Friday, June 13, 2014

Serikali haina dini!



Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria katika ujumbe wake uliotolewa kwa vyombo vya habari hivi karibuni linasema kwamba, dini ni sawa na upanga wenye makali kuwili, inaweza kutumika kwa ajili ya kuwajenga na kuwaimarisha watu katika umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kusimama kidete kulinda na kutetea madao ya wengi. Dini pia inaweza kutumiwa vibaya kuwagawa, kuwanyanyasa na kuwadhulumu watu na matokeo yake ni machafuko ya kidini na maafa kwa watu wasiokuwa na hatia!

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linasema kwamba, changamoto kubwa iliyoko mbele ya wananchi wa Nigeria ni kuweza kuweka uwiano mzuri katika masuala ya kidini, ustawi na maendeleo ya watu. Jambo hili linawezekana ikiwa kama Katiba ya nchi ambayo ni sheria mama itatekelezwa kikamilifu. Katiba inatambua kwamba, Nigeria ni nchi ambayo ina amini katika uwepo wa Mungu mmoja na kwamba Serikali kuu au Serikali za Kijimbo hazitaruhusiwa kuwa na dini kama dini ya Jimbo au Nchi ya Nigeria.

Kumbe, baadhi ya wanasiasa kuchukulia kwamba, Uislam ndiyo dini rasmi ya Majimbo yaliyoko Kaskazini mwa Nigeria ni kwenda kinyume cha Katiba ya nchi na matokeo yake ni kuendelea kushuhudia maafa ya watu wasiokuwa na hatia wanaoendelea kupoteza maisha yao kutokana na misimamo mikali ya kidini. Hali hii imepelekea hata kuwepo kwa sheria na sera za kibaguzi zinazotekelezwa na Serikali za Majimbo kiasi kwamba, Wakristo hawana haki ya kununua ardhi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za ibada na kwamba, wanatengwa hata katika ufadhili wa masuala ya hija za maisha ya kiroho!


Habari kwa hisani ya radio vatican


No comments:

Post a Comment