Sunday, March 30, 2014

Muswada wa ndoa ya wake wengi yachafua hali ya hewa nchini Kenya!

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya limemwandikia barua Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kumwomba, asikubali kuridhia muswada wa sheria uliopitishwa hivi karibuni na Bunge, nchini Kenya wa kutaka kuhalalisha ndoa za wake wengi. Barua iliyoandikwa na kutiwa mkwaju na Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya inasema kwamba, Kanisa limeendelea kuwa mstari wa mbele katika kukuza utu, maadili na nidhamu katika maisha ya wananchi wengi wa Kenya, hasa kuhusiana na masuala ya ndoa na familia, kwani huu ni msingi wa umoja, mshikamano na mfungamano wa maisha ya kijamii.

Hii ni changamoto kwa Serikali kuhakikisha kwamba, inasaidia kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, mambo yanayoakisi maadili na utu wema miongoni mwa wananchi wa Kenya. Muswada wa sheria uliopitishwa na Bunge la Kenya una vipengele ambavyo kimsingi vinakinzana na: Sheria asilia, Amri za Mungu pamoja na Mafundisho ya Kanisa; mambo ambayo hayakuzingatiwa kamwe wakati wa mchakato wa kutunga sheria hii mpya ya ndoa. Kutokana na mapungufu makubwa ya kimaadili na utu wema yanayojitokeza kwenye muswada huu, Kanisa Katoliki nchini Kenya, linamwomba, Rais Uhuru Kenyatta kutoridhia muswada huo.

Marekebisho mengine ya sheria ya ndoa ya Mwaka 2013 yanahusu mgawanyo wa mali ikiwa kama ndoa itavunjika. Hapa kila mtu atagawiwa kadiri ya mchango wake, jambo ambalo linapingwa vikali na Wabunge wanawake wapatao 69, kati ya wabunge 349 wa Bunge la Kenya. 


habari kwa hisani ya radio vatican 

No comments:

Post a Comment