Friday, July 11, 2014

Nilikuwa Gerezani mkaja kunitazama!

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi asubuhi, tarehe 21 Juni 2014 ameianza hija yake ya kichungaji Jimboni Cassano allo Jonio, lililoko Calabria, Kusini kwa Italia, kwa kuwatembelea na kuzungumza na wafungwa pamoja na askari magereza wa Castrovillari ili kuonesha mshikamano wa Papa na Kanisa kwa wafungwa sehemu mbali mbali za dunia, kama kielelezo cha utekelezaji wa matendo ya huruma, kadiri ya mafundisho ya Yesu mwenyewe!

Baba Mtakatifu anasema, tafakari yake na wafungwa inagusia kwa namna ya pekee haki msingi za binadamu na mahitaji msingi msingi ya wafungwa wanaotekeleza adhabu yao wakiwa gerezani na kwamba, sera za huduma magerezani ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha pekee kwa kusindikizwa na mikakati inayomwezesha mfungwa anapomaliza kutumikia kifungo chake aweze kujiunga tena na Jamii. malengo haya yanaposhindwa kutekelezwa matokeo yake ni adhabu zinazotolewa magerezani zinakuwa ni mzigo na uharibifu wa maisha ya kijamii na kwa mhusika na jamii inayomzunguka.

Baba Mtakatifu anawakumbusha wafungwa kwamba, mchakato unaopania kumrekebisha mfungwa ili anapomaliza adhabu yake aweze kujiunga tena na Jamii si tu juhudi za kibinadamu bali pia hapa kuna haja kwa wafungwa wenyewe kujibidisha kukutana na Mwenyezi Mungu ili kumwachia nafasi aweze kuwafunda, kwani anawapenda, anawafahamu na ana uwezo wa kuwasamehe makosa yao. Yesu ni mwalimu anayeweza kuwasaidia kujiunga tena na Jamii zao, kwa kuwashika mkono na kuwarejesha tena kwenye Jamii. Mwenyezi Mungu daima anasamehe na kuongoza; anaelewa na kungoja ili mwanadamu aweze kumwelewa, kusamahe na kuongozwa naye!

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, muda huu wa kutumikia adhabu ya kifungo gerezani hautapotea bure, bali utakuwa ni muda makini kabisa, kwa ajili ya kuomba na kupata neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu ya kubadilika na kuwa watu wema zaidi sanjari na mwelekeo mpya wa kijamii kwani matendo mbali mbali yanayofanywa ndani ya jamii yanachangia katika wema au ubaya wa Familia ya binadamu.

Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea wanafamia wote wa wafungwa walioko magerezani, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia utulivu na amani na kwamba, anapenda kuwatia shime askari magereza na wote wanaowahudumia wafungwa kutekeleza dhamani hii kwa unyofu mkubwa.

Wakati huo huo Bwana Fedele Rizzo, Mkuu wa Gereza la Castrovillari, kwa niaba ya askari magereza na wafanyakazi wote wa Gereza hilo anapenda kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatembelea, kuwafariji na kuwatia moyo, tukio ambalo limeacha chapa ya kudumu katika akili na mioyo yao. Wanampongeza kwa kuonesha mshikamano na watu, kiasi kwamba, watu wengi wanapenda kumwona na kumsikiliza kutokana na ushuhuda wa maisha yake yanayojikita katika unyofu, kiasi na uadilifu.

Naye Ivan, mmoja wa wafungwa wanaotumikia kifungo Gerezani hapo kwa niaba ya wafungwa wenzake, amemshukuru Baba Mtakatifu kwa kuwatembelea Kondoo waliopotea ili aweze kuwarudisha tena Zizini. Uwepo wake hapo Gerezani ni kielelezo cha Mchungaji mwema anayejali na kuguswa na mahangaiko ya watu wake.

Baba Mtakatifu anaonesha ile sura ya Mungu anayeendelea kumtafuta mwanadamu aliyepotea ili aweze kumwonjesha upendo na huruma akiheshimu mchakato wa kila mfungwa katika jitihada za kujirekebisha tena kutokana na mapungufu na makosa yake ya kibinadamu yaliyopelekea hata akatiwa hatiani. Wafungwa hao wamemhakikishia Baba Mtakatifu kwamba, wataendelea kumsindikiza kwa sala na kamwe hawatasahau siku hii aliyowatembelea na kuwasalimia.

Habari kwa hisani ya radio vatican


No comments:

Post a Comment