Saturday, August 9, 2014

Ugonjwa wa Ebola ni tishio kwa usalama wa umma na unapaswa kushughulikiwa kimataifa!

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, DR. Margaret Chan, baada ya mkutano wa siku mbili kuhusu dharura ya ugonjwa wa Ebola unaoendelea kuenea katika nchi kadhaa, Afrika Magharibi, Ijumaa tarehe 8 Agosti 2014 ametangaza rasmi kwamba, ugonjwa wa Ebola ni tishio kwa usalama wa umma na kwamba, ni janga linalopaswa kushughulikiwa kimataifa!

Watalaam wa Shirika la Afya Duniani wametangaza kwamba, ugonjwa huu unapaswa kushughulikiwa na kuratibiwa na Jumuiya ya Kimataifa, ili kuuzuia usienee sehemu nyingine zaidi, kwani athari zake zinavuka mipaka ya nchi husika. Shirika la Afya Duniani linatarajia kutoka maelekezo kwa nchi wanachama ili kuangalia namna ya kuweza kuzuia ugonjwa wa Ebola usienee zaidi.

Takwimu zinaonesha kwamba, hadi kufikia Ijumaa, tarehe 8 Agosti 2014, wagonjwa elfu moja wa Ebola wamekwishafariki dunia. Hali ni mbaya nchini Liberia, Guinea na Sierra Leone. Watu kutokana na hofu ya kuambukizwa na ugonjwa wa Ebola wanahofia hata kuwazika ndugu zao na kuwaacha barabarani, hali ambayo ni hatari zaidi.

Liberia imetangaza hali ya hatari kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa Ebola baada ya hatua za dharura zilizokuwa zimechukuliwa na Serikali yake kwa kipindi cha majuma mawili, kushindwa kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Ebola. Watu katika huduma zisizo za lazima kwa muda wa siku thelathini watapaswa kubaki majumbani mwao. 

 Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment