Baba
Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 16 Januari 2015 ameadhimisha Ibada
ya Misa Takatifu kwa ajili ya Wakleri, Watawa na Majandokasisi kutoka
nchini Ufilippini pamoja na wawakilishi kutoka katika nchi mbali mbali
Barani Asia, kwani hija hii ni kwa ajili ya Bara la Asia katika ujumla
wake. Ibada hii imefanyika kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa
Dhambi ya Asili, Jimbo kuu la Manila.
Katika mahubiri yake kwa
namna ya pekee kabisa Baba Mtakatifu ameitaka Familia ya Mungu nchini
Ufilippini kuonesha upendo wa dhati kwa Kristo pamoja na kutoa
kipaumbele cha kwanza kwa maskini, kwani hawa ni hazina kubwa ya Injili.
Amewakumbusha viongozi wa Kanisa pamoja na watawa kwamba, ufuasi na
upendo wao kwa Kristo unasaidia kukuza mchakato wa upatanisho.
Kama
sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 500 ya Ukristo
nchini Ufilippini, yatakayofikia hatima yake kunako mwaka 2021, Baba
Mtakatifu anasema kwamba, kizazi kilichopita kimesaidia kwa kiasi
kikubwa watu kufahamu Neno la Mungu, tunu msingi za maisha ya Kikristo,
ambazo zimemwilishwa katika huduma ya mapendo, upatanisho, mshikamano na
mafao ya wengi. Tunu hizi zimeimarisha si tu wakati wa mahubiri au
ujenzi wa Kanisa nchini Ufilippini, bali pia zimesaidia kumwilisha
Injili ya Upendo, msamaha, mshikamano na huduma kwa ajili ya mafao ya
wengi.
Baba Mtakatifu anawaalika vijana wa kizazi kipya
kuhakikisha kwamba, wanajenga madaraja yatakayolisaidia Bara la Ulaya
kupokea Neno la Mungu. Watu hawana budi kuonesha upendo kwa Kristo
anayewaletea upatanisho wa kweli. Mchakato wa kukutana na Yesu hauna
budi kuwakirimia waamini wongofu pamoja na kuchunguza dhamiri kama mtu
binafsi na jamii katika ujumla wake. Injili ya Kristo haina budi
kusaidia mchakato wa ujenzi wa jamii imara inayojikita katika msingi wa
haki na kukombolewa.
Baba Mtakatifu anawapongeza Maaskofu
Katoliki nchini Ufilippini wanaosimama kidete kupambana kufa na kupona
na mambo yanayosababisha ukosefu wa haki na usawa katika jamii. Injili
inamchangamotisha kila mwamini kuhakikisha kwamba, anaishi kwa
kuzingatia misingi ya uaminifu, ukweli pamoja na kujisadaka kwa ajili ya
mafao ya wengi. Injili inawataka Wakristo kujenga na kudumisha makundi
ya watu waaminifu; wenye kushikamana pamoja na kujitoa kwa ajili ya
kuleta mageuzi ndani ya jamii kwa njia ya ushuhuda wa kinabii.
Baba
Mtakatifu Francisko kwa kuiangalia changamoto hii, anawataka kwa namna
ya pekee, Wakleri na watawa kujenga utamaduni wa kusali kila siku kama
sehemu ya mchakato wa kukutana na Kristo pamoja na kupambana kufa na
kupona, ili kukataa kishawishi cha kutaka kumezwa na malimwengu;
ubinafsi pamoja na kupenda mali badala yake, wawe ni watu wanaojisadaka
kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jirani zao; watu wakweli na
waaminifu; wanaosaidia ustawi na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na
kimwili; tayari kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kueneza Injili katika
jamii inayojikita kwenye ubaguzi, mvuto usiokuwa na mashiko pamoja na
kashfa ya ukosefu wa misingi ya usawa.
Baba Mtakatifu anawataka
Maaskofu kutoa kipaumbele cha pekee kwa Mapadre vijana, watawa na
majandokasisi, ambao walikuwa wamefurika kwa wingi katika Ibada hii ya
Misa Takatifu, wanaoweza kuchanganyikiwa n akukata tamaa, lakini bado
wanaendelea kuliona Kanisa kama mwenzi katika hija ya maisha yao na
chemchemi ya furaha. Kanisa linapaswa kuwa karibu zaidi na wale wote
wanaoelemewa na umaskini, rushwa na ufisadi, kiasi cha kujikatia tamaa,
kiasi hata cha kuingiwa na kishawishi cha kuacha masomo na kujitosa
barabarani.
Baba Mtakatifu anawataka Wakleri kutangaza uzuri na
ukweli wa ndoa ya Kikristo katika jamii ambamo kuna mambo mengi ambayo
yanaendelea kuwachanganya watu kuhusiana na maisha ya ndoa na familia.
Huu ni ukweli ambao unakabiliwa na changamoto nyingi, zinazotaka
kuathiri mpango wa kazi ya uumbaji na kupotosha ukweli wa tunu msingi
za maisha zilizounda na kujenga uzuri wa utamaduni wa Ufilippini.
Baba
Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake kwa Wakleri, Watawa na
Majandokasisi kwa kusema kwamba, miaka 500 ya Ukristo nchini humo si
haba, kwani imesaidia kujenga upendo mkubwa kwa Mwenyezi Mungu, Ibada
kwa Bikira Maria na Rozari Takatifu, muhtasari wa Injili. Hapa kuna
nguvu kubwa inayoweza kusaidia mchakato wa umissionari unaopaswa
kusaidia utamaduni wa Kikristo miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ili
ari na moyo wa Kikristo uweze kupenya na hatimatimaye kuota mizizi
katika jamii ya Wafilippini na kwa njia yao, jamii nyingine sehemu mbali
mbali za dunia.
Naye Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu
wa Jimbo kuu la Manila katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu
kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, ametambua uwepo wa uwakilishi
wa Familia ya Mungu kutoka Barani Asia. Kanisa kuu la Manila ni
kielelezo makini cha wananchi wa Ufilippini, Kanisa ambalo limekumbana
na majanga mbali mbali katika historia, lakini bado liko imara; Pande
zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa.
Furaha ya wananchi wa Ufilippini inajikita katika muziki na imani
inayowawezesha kusimama tena na kusonga mbele baada kukumbwa na majanga
mbali mbali katika maisha.
Kardinali Luis Antonio anasema, uwepo
wa Baba Mtakatifu Francisko kati yao ili kuwaletea moto unaowatakasa;
tetemeko linalowaamsha, anawaletea silaha ili kuwalinda na kuendelea
kulijenga Kanisa la Kristo sanjari na kuwaimrisha ndugu zake katika
imani, matumaini na mapendo.
Mara tu baada ya Ibada ya Misa
Takatifu, Papa Francisko amekwenda kuwatembelea na kuwaslimia watoto
wanaoishi katika mazingira magumu wanaotunzwa na Kituo cha TNK
kilichoanzishwa na Padre Mathieu. Baba Mtakatifu amezungumza na watoto
hawa, akapiga nao picha za kumbu kumbu na baadaye wakampatia zawadi ya
Sanamu ya Bikira Maria na zawadi nyingine, mwishoni, anasema Padre
Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican, Baba Mtakatifu akawabariki
na hatimaye kuendelea na ratiba yake.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Lengo kuu ya jumuiya yetu ni kumtangaza Bwana YESU aliye alfa na omega katika historia ya wokovu wa binadamu wote hapa duniani.
Pages
- Home
- MALENGO YA JUMUIYA
- NGUVU YA ROZARI TAKATIFU
- PICHA ZA BWANA YESU
- AMRI ZA MUNGU
- AMRI ZA KANISA
- MFUMO WA UONGOZI
- SALA YA ASUBUHI
- SALA YA JIONI
- SALA MBALI MBALI
- MASOMO YA JUMAPILI NA TAFAKARI
- UMUHIMU WA SKAPULARI
- MAPAJI SABA YA ROHO MTAKATIFU
- KATEKISIMU KATOLIKI
- UFASIRI WA BIBLIA KATIKA KANISA
- “ROZARI YA BIKIRA MARIA”
- NANI MWABUDU SANAMU ?
- CONTACT US
- PICHA ZA BIKIRA MARIA
- HISTORIA NA UKUU WA BIKIRA MARIA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment