Friday, July 11, 2014

Iweni mashahidi wa Injili ya Furaha!


Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani kwa Mwaka 2014 linawaalika Mabaharia wenyewe kujitosa kimasomaso katika mchakato wa Uinjilishaji kwa kuwashirikisha wengine Injili ya Furaha.

Waamini wanakumbushwa kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wamejitwalia dhamana ya kuwa ni vyombo vya Uinjilishaji pamoja na kuwashirikisha wengine ile furaha inayobubujika kutoka imani kwa Kristo na Kanisa lake! Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanatolea ushuhuda wa imani pamoja na kukoleza moyo wa ibada hasa kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Itakumbukwa kwamba, Bikira Maria, nyota ya bahari ndiye msimamizi wa Utume wa Bahari, Mama anayewalinda na kuwatunza.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linawakumbusha waamini kwamba, , wanapaswa kuwa kweli ni vyombo vya Habari Njema ya Wokovu na upendo kwa mabaharia, ili waweze kuonja ukarimu unaobubujika kutoka katika imani inayomwilishwa katika matendo. Kwa njia hii wanaweza kuimarishwa katika maisha na utume wao kwa kuendelea kuwa ni wafuasi amini wa Yesu Kristo katika ulimwengu wa Mabaharia.

Maaskofu wa Hispania wanawakumbuka Mabaharia wote waliofariki dunia wakati wakitekeleza dhamana na utume wao baharini. Wanaziombea familia za mabaharia zimeze kuwa imara na thabiti wanapokabiliana na changamoto mbali mbali za maisha. Maaskofu wanawaweka Mabaharia wote chini ya ulinzi wa Bikira Maria wa Mlima Karmeli, ili aweze kufungua mioyo yao kwa Kristo na Kanisa lake, awasaidie waweze kuwa wasikivu bora wa Neno la Mungu, tayari kuwa kweli ni Mashahidi wa Injili ya Furaha, changamoto endelevu inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu!

No comments:

Post a Comment