Wednesday, July 23, 2014

Wakristo Mashariki ya Kati, kamwe si watu wa kuja!

Kardinali Leonardi Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki anasema amani inapaswa kutawala na hivyo kushinda kishawishi cha matumizi ya mtutu wa bunduki, jambo ambalo linaendelea kusababisha mateso makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia. Wakristo nchini Iraq wanadhulumiwa na kuteswa kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusaidia juhudi za kusitisha mapigano huko Mashariki ya Kati, ili amani ya kweli iweze kutawala kati ya watu.

Kardinali Sandri anaonesha masikitiko yake makubwa kutokana na mateso ya watu wanaolazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao. Wakristo huko Mosul na Aleppo wanakabiliana na madhulumu ya kidini, kwani nyumba na Makanisa yao yameharibiwa vibaya sana kutokana na chuki za kidini. Hali hii inaonesha kwamba, huko Mashariki ya Kati usalama kwa Wakristo ni kidogo sana, lakini kwa bahati mbaya, Jumuiya ya Kimataifa inaonekana kutoguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya Wakristo huko Iraq na Mashariki ya Kati katika ujumla wake.

Utu, maisha na heshima ya kila mtu vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na kamwe vita si suluhu ya amani ya kudumu, bali ni chanzo na mwendelezo wa watu kulipizana kisasi. Kardinali Sandri anapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na viongozi wa Makanisa ya Mashariki ambao wameendelea kuwa bega kwa bega na waamini wao katika kipindi hiki kigumu cha historia na maisha yao. Jambo la msingi ni watu kupania kudumisha uhuru wa kuabudu sanjari na kuendeleza haki msingi za binadamu.

Wakristo wanaoishi huko Mashariki ya Kati si watu wa kuja wala wageni, ni raia wenye haki na dhamana katika nchi yao wenyewe, kumbe vitendo vya kuwanyanyasa na kuwabagua ni kinyume cha sheria za nchi na haki msingi za binadamu. Wakristo wanapaswa kuendelea kuishi katika maeneo yao, ili kuchangia katika ustawi na maendeleo yao: kiroho na kimwili.

Kwa namna ya pekee kabisa, Kardinali Sandri anawakumbuka na kuwaombea Wakristo wanaoishi Nchi Takatifu, Lebanon, Syria, Iraq na Misri, bila kuwasahau wahanga wote wa mashambulizi ya kivita. Ni matumaini yake kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itasaidia juhudi za kujenga na kudumisha: uhuru, haki msingi za binadamu, upatanisho na amani ya kweli kati ya wananchi wanaoishi huko Mashariki ya Kati. Watu wajenge utamaduni wa kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana kama ndugu na kwamba, chuki na uhasama wa kidini ni mambo yaliyopitwa na wakati na wala hayana tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya watu.

Wakristo wanayo haki kabisa ya kuishi huko Mashariki ya Kati ambako ni chimbuko la Ukristo, yapata miaka elfu mbili iliyopita. Kardinali Leonardo Sandri anawaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kusali bila kuchoka kwa ajili ya kuombea amani, utulivu na upatanisho huko Mashariki ya Kati. Wanamwomba Yesu Kristo, Bwana wa amani, awasaidie kuendeleza moto wa matumaini hata katika mazingira haya magumu na yenye kukatisha tamaa.

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment