhehebu mengine, hasa yale ya Kipentekoste, huwa na ibada ambazo hazijaandikwa kitabuni: kiongozi wa ibada wa siku hiyo huja na madondoo yake na mtiririko wa ibada huenda kama "Roho" atakavyoongoza siku hiyo. Kwa sababu hiyo husema kwamba hawafuati desturi au mapokeo. Ukiangalia zaidi utaona kuwa ibada zao pia huwa na mtindo na mtiririko fulani, kama vile kuimba mapambio ya harakaharaka wakiwa wanapiga makofi, kucheza na kurukaruka. Mapambio hayo hufuatiliwa na mengine ya taratibu wakiinua mikono kuabudu. Inawezekana kusema hao nao wana utaratibu au liturugia yao ingawa haijaandikwa kwenye vitabu.
Upande mwingine wanakanisa wanajaribu kuonyesha jitihada zao katika jamii, ikiwa ni pamoja na kuleta amani na maendeleo na kutoa misaada ya kijamii. Kuna uwezekano kwa madhehebu kadhaa kubadilisha mkazo wao kuutoa kwenye imani tu na kuuweka kwenye huduma za jamii au elimu: hii inafanya yaonekane kama moja ya mashirika ya hisani.
Binadamu wa karne ya 21 wanahitaji jibu litakalosaidia kuwakwamua kutoka matatizo yao. Wenye dini mbalimbali, hususan Wakristo, wanadai kujua ufumbuzi wa matatizo makuu ya binadamu, ingawa wachache tu wameweza kuonyesha dhahiri matatizo yaliyotatuliwa kabisa kwa dini. Wakati mwingine wanadini wenyewe wamekuwa chanzo cha matatizo badala ya kuyatatua.
Jibu linaweza kupatikana katika maneno ya Yesu mwenyewe, aliposema kwamba wafuasi wake ni chumvi ya dunia, ambayo ilete ladha katika maisha ya watu, lakini kama chumvi hiyo inapoteza ladha yake, haifai kitu, isipokuwa kutupwa na kukanyagwa kwa dharau. Hivyo changamoto ya Wakristo ni kufuata vema mafundisho ya imani yao ili kukidhi hitaji la nyakati hizi la kuishi kwa amani, furaha na upendo duniani kote .
[hariri] Kurudi Kwa Kristo
Ni imani ya Wakristo, lakini pia ya Waislamu, kwamba Yesu atarudi duniani kwa utukufu, ingawa jambo hilo linatafsiriwa kwa namna tofauti.[hariri] Mfanano na dini nyingine
Ukristo na UyahudiNi wazi kuwa Ukristo unahusiana zaidi na dini ya Kiyahudi, kwa sababu unatokana nayo na kutumia vitabu vyake vitakatifu Tanakh. Haiwezekani kumuelewa Yesu kwa kumweka nje ya mazingira ya Kiyahudi.
Dini hizo mbili zilitengana moja kwa moja miaka 50 hivi baada ya Yesu kuaga dunia. Ni kwamba Wayahudi katika mkutano wa Jabneh (mwaka 80 hivi B.K.) waliamua kuwatenga kama wazushi wananchi wenzao waliomuamini Yesu, hasa baada ya kuona hawakusaidia vita vya ukombozi dhidi ya wakoloni Warumi vilivyosababisha maangamizi ya Hekalu na mji wa Yerusalemu mwaka 70 B.K. Tangu hapo Wakristo hawakushiriki tena ibada pamoja na Wayahudi, wakazidi kuzingatia sakramenti ya Kumega Mkate katika Siku ya Bwana (Jumapili, siku inaposadikika Yesu alifufuka) badala ya Sabato (Jumamosi, siku ya pumziko ya Wayahudi). Kabla ya hapo Wakristo wa Kiyahudi walikuwa wanashika siku zote mbili.
Ukristo na Ubuddha
Hakuna uhusiano wa kihistoria kati ya Yesu na Ubuddha. Hata hivyo mambo kadhaa yanafanana.
Yesu alifundisha kuhusu nidhamu mbili zinazompelekea mtu kuwa mwadilifu na hatimaye kuurithi utukufu wa kiroho ambao karama yake ni uzima wa milele: hizo ni kumpenda Mungu kwa moyo wako wote na kwa akili yako yote na jirani yeyote kama unavyojipenda mwenyewe. Buddha alifundisha hali ya kutodhuru viumbe hai wowote, tena kuwa na moyo mkuu wa mapenzi kwa vitu vyote. Hii ni miongozo inayolenga mtu atambue tabu anazodumisha yeye mwenyewe, kwa matendo yake na upeo ulio na mipaka, katika maisha yake ya kila siku.
Baada ya hili, mafundisho ya Kristo yanatofautiana katika kuchukulia hali hii. Kwa mujibu wa Kristo, dhambi, matendo yenye kukosea kanuni za kiroho na hata za kimaumbile, hufutwa na Kutubu; wakati katika mafundisho ya Buddha, makosa yote yanatokana na kotokuwa makini. Hivyo, kwa mujibu wa Buddha, njia pekee ya kumkomboa mtu na shida zake ni kufuata mwongozo wa Nguzo Nane ambazo humweka katika hali ya kuweza kuamka kiroho wakati utulivu wa kimwili na kiakili unapofikiwa. Haya ndiyo yanayofanya Ubuddha kuwa ni njia inayojali sana nidhamu ya mtu kimatendo, wakati Ukristo hufuata sana moyo wenye kukiri makosa, na kutafuta uadilifu wa kweli wa kiroho. Huu ni uzuri wa pekee kutoka kwenye mafundisho ya Yesu: Tubuni kwa kuwa saa ya ukombozi ni sasa...
Jingine lenye tofauti ni kuwa Kristo hufundisha kuhusu Upendo kwamba ni Mungu, kwa kuwa Upendo una maana kuliko hekima yote ya mwanadamu, nao ndio unaounganisha na kutunza vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Hilo hutambulika kupitia Kristo ambaye hujidhihirisha kwa yule mwenye kupokea Roho wa Mungu. Upande wa Buddha, hukanusha nafsi na pia Mungu, akisema: Ni Buddha mwenye ufahamu wa milele, tena hana nafsi isipokuwa Utupu; na ni wenye furaha isiyo kifani izidiyo yote yenye kufanyika ulimwenguni, yaani Nirvana; kila mtu ni Buddha aliyesahau asili yake ya ndani kabisa.
Ukristo na Uislamu
Ukristo na Uislamu vinafanana zaidi kwa sababu Muhammad alifahamu Wayahudi na Wakristo wengi katika nchi yake na katika safari zake. Dini hizo zinajulikana kwa kushika imani katika Mungu Pekee, muumba wa vitu vyote.
Mafundisho ya msingi ya Uislamu ni unyenyekevu kwa Mola mmoja aitwaye Allah , mwingi wa rehema na mwingi wa fadhila; nguzo ya Uislamu ni kumuabudu. Katika Uislamu, unyenyekevu wa mtu katika kumcha Mola kwa ibada na swala humpa kukirimika na kuhifadhika kwa Mola wake mwenye fadhila, ambaye atamtunuku haki yake. Naye mnyenyekevu kwa Mola ataishi kuona utukufu mwingi wa Mola wenye kutajwa katika Kurani kwa majina 99 ya Allah. Kati ya sifa na utukufu huo ulio na majina mengi, baadhi yake ni Al Rahman (kwa Kiarabu, "mwenye rehema"), Al Nur ("Mwenye Nuru") n.k. Hayo hufanana na neno la Nuru ya Bwana, rehema na ukombozi kuwa utukufu wa Mbingu katika mwongozo wa Kikristu.
Pia Uislamu unafundisha udugu miongoni mwa Waislamu yaani mzizi wa neno linalotumika sana katika Kuran: Waly (Wala, Wilayat, Mawla, Awla) katika kueleza jinsi Mwislamu apasavyo kuishi karibu na mwenzake. Nalo husisitiza upendo na kulindana kwa heri na pia kuepushana na shari. Hilo linafanana na upendo ambao katika Ukristo ndio adili kuu kuliko yote:
Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo... mimi si kitu kabisa. (1 Wakorintho 13:1-11).Lakini katika Ukristo upendo hauna mipaka wala masharti. Unatakiwa kuenea kwa maadui pia na kusamehe kila mara kufuatana na mfano wa Baba wa Mbinguni.
Mwislamu kadiri ya wingi wa unyenyekevu na usafi wa moyo wake huakisi sifa za Mola wake. Uislamu hufundisha kuhusu vita vya ndani ambavyo muumini hupigana na nafsi yake yenye matamanio ya chini, ambayo huzaa chuki, dhuluma, wivu, na maovu mengine ili kuishinda kwa utukufu wa Mola na kudumisha dini (mwongozo) yake katika ngazi zote za maisha. Kabla yake Yesu alihimiza wote wafuate mfano wake wa upole na unyenyekevu wa moyo, akitoa kielelezo katika Heri Nane za hotuba ya mlimani. Tofauti ya msingi ni kuwa kwa mujibu wa Kristo, ni kwa neema ya imani katika Neno la Uzima kwamba mtu hukombolewa kutoka matamanio yake ya kibinadamu, mbali ya kwamba anapaswa kujitahidi asije akapotewa na neema hiyo na kurudia utumwa wa dhambi.
Maandishi yanapatikana chini ya leseni ya Creative Commons Attribution/Share-Alike License; matakwa mengine yanaweza kutakiwa. Tazama maelezo zaidi ya Matakwa ya Utumiaji.
No comments:
Post a Comment