Thursday, May 29, 2014

Nguvu ya Imani!

Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anapoiangalia hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko Nchi Takatifu iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu, ili wote wawe wamoja anasema, Kanisa limeshuhudia nguvu ya imani ikimwilishwa katika uhalisia wa maisha ya Wakristo. RealAudioMP3

Kwa mara ya kwanza Patriaki Bartolomeo wa kwanza alishiriki katika Ibada ya Misa Takatifu, Papa Francisko alipokuwa anaanza utumishi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ilikuwa ni nafasi muhimu sana na tukio la kihistoria katika maisha na utume wa Kanisa, kiasi cha kupanga tena kukutana mjini Yerusalemu, kama kilele cha maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipokutana, akazungumza na kusali na Patriaki Anathegoras, mwanzo wa hija ya majadiliano ya Kiekumene.

Tukio la viongozi hawa wakuu kukutana na kusali kwa pamoja, Jumapili tarehe 25 Mei 2014, ni tukio la kihistoria, kwani limewahusisha pia viongozi wa Makanisa mengine ya Kikristo kwa kutambua uzito wa majadiliano ya kiekumene uliopo mbele yao! Khalifa wa Mtakatifu Petro anapaswa kuwa ni daraja ya huduma ya umoja, upendo na mshikamano kwa Makanisa ya Kikristo unaojikita kwanza kabisa katika maisha ya sala! Viongozi wa Makanisa wamesali kwenye Kaburi Takatifu la Yesu Mfufuka, matendo makuu ya Mungu.

Padre Lombardi anasema, kitendo cha Baba Mtakatifu Francisko kutoa mwaliko wa kusali pamoja na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina na Shimon Perez wa Israeli ni kuonesha ujasiri unaopata chimbuko lake katika nguvu ya sala! Baba Mtakatifu alikuwa anatambua uzito wa mwaliko huu, akawa tayari kujitosa kimasomaso kuwaalika viongozi hawa wawili, si kwa ajili ya kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Israeli na Palestina, bali kusali kwa pamoja na baada ya hapo, kila mmoja akiongozwa na dhamiri nyofu aweze kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Wapalestina na Waisraeli.

Padre Lombardi anasema, amani ambayo ilionekana kuwa ni jambo lisilowezekana kwa urahisi, Baba Mtakatifu Francisko ameonesha nguvu ya maisha ya kiroho katika mchakato wa majadiliano yanayopania kutafuta amani, upendo, mshikamano na mafao ya wengi. Kanisa lina matumaini makubwa kwamba, kwa njia ya sala mambo mengi yanaweza kubadilika! Ikumbukwe kwamba, amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Papa Francisko ni kiongozi mwenye imani katika neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Kanisa lake! Pale ambapo amani inaonekana kuwa ni jambo lisilowezekana, basi waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kuendelea kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia amani inayowawajibisha katika vipaumbele vyao!

Padre Federico Lombardi anasema kwamba, hadi sasa hakuna tarehe maalum iliyopangwa kwa ajili ya Marais wa Palestina na Israeli kukutana na kusali pamoja na Baba Mtakatifu Francisko mjini Roma. Ni matumaini ya Padre Lombardi kwamba, Marais hawa wawili ambao wameonesha kuridhia ombi na mwaliko kutoka kwa Baba Mtakatifu watapanga tarehe ya kukutana na kusali kwa pamoja. Waamini na watu wenye mapenzi mema, wanaweza kuendelea kusali kwa ajili yakufanikisha tukio hili la kihistoria kwa ajili ya kuombea amani.

Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko ilisheheni matulio makubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Licha ya Baba Mtakatifu na wale waliokuwa katika msafara wake kuchoka, lakini imekuwa ni chemchemi ya furaha, imani na matumaini kwa ajili ya mafao ya wengi: Baba Mtakatifu ametenda yote kadiri ya uwezo wake, Padre Lombardi anasema, bila shaka alikuwa ametunza akiba mahali fulani, hapa si bure!

Imeandaliwa na
Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment