Thursday, May 22, 2014

Amani, furaha na upendo ni sehemu ya vinasaba vya Mkristo!



Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Alhamisi tarehe 22 Mei 2014 anasema kwamba, furaha, amani na mapendo ni sehemu ya vinasaba vya utambulisho wa Mkristo; zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu anayewachangamotisha waamini kupenda na kuwashirikisha wengine furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake!

Amani, Furaha na Upendo ni zawadi ambazo Yesu kwa njia ya Roho Mtakatifu amewakirimia waja wake kama sehemu ya mchakato wa kumwilisha Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani katika uhalisia wa maisha ya mwamini. Waamini wanapaswa kupenda, lakini zaidi kubaki katika pendo lao na Yesu, huu ndio mwito na mwaliko kutoka kwa Kristo, kielelezo makini cha upendo wa Mwenyezi Mungu uliofunuliwa kwa njia ya Yesu Kristo.

Amani na Upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo unawawezesha waamini kujishikamanisha na Kristo na hivyo kuwamegea wengine. Baba Mtakatifu anasema, amani, furaha na upendo ni mnyororo unaowaunganisha: Mwenyezi Mungu, Yesu Kristo na Wakristo. Afya ya Mkristo katika maisha yake ya kiroho inajikita katika furaha hata pale anapopambana na madhulumu, nyanyaso na magumu katika maisha. Hivi ndivyo wafiadini walivyokabiliana na kifo pasi na woga.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Roho Mtakatifu akae ndani mwao, kwani wengi wao wanamsahau katika sala na maombi, ili aweze kuwasaidia kuwa kweli ni watunzaji wa amani, upendo na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake!

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment