Tuesday, May 13, 2014

Msimwekee kizingiti Roho Mtakatifu!



Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumatatu tarehe 12 Mei 2014 anasema kwamba, wapagani waliomwongokea Kristo ilikuwa ni kazi ya Roho Mtakatifu anayeliwezesha Kanisa kusonga mbele katika maisha na utume wake na wala hakuna mtu awaye yote anayeweza kuzuia nguvu ya Roho Mtakatifu, kwani Roho Mtakatifu anavuma pale anapotaka.

Baba Mtakatifu anasema kishawishi kikubwa kwa baadhi ya waamini ni kutaka kumwongoza Roho Mtakatifu kadiri ya vionjo na nia zao. Hiki ni kishawishi ambacho kimekuwepo hata ndani ya Kanisa kama inavyojionesha katika Liturujia ya Neno la Mungu katika Kitabu cha Matendo ya Mitume. Jumuiya ya Wapagani inapokea Neno la Mungu na Mtakatifu Petro ni shahidi wa ujio wa Roho Mtakatifu kwa watu hawa waliomwongokea Kristo. Kwa bahati mbaya anasema Baba Mtakatifu kuna baadhi ya watu waliotaka bado kushikilia Mapokeo na tamaduni zao za awali, kwao hii inakuwa ni kashfa ya mwaka!

Mtakatifu Petro alifafanua jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo alivyowajalia wapagani zawadi ya wokovu kwa njia ya wongofu wa ndani, kumbe, hakuna na sababu yoyote ya kumzuia Roho Mtakatifu kutenda kazi yake. Kwa maneno haya ya hekima na busara, amani na utulivu vinarejea tena katika Jumuiya ya Wakristo wa kwanza.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kutomwekea Roho Mtakatifu kizingiti anapowaonesha waja wake njia ya kufuata, changamoto na mwaliko kwa Maaskofu na Mapadre kuwa na ujasiri wa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu katika maamuzi yao. Wawe ni wahudumu wanaomfungulia Roho Mtakatifu mlango na kamwe wasimfungie nje, kwani Kanisa linaendelea kusonga mbele kutokana na uwepo wa Roho Mtakatifu, anayewafundisha ukweli wote!

Baba Mtakatifu anasema, Roho Mtakatifu ni kielelezo hai cha uwepo wa Mungu ndani ya Kanisa na nguvu inayolisukuma Kanisa kusonga mbele katika maisha na utume wake. Roho Mtakatifu na karama zake, analiongoza Kanisa na kwamba, huwezi kulifahamu Kanisa kwa ukamilifu bila ya uwepo wa Roho Mtakatifu. Ni Roho Mtakatifu anayefanya mageuzi ndani ya Kanisa kama alivyosema Mtakatifu Yohane XXIII.

Ni wajibu wa waamini kumwomba Roho Mtakatifu awasaidie unyenyekevu wa kuweza kusikiliza na kuelewa kile anachozungumza kwa ajili ya Kanisa kutoka katika undani wa mioyo ya watu. Roho Mtakatifu anatumia nafasi na matukio mbali mbali kuzungumza na Kanisa.

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment