Tuesday, May 27, 2014

Sala ya Familia katika Mwaka wa Familia Jimbo kuu la Dar es Salaam



Ee Mungu Mwenyezi, uliye asili ya familia, tunakushukuru kwa zawadi hii nzuri kwetu. Umetupatia familia, ili wanadamu waendelee kukutukuza wewe, katika kuendeleza kazi ya uumbaji. Umetaka familia iwe shule ya kwanza ya imani, matumaini na mapendo. Aidha, ulipenda familia ziwe kielelezo cha umoja na mshikamano, kwa mfano wa Utatu Mtakatifu na Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.
Uzifanye familia zetu ziwe chemchemi ya utakatifu, kwa kuwa watu wa sala, kushiriki Sakramenti, hasa ya Ekaristi na Kitubio, kujitoa kwa maisha ya jumuiya ndogondogo, na kuwa mwanga kwa uinjilishaji mpya. Utupe ujasiri wa kupalilia miito mitakatifu, ili Kanisa lako liwe na watendaji wengi na walio watakatifu.
Tunakuomba Ee Mungu, uzibariki familia zetu, uziongoze na uzilinde dhidi ya maadui, na upotofu wote, unaotaka kuzivunja na kuzitoa familia zetu katika malengo yako. Uzijalie familia zetu moyo wa ukarimu na ujasiri wa kupokea zawadi ya uhai mpya na kuutunza. Uzijalie fadhila ya msamaha, ulio msingi wa umoja na mshikamano. Uamshe ari na moyo wa kujitoa sadaka, ndani ya familia zetu, katika dunia hii iliyojaa ubinafsi mwingi. Utupe moyo wa ukarimu kwa wale walio wanyonge, na wadhaifu zaidi katika familia zetu.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana Wetu.
Amina.
Mtakatifu Yosefu msimamizi wa Jimbo letu, utuombee.

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment