Sunday, April 27, 2014

Madonda matakatifu ya Yesu ni kashfa na uhakika wa imani!



Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake tarehe 27 Aprili 2014 Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Huruma ya Mungu iliyoanzishwa na Yohane Paulo wa Pili, anasema inatawaliwa na madonda matakatifu ya Yesu Kristo Mfufuka, baada ya kuwatokea mitume wake, Toma ambaye hakuwepo jioni ile alipoambia hakusadiki na akataka kuhakikisha mwenyewe kwa kuweka vidole vyake kwenye madonda matakatifu ya Yesu, kitendo ambacho kilifanywa na Yesu mwenyewe siku nane baadaye!

Yesu Kristo mfufuka anamwambia Mtakatifu Toma kugusa madonda yake matakatifu, hapo Toma akaonesha unyofu wake kwa kuhakiki mwenyewe na hatimaye, akapiga magoti mbele ya Yesu na kukiri ukuu wake kwa kusema "Bwana wangu na Mungu wangu".

Baba Mtakatifu anasema, madonda matakatifu ya Yesu ni kashfa kwa imani, lakini pia yanasaidia kuhakiki imani, kwani madonda matakatifu ni kielelezo cha upendo wa hali ya juu wa Mwenyezi Mungu kwa binadamu. Madonda haya si kwa ajili ya kuthibitisha kwamba, Mungu yuko bali ni kuonesha kwamba, Mungu ni upendo, ni mwenye huruma na mwaminifu, kwani kwa kupigwa kwake ninyi mmeponywa.

Watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II walikuwa na ujasiri wa kuyaangalia madonda matakatifu ya Yesu na kugusa kwa mikono yao ubavu uliotobolewa kwa mkuki. Ni watu ambao hawakuonea aibu Kashfa ya Msalaba wa Yesu au mateso ya jirani zao, kwani katika mateso na mahangaiko ya kila mtu, walimwona Yesu. Ni viongozi wawili waliokuwa na ujasiri mkubwa, waliojazwa na nguvu ya Roho Mtakatifu, wakatolea ushuhuda wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo, huku wakionesha upendo na huruma ya Mungu.

Hawa wamekuwa ni Mapadre, Maaskofu na Mapapa wa Karne ya ishirini na moja walionja majanga ya maisha ya mwanadamu bila kukata tamaa. Mwenyezi Mungu alionekana kuwa na nguvu zaidi katika maisha yao, wakaonesha imani thabiti kwa yesu Kristo Mkombozi wa binadamu na Bwana wa historia; huruma ya Mungu iliyojionesha katika madonda matano ya Yesu, ilikuwa na nguvu zaidi na kwamba, Bikira Maria Mama wa Mungu, alionesha ukaribu wake.

Viongozi hawa wawili waliotafakari madonda ya Yesu na kutolea ushuhuda wa huruma ya Mungu, walivikwa matumaini, furaha na utukufu wa Mungu. Baba Mtakatifu anasema, matumaini na furaha ya Kristo Mfufuka, hakuna mtu anayeweza kuwapokonya wafuasi wa Kristo, ni furaha inayobubujika kutoka katika mateso na hali ya kujisadaka, kwa kuonesha mshikamano na ukaribu kwa wadhambi hadi tone la mwisho la maisha, kiasi hata cha kukinywea Kikombe cha mateso.

Baba Mtakatifu anasema, haya ndiyo matumaini na furaha ya Watakatifu Mapapa waliotangazwa na Mama Kanisa, kwani wamepokea zawadi ya Kristo mfufuka na wakawaonjesha Watu wa Mungu kwa mapana zaidi, kwa kuthamini ushuhuda wao. Haya ndiyo matumaini na furaha iliyokuwa inabubujika kutoka katika Jumuiya ya kwanza ya Wakristo mjini Yerusalemu. Hii ni jumuiya iliyokuwa imejikita katika mambo msingi ya Kiinjili yaani: upendo, huruma, unyofu na udugu..

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ndiyo taswira ambayo Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wamependa kuiweka mbele ya maisha na utume wa Yohane XXIII na Yohane Paulo II, walioshirikiana bega kwa bega na Roho Mtakatifu katika kuleta mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa, mwelekeo ambao umeshuhudiwa na watakatifu katika historia na maisha ya Kanisa.

Kwa kuitisha maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Papa Yohane XXIII ameonesha unyenyekevu mbele ya Roho Mtakatifu, akampatia nafasi ya kumwongoza, kiasi kwamba, akawa kweli: mchungaji, kiongozi na mwongozwaji. Huu ndio mchango wake mkuu katika huduma kwa Mama Kanisa; amekuwa ni Papa aliyejinyenyekesha mbele ya Roho Mtakatifu.

Katika huduma kwa Watu wa Mungu, Papa Yohane Paulo II atakumbukwa na wengi kuwa ni Papa wa familia, jambo ambalo limetiliwa mkazo na Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kuadhimisha Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili pamoja na familia. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II huko mbinguni, anaendelea kuliombea Kanisa.

Baba Mtakatifu anawaomba watakatifu waliotangazwa na Mama Kanisa kuliombea Kanisa katika kipindi cha miaka miwili, ili liweze kujinyenyekesha mbele ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa familia. Watakatifu hawa wawili wawafundishe waamini kutoona kashfa kuhusu madonda matakatifu ya Yesu, bali wawasaidie kuingia katika Fumbo la huruma ya Kimungu, inayotoa matumaini, inayosamehe kwani daima huruma hii inajikita katika upendo. 

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment