Saturday, May 16, 2015

Mkutano mkuu wa 68 wa CEI kufunguliwa na Papa Francisko mjini Vatican



Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu jioni tarehe 18 Mei 2015 majira ya saa 10: 30 anatarajiwa kufungua mkutano mkuu wa 68 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI unaojikita katika tafakari ya kina kuhusu Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, Injili ya Furaha, Evangelii gaudii. Mkutano huu utafanyika kwenye Ukumbi wa Sinodi mjini Vatican. Kardinali Angelo Bagnasco Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, Jumanne tarehe 19 Mei 2015 baada ya hotuba yake elekezi, Maaskofu wataendelea na mkutano wao hadi tarehe 21 Mei 2015.
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linapenda kufanya upembuzi wa kina kuhusu Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko Injili ya Furaha. Kati ya mambo mengine yaliyopangwa kwenye ajenda ni pamoja na maandalizi ya maadhimisho ya Kongamano la tano la Kanisa Kitaifa, litakalofanyika Jimbo kuu la Firenze kuanzia tarehe 9 hadi 13 Novemba 2015.
Maaskofu wataendelea kuangalia maboresho kuhusiana na maisha pamoja na majiundo awali na endelevu kwa Wakleri nchini Italia. Maaskofu pia watajipanga vyema ili kushiriki kikamilifu katika maadhimisho  ya uzinduzi wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, utakaozinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2015. Itakuwa ni nafasi pia kupitisha bajeti ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia.
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, Jumatano tarehe 20 Mei 2015 litaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuongozwa na Kardinali Marc Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maaskofu na Alhamisi, tarehe 21 Mei 2015, Kardinali Angelo Bagnasco atazungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo yatakayokuwa yamejiri kwenye maadhimisho ya mkutano mkuu wa 68 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Habari kwa hisani  ya Radio Vatican.

No comments:

Post a Comment