Mwandishi anaendelea kueleza uhusiano wa Mungu na
mwanadamu kupitia Bikira Maria kupitia Agano la Kale ambalo ni
matayarisho ya Agano Jipya. Agano Jipya lilianza rasmi kwa maneno ya
Bikira Maria alipojiweka mikononi mwa Mungu kwa niaba ya taifa jipya la
Mungu, yaani Kanisa: “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana; na iwe kwangu
kama ulivyosema.” Soma kwa makini.
Na Leonard Maliva AGANO la Kale lilikuwa ni matayarisho ya Agano
Jipya ndiyo maana Yesu anasema kuwa amekuja ili kulikamilisha. Kuna
sababu kuu mbili ambazo zinalifanya Agano la Kale liwe ni matayarisho na
lisiwe limekamilika: Agano la Kale lilifanywa kati ya Mungu na taifa
moja tu la Israeli kwa njia ya nabii Musa. Agano la Kale halikuwa na
nguvu ya kuiondoa dhambi ya asili iliyoletwa kwa njia ya shetani, Adamu
na Eva. Kwa njia ya Yesu Kristo, agano linakuwa sio tena kati ya Mungu
na Israeli, bali Agano Jipya kati ya Mungu na watu wote. Ni agano lenye
nguvu ya kuiondoa dhambi ya asili na dhambi binafsi. Kwa hiyo ni Agano
Jipya na la milele: Nao walipokuwa wakila, Yesu alitwaa mkate,
akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, “Twaeni, mle; huu
ndio mwili wangu.” Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema,
“Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano,
imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.”Mathayo 26:26-28
Agano hilo jipya na la milele lililoletwa na Yesu lilitabiriwa na
manabii tangu zamani kuwa litakuwa ni agano si la Waisraeli peke yao
bali ni la mataifa yote duniani. Nabii Isaya alilitangaza kuwa litakuwa
ni agano litakaloleta ukombozi kwa mataifa yote duniani yatakayomtambua
Mungu wa kweli: Hubirini, toeni habari, naam, na wafanye mashauri
pamoja! Ni nani aliyeonesha haya tangu zamani za kale? Ni nani
aliyehubiri hapo zamani? Si mimi, Bwana? Wala hapana mwingine zaidi ya
mimi. Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia, maana mimi
ni Mungu, hapana mwingine. Isaya 45:21-22 Nabii Yeremia pia alitabiri
habari za Agano Jipya miaka mingi kabla ya Yesu kuja duniani. Nabii
Yeremia alilitangaza agano hilo kuwa litahusu msamaha wa dhambi binafsi.
Dhambi binafsi ni tofauti na ile dhambi ya Asili. Dhambi ya Asili ni
ile tuliyoirithi toka kwa mama yetu Eva. Dhambi binafsi ni yetu wenyewe
tunapovunja amri za Mungu (agano la Sinai) kwa makusudi. Nabii Yeremia
pia analitofautisha Agano la Kale na Agano Jipya kwani katika Agano la
Kale amri za Mungu ziliandikwa katika mawe mawili, kumbe katika Agano
Jipya amri za Mungu zinaandikwa ndani ya mioyo ya watu: Angalieni, siku
zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli,
na nyumba ya Yuda. Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao,
katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri;
ambalo agano hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana.
Basi agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku
zile, asema Bwana: nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao
nitaiandika. Nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. …..Asema
Bwana; “maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena”.
Yeremia 31:31-33 Nabii Ezekieli naye alilitangaza Agano Jipya kuwa
litakuwa ni la milele na hasa litafanywa ili kurudisha amani kati ya
Mungu na mataifa yote ya dunia. Kwa njia ya agano hilo jipya, Mungu
ataweka makao yake kati ya watu wote na wote watamtambua kuwa ni Mungu
wao: “Tena nitafanya agano la amani pamoja nao, litakuwa agano la milele
pamoja nao. Nami nitawaweka na kuwazidisha, na patakatifu pangu
nitapaweka katikati yao milele. Tena maskani yangu itakuwa pamoja nao;
nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Na mataifa watajua ya
kuwa mimi ndimi Bwana, mimi niwatakasaye Israeli, patakatifu pangu
patakapokuwa katikati yao milele.” Ezekieli 37:26-28 Hivyo basi, neno
agano katika Historia ya Ukombozi linabeba uzito mkubwa katika kueleza
uhusiano wa Mungu na wanadamu. Hii ndiyo sababu Biblia inagawika katika
sehemu kuu mbili: Agano la kale na Agano Jipya. Katika Historia ya
Ukombozi, maneno kale na jipya yanatofautishwa katika namna na wakati
agano lilivyofanywa. Neno kale hapa halina maana ya kitu cha zamani
kilichopoteza thamani bali lina maana ya kitu kilichofanyika awali na
chenye thamani hata leo. Ukale wake upo katika wakati au kipindi, yaani
awali, kabla ya Yesu. Ukale huo pia upo katika namna au mtindo, yaani
Mungu alifanya agano kwa njia ya watu wanaoitwa manabii. Neno jipya
halina maana ya kitu kipya chenye thamani zaidi ya kile cha awali bali
upya wake upo katika wakati au kipindi na namna au mtindo. Katika Agano
Jipya Mungu hatumii tena manabii bali anafanya agano na watu wake wote
yeye mwenyewe kwa njia ya mwanae Yesu Kristo: Mungu ambaye alisema
zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi,
mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa
mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni
mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akavichukua vyote kwa
amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa
kuume wa ukuu huko juu; amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina
alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao. Waebrania 1:1-4 Agano la Kale na
Agano Jipya ni sehemu mbili za Biblia zenye thamani sawa kabisa na ni
sehemu mbili zinazotegemezana na kukamilishana kabisa. Haiwezekani
kulielewa Agano la kale bila Agano Jipya, pia haiwezekani kulielewa
Agano Jipya bila ya Agano la Kale. Maagano yote mawili yalianza rasmi
kwa maneno yanayofanana katika maudhui yake: Agano la Kale lilianza
rasmi kwa maneno ya wana wa Israeli walipomwambia Mungu kwa njia ya
Musa: “Hayo yote aliyoyasema Bwana tutayatenda.” Agano Jipya lilianza
rasmi kwa maneno ya Bikira Maria alipojiweka mikononi mwa Mungu kwa
niaba ya taifa jipya la Mungu, yaani Kanisa: “Tazama, mimi ni mtumishi
wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.”
Habari kwa hisani ya gazeti la kiongozi
No comments:
Post a Comment