SIKU chache
baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (necta), kutangaza matokeo ya
kidato cha sita na kuonekana shule ya Sekondari ya St. Joseph
inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, kufanya
vizuri, Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo,
ameutahadharisha uongozi wa shule hiyo kuepuka vitendo vya rushwa.
Aidha Kardinali Pengo alionya kuwa endapo uongozi wa Shule ya
Sekondari ya Mtakatifu Joseph itaruhusu mwanya wa rushwa kwa baadhi ya
wazazi wenye fedha kuwapatia nafasi ya masomo watoto wao kwenye shule
hiyo, ijiandae kupata matokeo mabaya.
Kardinali Pengo alitoa tahadhari hiyo hivi karibuni wakati alipokuwa
akizungumza na kuwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika matokeo ya
kidato cha sita kutoka shule ya Sekondari ya Mtakatifu Joseph, hafla
iliyofanyika nyumbani kwake Kurasini, jijini Dar es Salaam.
“Inapotokea shule fulani inakuwa bora wazazi wengi hukimbilia
kupeleka watoto wao, huku baadhi ya wazazi wenye fedha kutanguliza
rushwa ili waweze kuwapatia watoto wao nafasi hata kama hawana sifa za
kuwepo katika shule:
Hali hii ikitokea katika shule ya Mtakatifu Joseph inaweza kuleta
matokeo mabaya sana na hatimaye kudidimia na kuanza kuuliza ile namba
moja iko wapi?”,alisema Kardinali Pengo.
Hata hivyo Kardinal Pengo alisema anashangazwa na nidhamu
iliyoonyeshwa na wanafunzi wa shule hiyo kwa kuwa si jambo rahisi
kufaulu na kuwa na nidhamu hususan katika jiji la Dar es Salaam na
kusema kuwa nidhamu imewasaidia kufanya vizuri katika mitihani hiyo.
Kardinali Pengo alisema ni jambo la faraja na furaha kwa Kanisa kwa
kuwa mafanikio hayo ni mkakati wa Kanisa Katoliki na Makanisa mengine
kupandisha kiwango cha elimu nchini baada ya kiwango hicho nchini
kuyumba, hali inayoleta faraja katika shule za Kanisa kwa ujumla.
“Ilikuwa ni muhimu kwa Kanisa na tulikubaliana na makanisa mengine
kufanya kitu ili kupandisha Elimu ya Tanzania na kila Askofu lazima awe
na shule moja ya awali , Shule ya msingi na sekondari ya kidato cha tano
na sita ingawa jitihada hizo za kanisa kupandisha elimu ilileta
changamoto kwa Serikali ”,alisema Kardinali Pengo.
Akizungumzia kushuka kwa baadhi ya Shule za Kanisa hususan Seminari
Kardinali Pengo alisema pamoja na shule za Kanisa kuwa 10 bora kwa miaka
mingi hatuwezi kusema daima 10 bora ni za makanisa, hivyo hayo ni
matokeo kama yalivyo matokeo mengine.
“Tuna sababu ya kufurahi lakini pia ni changamoto kwa walimu wa shule
ya Sekondari ya Mtakatifu Joseph ili isije kuonekana hapa mmebahatisha,
ingawa si lazima mbaki namba moja lakini hatutegemei mshuke…hivyo ni
changamoto kubwa kwa shule yenu”,alisema Kardinali Pengo.
Licha ya kuwapongeza wanafunzi hao Kardinali Pengo alisononeshwa na
ushindi huo kuwa wa wavulana na kutilia shaka ya dhana iliyowekwa na
baadhi ya watu kuwa mwanaume ndiyo kila kitu, huku akitoa wito kwa
wasichana wa shule hiyo kufanya mabadiliko katika mtihani ujao kwa
kushika nafasi za juu kama ilivyokuwa kwa wavulana katika shule hiyo.
Akizungumzia suala la Kanisa kuwa na shule nyingi za wasichana kuliko
za wavulana Kardinali huyo, alisema sababu ya kanisa kuweka shule
nyingi za wasichana kwa kuwa kanisa liliona wasichana wamebaki nyuma
kutokana na historia yao ya kutoka nyumbani ya kwamba wasichana hawana
umuhimu katika suala la kupata elimu na wavulana ndiyo waliokuwa
wanaonekana wanafaa, hivyo kanisa liliona taifa letu linaweza kuwa na
wasomi wengi wavulana.
Kwa mujibu wa Kardinali huyo, alisema wasichana wenye kiwango cha juu
cha elimu ni shida kupata mwanaume wa kiwango chake na hivyo
kusababisha kukosa mume.
Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo Sista Theodora Faustine
alizungumzia changamoto inayowakabili katika shule hiyo kuwa ni
pamoja na wanafunzi wa kike kuwa wachache ikilinganishwa na wavulana
kwani robo tatu ya wanafunzi katika shule hiyo wasichana na kusema kuwa
hali hiyo inasababishwa na kuwepo kwa shule nyingi za wasichana katika
kanisa kuliko za wavulana.
Sista Faustine aliongeza kuwa matokeo hayo yamewapa faraja wanafunzi
wa shule hiyo kwa kuwa kutokana na ufaulu mzuri walioupata wanafunzi
wote wanaenda vyuo vikuu.
Wanafunzi hao waliofanya vizuri kitaifa ni pamoja na Isaac Shayo
ambaye ameshika nafasi ya kwanza kwa mwanafunzi bora kitafa ikiwa pamoja
na mwanafunzi aliyefanya vizuri katika masomo ya Sayansi kitaifa,
Joseph Ngobya aliyeongoza katika masomo ya sanaa na Prince Mwambaja
aliyeongoza katika masomo ya biashara.
Isaac Shayo alibainisha siri ya mafanikio yake kuwa ni pamoja na
wazazi wake kumsaidia katika mahitaji yake ya shule ikiwemo Mwalimu mkuu
wa shule hiyo kuwaongoza vema kusoma vitabu mbalimbali ambavyo
vimewasaidia na kuwaletea mafanikio makubwa.
Habari kwa hisani ya radio tumaini
No comments:
Post a Comment