Tuesday, May 27, 2014

Kituo cha Familia Kimataifa mjini Nazareti



 Chama cha Kikatoliki cha Uamsho wa Roho Mtakatifu, kinamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuombea mradi wa Kituo cha Familia Kimataifa kilichoko mjini Nazareti wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, kwenye Uwanja wa Pango la Mtoto Yesu, Jumapili tarehe 25 Mei 2014 wakati wa hija yake ya kitume Nchi Takatifu. Baba Mtakatifu ameonesha nia ya kutembele Nazareti mahali ilipoishi Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu panapo majaliwa!

Kituo cha Familia Kimataifa kilianzishwa na Baraza la Kipapa la Familia na kukikabidhi kwa Chama cha Kikatoliki cha Uamsho wa Roho Mtakatifu kukiendesha. Mradi huu mkubwa utakapokamilika, unatarajiwa kuwa ni kituo cha majiundo ya tasaufi ya familia; mahali ambapo familia mbali mbali zinazofanya hija Nchi Takatifu zinaweza kupata malazi ya muda. Hapa waamini watapata majiundo makini na endelevu kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Wafanyakazi katika utume wa ndoa na familia wataweza kujinoa kwenye kituo cha Familia Kimataifa. Kwa ufupi, hapa ni mahali ambapo Familia za Kikristo zitaandaliwa kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa tunu msingi za maisha ya kifamilia.

Kituo hiki cha Kimataifa kitatoa kozi maalum za ndoa na familia kwa ajili ya waamini wanaoishi ndani na nje ya Nchi Takatifu, kwa kushirikiana na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Duniani pamoja na vyuo vikuu vya Kanisa Katoliki; lengo ni kutoa huduma makini ya kiroho na kimwili kwa ajili ya familia. Kituo hiki kinatarajiwa kuwa ni faraja kwa familia zinazokabiliana na hali ngumu ya maisha, kwa kutumia mfuko maalum kwa ajili ya familia.


Habari kwa hisani ya radio vatican


No comments:

Post a Comment