Monday, April 28, 2014

Oneni matendo makuu ya Mungu kwa Kanisa lake!



Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alipoingia kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu ya kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu amepokelewa kwa vigelegele na shangwe kubwa kutoka kwa waamini waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro pamoja na viunga vyake. Baba Mtakatifu mstaafu amesalimiana na baadhi ya Makardinali na viongozi wa Serikali waliokuwa karibu naye.

Kelele za furaha zilisikika pale Baba Mtakatifu Francisko walipokumbatiana na kusalimiana na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa Katoliki, kuwatangaza Mapapa wawili kuwa watakatifu katika Ibada ambayo imehudhuriwa na Mapapa wawili, mmoja akiwa ameng'atuka kutoka madarakani na mwingine akiwa bado anaendelea kuliongoza Kanisa la Kristo. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI ana historia kubwa na uhusiano wa pekee kabisa na Watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, amekwenda moja kwa moja kumsalimia na kumshukuru Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, kwa kuhudhuria katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa Watakatifu. Baba Mtakatifu pia alipata fursa ya kuzungumza na viongozi mbali mbali waliohudhuria kwenye Ibada hii.

Habari kwa hisani ya radio vatican


No comments:

Post a Comment