Friday, October 3, 2014

JINSI YA KUSALI ROZARI YA MAMA BIKIRA MARIA


ROZARI TAKATIFU YA MAMA BIKIRA MARIA

Anza kusali Rozari kwa kuibusu miguu ya Bwana Yesu katika taswira (picha) yake Msalabani kisha fanya Ishara ya Msalaba ukiwa unasema “Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina”.

 

Taja kwa ufupi nia za Rozari hii. Tangaza nia hizo kwa sauti kama mnasali wengi kwa pamoja, Mfano, “Tusali kuombea amani katika nchi yetu na ulimwenguni kote, na tuunganishe nia hizo na nia zetu sisi wenyewe, nk) .

 

Baada ya Sala ya Nasadiki pamoja na ya Baba Yetu, tunamwomba Mungu (Utatu Mtakatifu) fadhila za Imani, Matumaini na Mapendo, zikiambatana na Salamu Maria tatu.

 

Mojawapo ya maneno yafuatayo huweza kutumika:

“Mungu Baba utuongezee Imani. Salamu Maria, …… Mungu Mwana utuongezee matumaini, Salamu Maria, …… Mungu Roho Mtakatifu washa nyoyo zetu kwa mapendo yako, Salamu Maria, …..” Au;

“Utuongezee Imani ee Bwana, Salamu Maria,…. Utuongezee matumaini ee Bwana, Salamu Maria,…. Uwashe nyoyo zetu kwa mapendo yako ee Bwana, Salamu Maria, …..” Au;

“Salamu e uliyechaguliwa na Mungu Baba, Salamu Maria,….. Salamu e Mama wa Mungu Mwana, Salamu Maria,….. Salamu e Mchumba wa Mungu Roho Mtakatifu, Salamu Maria,……”

Atukuzwe Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo na sasa na siku zote, na milele, Amina.

Ee Yesu wangu, utusamehe dhambi zetu, utuepushe na moto wa milele, ongoza roho zote mbinguni, hasa za wale wanaohitaji huruma yako zaidi.

Tuwasifu milele, Yesu, Maria na Yosef.

Kisha endelea na sala zinazofuata kama mpangilio unavyoonyesha hapo juu.

Kila baada ya Tendo moja na makumi ya Salamu Maria…, “Atukuzwe..”, “Ee Yesu wangu…” na “Tuwasifu milele...” kama muda unatosha wimbo ufaao wa Bikira Maria uimbwe (kama muda ni mfupi basi angalau ubeti mmoja mmoja uimbwe kila baada ya makumi hayo). Baada ya Wimbo, Tendo linalofuata litangazwe kwa sauti pamoja na tafakari fupi au ombi linaloambatana na Tendo husika kama inavyoonyeshwa hapa chini.

 

 

MATENDO YA ROZARI TAKATIFU

MATENDO YA FURAHA (Jumatatu na Jumamosi)

 

Tendo la kwanza; Malaika Gabrieli anampasha habari Maria kuwa atakuwa Mama wa Mungu. Tumwombe Mungu  atujalie unyenyekevu.

 

Tendo la pili; Maria Mtakatifu anakwenda kumtembelea Elizabeti. Tumwombe Mungu atujalie mapendo ya jirani.

 

Tendo la tatu; Yesu anazaliwa Betlehemu. Tumwombe Mungu atujalie moyo wa ufukara

 

Tendo la nne; Yesu anatolewa hekaluni. Tumwombe Mungu atujalie usafi wa moyo.

 

Tendo la tano; Maria anamkuta Yesu hekaluni. Tumwombe Mungu atujalie kuwatii wakubwa wetu.

 

MATENDO YA UCHUNGU (Jumanne na Ijumaa)

 

Tendo la kwanza; Yesu anatoka jasho la damu kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie sikitiko la dhambi.

 

Tendo la pili; Yesu anapigwa kwa mijeledi kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie kuacha dhambi za uchafu.

 

Tendo la tatu; Yesu anatiwa miiba kichwani kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie kushinda kiburi.

 

Tendo la nne; Yesu anachukua Msalaba kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie kuvumilia taabu.

 

Tendo la tano; Yesu anakufa Msalabani. Tumwombe Mungu atujalie kuwapenda Yesu na Maria.

 

 

MATENDO YA UTUKUFU (Jumatano na Jumapili)

 

Tendo la kwanza; Yesu anafufuka. Tumwombe Mungu atujalie kugeuka watakatifu.

 

Tendo la pili; Yesu anapaa mbinguni. Tumwombe Mungu atujalie kwenda mbinguni.

 

Tendo la tatu; Roho Mtakatifu anawashukia Mitume. Tumwombe Mungu atujalie bidii katika dini yetu.

 

Tendo la nne; Bikira Maria anapalizwa mbinguni. Tumwombe Mungu atujalie kufa vizuri.

 

Tendo la tano; Bikira Maria anawekwa Malkia mbinguni. Tumwombe Mungu atujalie kudumu katika njia njema.




MATENDO YA MWANGA (Alhamisi)

 

Tendo la kwanza; Yesu anabatizwa Mto Jordani. Tumwombe Mungu atujalie uaminifu kwa ahadi zetu za ubatizo.

 

Tendo la pili; Yesu anageuza maji kuwa divai huko Kana. Tumwombe Mungu atujalie kuukoleza ulimwengu kwa chachu ya enjili.

 

Tendo la tatu; Yesu anatangaza Ufalme wa Mungu. Tumwombe Mungu atujalie kupokea Ufalme wake kwa toba ya kweli.

 

Tendo la nne; Yesu anageuka sura. Tumwombe Mungu atujalie neema ya kuung’arisha ulimwengu kwa uso wa Yesu.

Tendo la tano; Yesu anaweka Sakramenti ya Ekaristia. Tumwombe Mungu atujalie neema ya kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine.

 

*******

6 comments: