Sunday, April 27, 2014

Asanteni sana, kuwa kufanikisha tukio hili la kihistoria!



Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuhitimisha adhimisho kuu la imani kwa kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu, Jumapili tarehe 27 Aprili kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican amewashukuru watu wote waliofika kushuhudia tukio hili la kihistoria. Amewashukuru watu wote wa Mungu, wawakilishi kutoka katika nchi mbali mbali waliofika kushuhudia mchango uliotolewa na Watakatifu waliotangazwa na Mama Kanisa, Siku ya Jumapili ya Huruma ya Mungu, katika ustawi, maendeleo na amani kati ya watu.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, amewashukuru viongozi wa Serikali ya Italia kwa ushirikiano wao makini uliosaidia kufanikisha maadhimisho haya. Ametambua uwepo wa mahujaji kutoka Jimbo Katoliki la Bergamo, Italia na Krakovia, Poland, changamoto na mwaliko wa kuwaenzi miamba hawa wa imani kwa njia ya kumwilisha mafundisho yao katika matendo.

Baba Mtakatifu amewashukuru viongozi wa Jimbo kuu la Roma na Jiji la Roma katika ujumla wake walioshiriki kwa namna ya pekee katika maandalizi na maadhimisho ya tukio hili la kihistoria, vikosi vya ulinzi na usalama, mashirika mbali mbali na vikundi vya kujitolea.

Baba Mtakatifu amewakumbuka waamini, mahujaji na watu wenye mapenzi mema waliokuwa wamefurika kwenye barabara na viunga vya mji wa Vatican ili kushuhudia tukio hili la kihistoria kwa njia ya vyombo mbali mbali vya mawasiliano ya kijamii. Amewakumbuka, wagonjwa na wazee ambao kwa hakika walikuwa na upendeleo wa pekee katika maisha na utume wa Watakatifu wapya.

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment