Sunday, August 24, 2014

Mkoa wa Kagera na tamaduni zake

Utamaduni ni kielelezo cha uzalendo na amani, umoja na mshikamano baina ya wananchi,Taifa ndani na nje ya nchi.
Pamoja na hayo utamaduni pia huchochea ufahamu wa kuthamini na kushiriki katika kukuza na kuendeleza utamaduni.
Kwa kutambua umuhimu wa utamaduni kila nchi imepanga siku ya utamaduni ikiwa kuwakumbusha wananchi vitu mbalimbali vya asili ambapo Tanzania siku ya utamaduni iliadhimishwa kwa mara ya kwanza   Mei 21, 2005 na hivyo kuadhimishwa kila mwaka inapofika tarehe na mwezi kama huo.
Vitu muhimu vinavyoadhimishwa siku hiyo ni pamoja na uvaaji wa mavazi ya kiasili, upambaji wa ukumbi wa shughuli ambapo hutumika vifaa vya mapambo ya asili, burudani na ngoma za asili na muziki wa kitanzania, vyakula mbalimbali vya asili makabila ya kitanzania na kupokea wageni kwa heshima kwa kufuata mila na desturi ya kitanzania.
Bado tupo mkoani Kagera ambao ni moja ya Mikoa iliyopo nchini Tanzania ambapo Julius Rwehangura mwenye asili ya kabila la Wahaya mkazi wa tabata kisukuru ambaye pia nia mwenyeji wa Mkoa wa Kagera anaelezea zaidi kuhusu jina  analopewa mtoto anapozaliwa na nyakati zake.
Rwehangura anaeleza kuwa mtoto anapozaliwa jina hutolewa na babu au bibi wa upande wa baba na kama ao hawapo anaweza akatoa baba kulingana na utaratibu ulioko katika ukoo.
Endapo kutakuwa na mgonjwa ana hali mbaya  katika familia mfano shangazi,bibi,mjomba na wengineo,na mtoto akazaliwa wakati huo na mgonjwa akapona basi mtoto huyo ataitwa (kokuumbya) ikiwa na maana kama mtoto huyo malaika ambaye alikuwa akimuombea mgonjwa.
Rwehangura anaeleza kuwa endapo mtoto amezaliwa na amekuta baba yake amefariki,yaani baba amemwacha mama akiwa mjamzito atakapozaliwa  akiwa wa kiume mtoto ataitwa jina la (Kashangaki).
Jina la (Kamugisha) lina maan ya bahati,yaani endapo mtoto kazaliwa katika familia na ndugu yoyote katika ukoo akapata kazi,ama kafaulu masomo kwa hiyo mtoto huyo anamaanisha kaja na bahati.
Rwehangura anaeleza kuwa endapo kumetokea kesi mahakamani ama katika ukoo mtu amefukuzwa kazi akapambana akashinda na hapo mtoto akazaliwa ataitwa (Mutalemwa ) ikiwa na maana ni mtu ambaye hashindwi.
Ikiwa mama amefululiza kuzaa watoto wa jinsia moja,mfano mtoto wa kwanza hadi wa tatu ni wa kiume na akategemea mtoto wa nne akizaliwa atakuwa wa kike na badala yake akazaliwa tena kiume basi mtoto huyo ataitwa (Byalugaba) ikiwa na maana haya ni ya Mungu yaani yeye ndiye anayetoa.
Mama akizaa watoto wengi wa kike akaja kuzaa mtoto wa kiume mtoto huyo ataitwa (Karumuna) ikiwa na maana kama ni mdogo wa baba.
Rwehangura anaelezea kuwa endapo kutakuwa na vurugu katika ukoo, ndugu hawaelewani kisha akazaliwa  mtoto ndugu wakapatana  basi akiwa mtoto wa kiume ataitwa (Mombeki) na akiwa wa kike ataitwa (Kimilembe) ikiwa na maana ya mpatanishi au mjenzi wa familia.
Jina la Rweyemamo ni mtoto anayeweza kujisimamia mwenyewe yaani ikiwa mtoto aliyetangulia kuzaliwa mbele yake ana matatizo ya kiafya na hivyo atakapozaliwa yeye akawa mzima atapewa jina hilo ili ajisimamie mwenyewe.
Rwehangura anaelezea kuwa endapo kuna ndugu katika ukoo amepotea miaka mingi inawezekana katika kwenda kutafuta maisha na ndugu mkakata tamaa ,mara mtu huyo akarudi ama zikaja taarifa ameonekana sehemu fulani na mkawasiliana naye hata kama hajarudi nyumbani,wakati huo akazaliwa mtoto ataitwa (Kamzora) ikiwa na maana ya ameonekana.
Ikiwa mtoto amezaliwa nje ya ndoa  atapewa jina la (Rwechengura) ikiwa na maana anayejidhamini yaani mtoto huyo baadaye atakuja mwenyewe hivyo ni mtoto anayeweza kujidhamini mwenyewe.
Rwehangura anaeleza kuwa ikiwa baba ameitelekeza familia yake na kisha akarudi na mtoto akazaliwa  mtoto huyo ataitwa (Kabigumila) ikiwa na maana mvumilivu kwa hiyo jambo lolote anaweza kuvumilia.
Endapo mtoto atazaliwa mgonjwa sana halafu akaja akapona ataitwa jina la (Rweombiza) ikiwa na maana ya amejiombea mwenyewe.

Habari kwa hisani ya radio Tumaini

No comments:

Post a Comment