Sunday, April 27, 2014

Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo: Je, Kristo amegawanyika?


Wakristo wanakumbushwa kwamba, jitihada za kuombea umoja wa Kanisa ni mchakato endelevu unaopaswa kutekelezwa katika hija ya kila siku ya mwamini katika kipindi cha mwaka mzima. Lakini Makanisa yametenga kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari, Siku kuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mwalimu wa Mataifa kuwa ni Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo; tukio ambalo lilianzishwa kunako Mwaka 1926 na Paul Wattson. RealAudioMP3

Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa linalohamasisha Umoja wa Wakristo utayarisha masomo na sala kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo, masomo na sala hizi zinaweza kutungwa kadiri ya hali na mazingira ya Makanisa husika ili kukoleza zaidi ari, moyo na majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Makanisa.

Neno la Mungu linaloongoza Maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2014 ni kutoka katika Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho 1: 1-17. Je, Kristo amegawanyika? Sala na tafakari kwa mwaka huu, zimeandaliwa na Wakristo kutoka Canada, nchi ambayo ina tofauti kubwa ya lugha, tamaduni na hali ya hewa. Mwelekeo huu unajionesha pia kwa Wakristo waliogawanyika katika Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo nchini humo, jambo linaloonesha kashfa ya utengano miongoni mwa Wakristo!

Canada ni nchi ambayo ina utajiri mkubwa wa rasilimali na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Mtakatifu Paulo katika Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho anazungumzia kuhusu kashfa ya mgawanyiko unaojionesha katika Kanisa la Mungu na kwamba, wanaitwa kuwa ni Watakatifu kwa kushirikiana na wote wanaomuungama Kristo na kuendelea kupokea neema, baraka na amani zinazobubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe. Wakristo wanaulizwa, ikiwa kama wamefanikiwa kuonja neema ya Mungu na amani katika Makanisa yao mahalia. Wakristo wanachangamotishwa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano kati yao na Mwenyezi Mungu.

Waamini wanakumbushwa kwamba, Kristo hakugawanyika, bali ni yule yule aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu, Wote hata katika utofauti wao, wanaalikwa kujishikamanisha na Kristo pamoja na jirani zao, ili kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa; hatimaye, kuelekea katika umoja kamili kama ambavyo Yesu Kristo mwenyewe aliwaombea wafuasi wake.

Wakristo wanapaswa kukumbuka kwamba, wao kama wafuasi wa Kristo kama anavyosema Mtakatifu Paulo wanaunganishwa pamoja kwa njia ya Imani katika Ubatizo na Msalaba wa Kristo, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu wote. Umoja wao unafumbatwa katika Kristo, wokovu na maisha ya uzima wa milele yanayobubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe.
Imani ndiyo inayowawezesha kutembea pamoja kama Wafuasi wa Kristo, tayari kutoka kifua mbele kutangaza Habari Njema ya Wokovu, waliyoipokea katika imani na furaha. Wakristo waendelee kutafakari ikiwa kama wamekuwa kweli ni sehemu ya Habari Njema ya Wokovu kwa jirani zao au bado wanaendelea kuendekeza utengano kwa jina la Yesu Kristo na hivyo kufisha nguvu ya Msalaba wa Kristo.

Wakristo waendelee kushirikiana katika mapambano dhidi ya ujinga, umaskini ma maradhi; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Kila Mkristo adhamirie moyoni mwake kujenga na kuimarisha umoja wa Wakristo. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja ya kutubu na kuongoka na kuanza kutafuta njia mpya za kushuhudia Injili ya Kristo katika umoja na mshikamano.

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment