Tuesday, August 18, 2015

Ndoa kadiri ya mpango wa Mungu ni kati ya Bwana na Bibi na wala si vinginevyo!

Kanisa linasadiki na kufundisha kwamba, Mwenyezi Mungu ambaye ni asili na kiini cha upendo amemuumba mtu kwa upendo na amemwita kupenda. Kwa kuumba mwanaume na mwanamke, aliwaita katika Ndoa kuwa na umoja wa dhati wa maisha na upendo kati yao, ndiyo maana si wawili tena, bali wamekuwa ni mwili mmoja. Mwenyezi Mungu amewabariki ili wazae na kuongezeka. Mafundisho ya Kanisa kuhusu ndoa yanaweza yasiwafuraishe baadhi ya watu ndani ya jamii lakini yataendelea kubaki jinsi yalivyo.
Huu ni mkazo ambao umetolewa hivi karibuni na Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria wakati alipokuwa anatembelea Jimbo Katoliki la Makurdi. Itakumbukwa kwamba, wakati wa ziara yake ya kikazi Barani Afrika hivi karibuni, Rais Barack Obama wa Marekani akiwa nchini Kenya pamoja na mambo mengine aliitaka Serikali ya Kenya kuheshimu uhuru wa watu wanaoshabikia ndoa za watu wa jinsia moja na kamwe wasibaguliwe. Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alijibu na kusema, ndoa za watu wa jinsia moja si kipaumbele cha Serikali ya Kenya.
Msimamo huu wa Rais Barack Obama umechafua mawazo ya wanachi wengi Barani Afrika kwa kusema kwamba, huu si utamaduni wa kiafrika na wala si kielelezo cha haki msingi za binadamu. Kardinali Onayekan anasema, Kanisa litaendelea kutangaza kweli na shuhuda za Kiinjili kwa watu wa mataifa, hata kama kumong’onyoka kwa misingi ya maadili na utu wema kunaonekana kuwa ni haki binafsi.
Kardinali Onayekani anasikitika kusema kwamba, mambo kama ndoa za watu wa jinsia moja yanaonekana kuwa ni mambo ya kawaida, kiasi hata cha kutungiwa na kushabikiwa na sheria. Hata kama yamekubalika katika baadhi ya nchi si kweli kwamba ni matendo ya haki. Hakuna ndoa ya kweli kadiri ya mpango wa Mungu kati ya watu wa jinsia moja.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Habari:Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CISA.

No comments:

Post a Comment