Wednesday, April 30, 2014

YESU KRISTO MFALME WA ULIMWENGU NDIYE MLANGO WA IMANI



Tunakuleteeni habari njema ya furaha tunapotafakari pamoja ujumbe wa Neno aliyefanyika mwili, Mfalme wa mbingu na nchi. Ni Dominika ya 34 ya mwaka B iliyo pia Sherehe ya Yesu Kristu Mfalme. RealAudioMP3

Kanisa linashangilia na kusherehekea utukufu wa Mwana wa Mungu, Yesu Kristo Mfalme. Kanisa linatangaza daima utawala na enzi ni vya Yesu Kristu mfalme na hivi lajiweka chini ya uongozi wake aliye kichwa na mwanga katika safari ya kuelekea mbinguni. Pamoja na tangazo hilo Kanisa latuhimiza kumfuata Yesu Kristu mfalme, kukiri ukuu wake wazi wazi machoni pa mataifa lililo hasa lengo la sherehe hii.

Nabii Ezekieli anatupa picha halisi ya mfalme aliye pia mchungaji mwema, aliye kinyume na wafalme wa dunia. Mchungaji wa kondoo anayetabiriwa na Ezekieli ni yule ambaye anatafuta kundi lake lililopotea na kulirudisha katika malisho safi na baadaye kulisalimisha pia nyumbani.

Kundi hili la kondoo ni wagonjwa, waliopotea waliovunjika moyo na waliofukuzwa. Picha hii ya mchungaji inajitokeza katika Yesu Kristu mfalme ambaye kwa njia ya msalaba watu wote wamerudishwa nyumbani. Kumbuka maneno yake alipokuwa akizungumza na Nikodemo “kama vile Musa alivyomwinua juu nyoka wa shaba kule jangwani naye mwana wa mtu atainuliwa juu vivyohivyo ili kila anayemwamini awe na uhai wa milele” Yn 3:14-15.

Katika somo la pili mtume Paulo akiwaandikia Wakorintho anatualika kusadiki kuwa Kristu ndiye limbuko letu. Ndiye ambaye amebatilisha kifo kwa njia ya msalaba wa ushindi. Anaonesha ufalme na ukuu wake kwa kushinda kifo kilicholetwa duniani kwa njia ya Adamu. Kwa ushindi dhidi ya kifo Mungu amemtukuza na kumwadhimisha mno, na hivi mwishoni mwa dunia utawala wa shetani utashindwa kabisa. Mtume Paulo hatangazi jambo jingine bali kuwa Yesu Kristo ni Mfalme ambaye Kanisa lamshangilia nakumtukuza kwa shangwe na vigelegele. Sisi wanakanisa tunapaswa kufuata mtililiko huohuo pasipo mashaka tukitangaza ushindi wa Bwana.

Mwinjili Mathayo anatuonesha mfalme mwenye mamlaka juu ya mbingu na dunia, mwenye uwezo wa kutoa hukumu kadiri ya upendo na haki. Mfalme huyu ameketi katika kiti cha enzi akiwabagua mataifa yote, wengine mkono wa kulia na wengine mkono wa kushoto. Ndiyo kusema kwanza ana enzi na mamlaka lakini pia ana haki.

Katika hukumu anayotoa yapo mambo msingi ambayo anayatazama. Kama mmoja aliwalisha maskini au hapana, kama mmoja aliwatazama wagonjwa ambao ni kielelezo cha uwapo wa sauti ya Mungu katikati ya jumuiya ya watu. Kigezo kingine ni kile cha kuwatazama wafungwa kifungoni, walio utumwani na wenye njaa. Kwa wale ambao waliwahudumia hawa wahitaji atawaambia kaeni mkono wa kulia na mkapate kula vilivyo vya Baba yangu maana nilipokuwa mgonjwa mlikuja kuniona hospitali. Kumbuka kuwa mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kwa hakika ukitazama vema lengo la ainisho hili la watu mbalimbali waliowahitaji, utagundua nguzo kuu ili mmoja aweze kuingia katika ufalme wa Mbinguni ni MAPENDO KWA JIRANI NA KWA MUNGU. Ni kushuhudia kwa dhati IMANI Katoliki, imani tendaji, imani inayokuza ubatizo hadi mwisho wa nyakati. Ni kubaki katika pendo la Mwana wa Mungu katika kuhudumu waliowake.

Mpendwa tunaposherehekea Sherehe ya Mfalme wetu tukumbuke kuwa yeye anapaswa kutawala katika familia zetu zote, katika maneno yetu na matendo yetu. Maneno kama “ mteja ni mfalme” yafaa kuangaliwa vizuri kama kweli yanakuza ufalme wa Kristu au ufalme wetu sisi wenyewe!

Tunawatakieni heri na baraka Waamini wote na zaidi wale ambao parokia zao na makanisa yao yako chini ya somo Yesu Kristo Mfalme. Mkashike imani na mtoe mfano wa kuigwa mkiongozwa na Yesu Kristu mfalme wa Amani. Tumsifu Yesu Kristo Mfalme.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya, C.PP.S.

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment