Monday, February 3, 2014

Mchakato wa kukutana na Yesu!


Kadiri ya misale ya mwaka 1962 ya Papa Yohane 23 kipindi cha noeli kinaisha kwa sikukuu ya leo. Lakini baada ya marekebisho ya kalenda mwisho wa kipindi cha Noeli ni baada ya Sikukuu ya Epifania, yaani baada ya sikukuu ya ubatizo wa Bwana wetu. Aidha, ni mwisho wa kipindi cha Epifania.

Zamani sikukuu hii ilijulikana kama sikukuu ya Mweuo wa Bikira Maria, lakini sasa ni “Kutolewa Bwana”. Kabla kabisa sikukuu hii ilikuwa inaadhimishwa huko kwenye Kanisa la Mashariki likijulikana kama sikukuu ya Maonano, au sikukuu ya kukutana kwa kigiriki wanaita Hypapante; au kwa kimombo ni “encounter”.

Ni kutokana na maana hiyo ya kukutana tarehe 6 Januari mwaka 1997, Papa Yohane Paulo II akaiweka tarehe 2 Februari kuwa ni siku rasmi kwa watawa kiulimwengu. Yaani ni Sikukuu ya wale wanaofuata maisha ya wakfu. Siku hiyo watawa hukutanika na kuisherekea siku hiyo pamoja kwa sala. Hadi siku leo zimeshapita siku 40 tangu tusherehekee Noeli. Leo ndiyo Kanisa linatuletea sherehe ya kuonana au kukutana.

Ni siku rasmi ya kukutana na huyu mgeni aliyetufikia. Muda wote huu alikuwa na wazazi tu na majirani wa karibu. Kuhusu mahali pa kukutana na mgeni huyu, Mwinjili Luka anatutolea uvivu wa kumfuata nyumbani, bali anatuletea mtoto hekaluni, ambako wazazi wake. Mungu aliyekuwa anasubiriwa na taifa lake sasa amejileta mwenyewe hapo Hekaluni. Kwa sikukuu hii mnaalikwa nyote mkitaka kukutana na mtoto Yesu nendeni hekaluni huko ameletwa na wazazi wake ili kumtolea hekaluni. Kama una mazoea ya kwenda kanisani, unaweza kubahatika kumtambua, na si mazoea yako, hata hivyo mimi ninakualika leo kwenda, pengine utabahatika kumtambua na pengine hata kumshika mkononi huyo mtoto.

Kwa vile siku ya leo ni ya kukutana, tujaribu kuifanyia fikara dhamira hii ya kukutana, ya kuonana, na kuangalia kama tunaweza kufaidika na dhamira hiyo ya kukutana. Hebu tuangalie kwanza aina tatu za kukutana unazoweza kuziona katika sikukuu ya leo.

Aina ya kwanza ya kukutana ni ya Mahekalu:
Hekalu la Yerusalemu lilikuwa ni pahala patakatifu pa kumwabudu Mungu kwa Wayahudi. Hata Yesu alipowakurupusha kwa fimbo watu waliofanya biashara humo hekaluni alisema: “Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala”. Kwa hiyo hekalu lile lilikuwa ni nyumba ya Mungu Baba yake, na ilikuwa pia ni nyumba yake. Yesu Kristu ni Hekalu kama yeye mwenyewe alivyosema: “Bomoeni hekalu hili, nami nitalijenga kwa siku tatu”, aliyasema maneno haya akimaanisha mwili wake mwenyewe.

Hivi Yesu Kristo ni Hekalu la Agano jipya. Leo Yesu aliye hekalu, ameingizwa kwenye Hekaluni la Yerusalem walimoabudia watu wa Agano la kale. Hapo Mahekalu yamekutana. Ni mwonano mzuri, wa Hekalu la Agano jipya kulitakatifuza na kuliimarisha Hekalu la Agano la Kale. Wewe ukiwa kama hekalu la Mungu kwa ubatizo, usiliambae kanisa.

Aina ya pili ya Makutano ya Neno la Mungu:
Ndani ya Hekaluni la Yerusalemu kuliwekwa daima Torah yaani Maandiko Mtakatifu au Neno la Mungu, ikiwakilisha Agano la Kale. Yesu Kristu ni Neno kama tunavyosoma “Neno la Mungu akatwa mwili akakaa kwetu”. Hapa Neno la Agano Jipya linakutana na Neno la Agano la Kale ndani ya Hekalu. Wewe ni uliye Neno hali la Mungu, hekalu la Roho Mtakatifu kwa kipaimara, usiache kulisoma Neno la Mungu-Agano la Kale na Jipya.

Aina ya tatu ya Makutano ni ya Mtoto Yesu na aina mbalimbali ya watu:

Tuko mwanzoni tu mwa ujio wa Yesu hapa duniani na tayari tunaona msururu wa watu waliojaa dukuduku moyoni za kutaka kumwona hata kabla hajafikia kiwango cha kutamka neno yaani kuhubiri, kwa vile bado ni mtoto mchanga. Mtoto Yesu amebebwa na kuletwa kanisani (hekaluni. Huko daima kuna watu kama vile makuhani, na baadhi ya waumini wanaofikafika tu kusali. Tunategemea kusikia kwamba leo anaonana na mapadre, maparoko, watawa, na waumini kibao. Hebu sasa tuione furaha ya binadamu anayefikiwa na Mungu wake.

Aina ya kwanza ya watu ni wazazi wake : Yosefu na Maria
Kabla ya kuwazungumzia watu wengine walioonana na Yesu, hebu tuone jinsi wazazi wake waliomleta walivyofanya: Imeandikwa kwamba “Zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa, wazee wa Yesu walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, kila mtoto mwanaume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana). Wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana: Hua wawili au makinda ya njiwa wawili.”

Kuna maana mbili: Mosi: wazazi (Yosefu na Maria wanamtolea mtoto wao wa kwanza). Ujumbe muhimu kwetu ni kuwa, wazazi hawa walitambua kwamba mtoto huyo si wao, bali ni wa Mungu, wao wamekabidhiwa na kuaminishwa tu ili kumwandaa kwa ajili ya utume aliotumwa kuja kuutekeleza hapa duniani. Wao wanamwandaa tu ili aweze kuwa kama anavyotakiwa kuwa kadiri ya hali inayotegemewa na Bwana aliyemtuma.

Kwa hiyo fundisho ni kwamba kila mtu na kila mtoto anayeingia hapa duniani ni zawadi tu kwetu ni mali ya Mungu. Anachotakiwa kukifanya kila mzazi ni kumtolea mtoto huyo kwa Mungu na siyo kumhodhi tu. Wazazi wanatakiwa wamtunze na kumhudumia ili aweze kutimiza utume alioitiwa kwa kuzaliwa hapa duniani. Pili, Wazazi hawa hawatoi kondoo kama wafanyavyo wenye kipato, bali wanatoa njiwa ili kuonesha jinsi walivyokuwa fukara. Huu ni mfano kwa mwumini kuwa mtu wa kawaida siyo wa kutaka makuu na kupaparikia mali na kutawaliwa nayo.

Aina ya pili ya watu ni kukutana Simoni na Anna:
Tunaletewa mtu wa kwanza aliyeonana na Yesu ikisema: “Palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya israeli. Na Roho mtakatifu alikuwa juu yake.” Mtu huyu Simeoni tuliyeletewa tunaambiwa kuwa ni mtu mwenye haki na wa kumcha Mungu (mtu wa sala). Maana yake, hapa kuna makutano kati ya mwisraeli wa kwelikweli na Masiha wa kweli anayesubiriwa. Simeoni ameoneshwa Masiha aliyekuwa anasubiriwa katika kipindi chote cha Agano la Kale lililokuwa linasubiriwa kutimilizwa.

Cha ajabu ni kwamba pale hekaluni palikuwa pamejaa lukuki ya binadamu. Lakini ni watu wawili tu ndiyo wanaomtambua mtoto huyu kuwa ni Masiha. Aidha watu hawa wala si mapadiri wala watawa, bali ni vizee vya kawaida tu. Ni tofauti na vijana tu wazazi wa mtoto (Yosefu na Maria). Kulikoni? Je, vizee hivi vilifanya nini cha ajabu hadi vikafaulu kumtambua mtoto huyu kuwa ni Masiha wa Bwana?

Jibu linapatikana katika Maandiko hayohayo pale inaposema kwamba: “Simeoni alikuwa mtu mwenye haki na mcha Mungu, alikuwa na roho safi na nyeupe”. Heri wenye moyo safi maana hao watamwona Mungu. Watu wenye moyo safi ndiyo wanaweza kuona zaidi ya kile kinachoonekana kwa macho. Watu wengine waliofika pale hekaluni walikuwa wanamwona mtoto huyu kama vile angekuwa kama watoto wengine wa kawaida. Yaani mtoto asiye na la pekee.

Simone kumbe, analo jicho la pekee na anafaulu kuona hadhi ya pekee aliyokuwa nayo mtoto huyu kuwa siyo wa kawaida, yaani ni Masiha wa Bwana. Kuna pia hoja nyingine inayomsaidia Simoni kuona mambo tofauti na wanavyoona wengine. “Ni kwamba Roho Mtakatifu alikuwa juu yake, kwamba Roho mtakatifu alimtaarifu mapema kwamba hatakufa kabla ya kumwona Kristu wa Bwana. Aidha alikuja hekaluni ameongozwa na Roho” Kwa mantiki hiyo Simoni alikuwa amesukumwa na Roho. Alikuwa daima katika maisha yake anaongozwa na Roho wa Bwana na siyo kuburuzwa na vionjo vya ulimwengu huu. Kumbe Roho huyo anaongea pia ndani yetu.

Yabidi kumsikiliza, badala ya kumvuruga, na kumdharau na kumpurukusha hadi anashindwa kusikika anapootuongelesha nafsini mwetu. Tunabaki tumeng’ang’ana na hoja zetu na fikra zetu tu. Roho anaongea nasi, hasa tunapokutana na Kristo anapoongea nasi katika Neno lake, katika watu wanaotushauri na kutuhubiria, hapo ndipo kuna sauti ya huyo Roho anayetuwezesha kumtambua na kusema huyu ndiye Kristu, hii ni sauti ya Roho mtakatifu.

Mzee Simoni alikuwa alisikiliza daima sauti hiyo. Kwa kufanya hivyo alimtukuza Bwana na ameweza kuyapa maana maisha yake. Kwa vile ni mzee unamwona pia anaimba. Watawa daima tunaimba wimbo wa mzee Simoni katika sala za mwisho (kompleto): “Sasa Bwana wamruhusu mtumishi wako, kwa amani, kama ulivyosema; kwa kuwa macho yangu yemeuona wokovu wako, nuru ya kuwa mwangaza wa mataifa na kutukufu wa watu wako Israeli”.

Kwa maneno haya Umruhusu mtumishi wako mzee Simoni anatufundisha jinsi nzuri ya kuzeeka na kukabiliana na kifo. Mzee huyu anaangalia mbele katika maisha. Siyo kulalamika na kunung’unikia maisha yaliyoishapita au yaliyopo. Haangalii nyuma kwamba maisha hayana maana. Kwake kifo ni kama kwenda kwenye amani. Ni kama kusema, nimeishi maisha yangu nikiongozwa na Roho wa Bwana, sasa sihitaji tena kitu kingine bali ni kuachana na maisha haya. Nimeshaona mwanga tayari. Sasa kumebaki ni kwenda mbele kuelekea kwenye amani.

Kuhusu neno kuruhusu, halimaanishi kukimbia majukumu kama wasemavyo wengi. Mimi ni mzee mniache nipumzike. La hasha, bali ni kwenda kutangaza habari njema. Mzee Simeoni hajifikirii yeye mwenyewe tu, bali anafikiria juu ya mwanga utakaoangaza ulimwengu. Kisha anashukuru Maria na Yosefu, na anafanya utabiri. Mtoto huyu ni anguko na ufufuko kwa wengi Israeli. Yaani ni upanga utakaochoma moyo. Kuna woga wa lengo la mtoto huyu. Wengine watampokea wengine watamkataa. Mtoto huyu anao wito wa kufanya. Yeye mwenyewe atakataliwa na itamwumiza pia huyu mtoto huko kukataliwa.

Kuhusu Nabii huyu wa kike Anna siyo yule mke wa Yoakim ambao ni wazazi wa mama wa Maria. Mama huyu anatajwa hapa kama alama tu inayotaka kutufundisha au kutuletea ujumbe fulani wa maana. Tunaambiwa alikuwa na miaka 84. Miaka hii ina maana yake zaidi ya kutuonesha umri wake. Namba hii inapatikana kwa kuzidisha 7 mara 12. Namba saba inamaanisha ukamilifu, pindi namba kumbi na mbili ni alama ya watu yaani makabila kumi na mbili ya Israeli, na pia mitume kumi na wawili. Mama huyu anawakilisha taifa hili la waisraeli wanaompokea Masiha wa Mungu. Watu hawa waisraeli ndiyo wale wanaotegemewa kumpokea Masiha wa Mungu.

Alama nyingine anayotuonesha mama huyu Anna ni kwamba alikuwa ni mwanamke aliyeolewa na kukaa na mume wake kwa miaka saba (hata hapa namba inayoonesha ukamilifu) kisha anabaki mjane (ingawa haisemwi kama alifiwa na mume au aliachika tu) lakini jambo muhimu linaloonekana kwake ni kwamba, anabaki hivi mjane bila kuolewa tena na mume mwingine. Mama huyu ni alama ya uaminifu yaani anawakilisha uaminifu.

Aliamua kutopenda tena mtu mwingine, bali ni kubaki mwaminifu kwa mume wake wa kwanza (ndoa) aliyemfungia nadhiri zake. Katika kipengee hiki Anna anawakilisha uaminifu kwa mume au Bwana mmoja ambaye kwa wana Taifa la Israeli, ni uaminifu kwa Bwana mmoja yaani Mungu. Yeye ndiye mume wa ndoa ambaye si mtoa amri, mwamrishaji, siyo katili. Ni mume aliyempenda mke wake yaani ulimwengu. Huyo Bwana arusi wa kanisa ni Yesu Kristu. Mke wake ndoa ni Kanisa, huyo ndiye anampokea na kumkumbatia Bwana wake. Hapa unakuta tena kukutana kwingine, kati ya Bwana na Bibi arusi. Mungu na binadamu. Bi arusi (Anna) anamtambua Bwana arusi na wanakumbatiana.

Alama nyingine anayotuonesha Anna inatokana na asili yake. Hasahasa jinsi asivyoogopa wala kuona aibu kujionesha mbele za watu licha ya utofauti huo. Imeandikwa kwamba Mama huyu alikuwa biti Fanueli wa kabila la Asheri. Kabila hili, lilikuwa na bahati ya kukabidhiwa ardhi yenye rutuba sana, hivi wakajiendeleza sana kiuchumi. Kwa vile ardhi hiyo ilikuwa ni sehemu ya upagani, wakachangamana nao,na kujizamisha katika raha za utajiri, kisha kabila likajikuta limepoteza utamaduni na imani yake na hatimaye likafifia kabisa. Kwa hiyo wakati wa (enzi za Yesu) kabila hili lilikuwa limeshafifia kabisa. Kama kulikuwa na watu waliobakia wa kabila hili, waliona aibu sana kujionesha kadamnasi.

Kumbe ni mama huyu tu aliyebaki mwaminifu kwa imani yake kwa Mungu mmoja bila kuyumbishwa na miungu mingine ya kipagani. Mama huyu anawakilisha waisraeli waliobaki waaminifu bila kuyumbishwa na miungu mbalimbali inayowazunguka. Mama huyu anajiwakilisha tofauti na wengine. Ndugu zangu ni ngumu sana kumfuata Kristu katika mazingara yenye thamani fulani za dunianhii zinazovutia kwa nguvu sana. Yabidi wakati mwingine kujikaza na kubaki katika msimamo wako.

Hata kiutamaduni. Makabila mengine yanapoteza utamaduni wake kutokana na kushabikia utamaduni wa makabila mengine. Kadhalika utamaduni wa nchi, unaweza kufifia wenyewe bila kujitambua kwa kuyumbishwa na utamaduni wa mataifa mengine, iwe lugha, mavazi, muziki, nk. Kazee haka kanatufundisha kutojivua nguo za utamaduni zilizohifadhi utu wetu na kujifunika maua ya utamaduni wa mataifa mengine kwa vile yanapendeza kuyatazama.

Ujumbe wa Papa kwa siku ya 17 ya Siku ya Watawa ulimwenguni: “Katika Kristo tunajigundua kuwa tumependwa na Mungu, kwamba tayari tulishatiwa wakfu kwake katika ubatizo, tukaitwa kujitolea sadaka wewe katika upendo, tukitegemezwa na neema ya Roho mtakatifu. Katika yeye tunakuta kila siku maana ya mwito wetu na kupata furaha ya kuwa wanafunzi na mashuhuda wake.”

Tafakari hii imeandaliwa na
Padre Alcuin Nyirenda, OSB.


Habari : radio vaticana

No comments:

Post a Comment