Na Marcel Mukadi, SDS TUNASOMA katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki
Ufupisho-Makini kuwa, “Sakramenti ni alama wazi zinazoonekana na zenye
nguvu ya kuleta neema, ziliwekwa na Kristo na kukabidhiwa kwa Kanisa
ziwe njia za kutuletea uzima wa kimungu”. Ziko saba : Ubatizo,
Kipaimara, Ekaristi, Kitubio, Mpako wa Wagonjwa, Daraja Takatifu na Ndoa
(§224). MAANA YAKE NINI ? Ni kweli kuwa hakuna mahali katika Maandiko
Matakatifu, Yesu anatamka neno hili au kutoa ufafanuzi kuhusu neno hili.
Na wala hakuna mahali Yesu ametoa idadi ya sakramenti hizi. Narudia
yale niliyoyasema hapo awali kuwa si kwa sababu neno halipo katika
Biblia, basi Yesu hajalitumia ; au si kwa sababu Yesu hajatumia neno
fulani ; basi sisi hatuwezi kulitumia. Tujue kuwa hata kama neno halipo,
wazo lipo. Wazo kubwa ni maisha ya Yesu. Kwa sababu hiyo, tunakiri kuwa
“mafumbo ya maisha ya Kristo ndiyo msingi wa sakramenti”. Maisha ya
Yesu hadharani ni sakramenti tosha. Hivi kuanzishwa kwa sakramenti
kunaonekana katika kitendo cha Ubatizo (Yoh 3 : 22-23.26 ; 4 : 1),
uoshaji miguu (Yoh 13:3-12), kusamehe dhambi (Mk 2:5), kuponya wagonjwa
(Mk 1:29-31;32-39;40-45), kushirikisha karamu (Mk 2:13-17 ; 14:22-25),
kuleta msimamo kuhusu maisha (Mt 19:1-12) na kuanzishwa kwa Kanisa (Mt
16:17). Hata hivyo, ni bora kusisitiza kuwa tukio la Pasaka peke yake
ndilo lililowezesha kubadilisha matendo ya kiishara ya Yesu kuwa
sakramenti. Ufufuo wake unahakikisha kuwa maisha yake ni wokovu kweli.
Tunapoangalia maisha ya Yesu, ni maneno na matendo yake tunayoangalia na
miwani ya ufufuko wake kwani ufufuo huo umefanya upya kila kitu. Ndiyo
maana “Yale yaliyoonekana katika Mwokozi wetu yameingia katika
sakramenti zake,” yaani “maneno na matendo ya Yesu Kristo kipindi cha
maisha yake yaliyofichika na cha huduma yake ya hadhara yalikuwa tayari
ya wokovu, kwani yalitazamia mbele nguvu ya fumbo lake la Pasaka. Hayo
yalikuwa yanatangaza na kutayarisha kile ambacho angalikitoa kwa Kanisa
wakati yote yatakapokuwa yametia. Mafumbo ya maisha ya Kristo huunda
misingi ya kile ambacho sasa Kristo hukigawa katika sakramenti kwa njia
ya wahudumu wa Kanisa, kwani ‘kile kilichokuwa kinaonekana ndani ya
Mwokozi wetu kimepitishwa ndani ya mafumbo yake’ (KKK § 1115). Ufufuo wa
Yesu unatufunulia maisha yote ya Yesu kama chanzo cha Wokovu. Yesu ni
Emmanueli, yaani, Mungu pamoja nasi. Jina Yesu, linatokana na neno la
Kiebrania : “Yehoshua” yaani, Mungu ni Wokovu. Jina hili linadokezwa na
malaika anayeeleza kwamba mtoto huyu atawakomboa watu wake kutoka dhambi
zao (Mt 1:21-23). Wokovu unakuja kwa njia ya huyu Yesu. Ni yeye chanzo
kweli cha wokovu au ni yeye Wokovu wetu, na wokovu wake ni toba na
msamaha wa dhambi (Lk 1:77 : Mdo 5:31). Kwa mantiki hii, maneno na
matendo yote ndani ya maisha yake ni kwa ajili ya kuleta wokovu na si
vinginevyo. Na haya yote, yamejengwa juu ya msingi wa Maandiko haya ya
Yohane, “Neno la Mungu akatwaa mwili, akakaa kwetu” (Yoh 1:14). Maana
yake, Mungu amejifanya mtu ili mtu ashiriki Umungu wa muumba wake.
Yanaeleweka vizuri kwa lugha ya Kilatini, “Deus homo factus est ut homo
Deus fieret”. “Kama vile tulivyoichukua sura ya yule wa udongo,
tutaichukua vile vile sura ya yeye aliye wa mbinguni” (1Kor 15 :49). Kwa
kweli Mungu alijifanya Mtu, na huyu Yesu, aliyezaliwa na Bikira Maria
huko Betlehemu, na akateswa kwa mamlaka ya Ponsio Pilato, awe Mungu
aliyejifanya Mtu, haya mawazo mawili ndiyo kiini cha imani yetu. Kwa
kweli, ni huyu Kristo, Mtu kweli na Mungu kweli, anayetufunulia kuwa
Mungu ni nani na mtu ni nani. Kristo hufunua Mungu ni nani. Na ni huyu
huyu Kristo anayetufunulia tena mtu ni nani. Ni Kristo, pekee awezaye
kutuonesha kwa nafsi yake kile alicho nacho Mungu na kile alicho nacho
mtu. Mungu ni Upendo (1Yoh 4:8.16). “Anionae Mimi, humuona Baba” (Yoh
14:9). Ni yeye tena awezaye kutufunulia mtu ni nani. Jitihada ya
wanadamu katika maisha yao ni kuwa pamoja na Mungu, si bila Mungu. Kama
mwanadamu Yesu ni Mungu, basi nasi tunaweza kuwa ‘Mungu’. Kwa nini
Kristo ni Mtu kweli ? Kwa sababu hana dhambi ! Na sisi binadamu
kitukoseshacho kuwa binadamu kweli, ni kwa sababu tu wenye dhambi.
Kristu hutufanya kweli watu, na hapo hapo hutufanya ‘Mungu’ (Christ
humanizes us and at the same time Christ divinizes us). Kristo ni sura
ya Mungu kwa mtu na tena, Kristo ni sura ya mtu kwa Mungu. Basi
unapoangalia sura ya Kristo unamuona Mungu kweli, na hapo hapo unamuona
Mtu kweli. Ndiyo maana ya Yesu Kristo ni Mungu kweli na Mtu kweli.
Kutokana na haya yote, nathubuthu kusema “sakramenti” ni “Neno akatwaa
mwili, na akakaa kwetu”. Katika sakramenti, Mungu anakuja kwetu kwa
maneno na matendo ya huyu Yesu Kristo yanayotujaza na neema yake ili
tupate kujitakatifuza na kuwa kama Mungu pamoja na Kristo. Katika
sakramenti, tunakumbushwa kuwa sisi ni “miungu” kama tunavyosikia kutoka
kinywani mwa Mungu mwenyewe: Mimi nimesema: “Ninyi ni miungu, ninyi
wote ni wana wa yule Aliye-juu” (Ps 82:6). Na Yesu anatumia aya hii
kuthibitisha kuwa wale ambao Neno la Mungu linaelekezwa kwao, wanaweza
kuitwa “miungu” (Yoh 10:34). Ninakubaliana na Mtakatifu Ireneus, baada
ya kusema “utukufu wa Mungu, unaonekana ndani ya mtu aliye hai”,
ameongeza na kusema; “Kwa hiyo, maisha ya mtu aliye hai ni kumsifu au
kumsujudu Mungu”. Kwa mujibu wa mafundisho ya Mtakatifu Ireneus, huyu
Mtu kamili ni Yesu. Lengo la kila sakramenti ni kutufanya viumbe vipya
ndani ya Mungu kwa njia ya Yesu Kristo; ni kutufanya “miungu”, wana wa
yule Aliye-juu, ndiye Mungu. Toka hapo tunaelewa kuwa ndani ya kila
sakramenti, kuna uhusiano wa uwepo wa Mungu na ukubwa wa binadamu.
Yaani, Mungu anakuja kwa mwanadamu kwa njia ya Yesu Kristo, kumuinua
huyu mwanadamu katika hali ya Mtu kweli kwa njia ya huyu huyu Kristo.
Mungu ni Fumbo. Watu wengi wanafikiri kuwa “fumbo” ni kitu
kisichoeleweka; bali sivyo. Fumbo ni kitu ambacho hatuachi kamwe
kukitafakari. “Hakuna amjuaye Mwana, ila Baba. Wala hakuna amjuaye Baba,
ila Mwana na yeyote ambaye Mwana apenda kumfunulia”(Mt 11:27). Ndiyo
maana, tunamtazama Kristo aliye Sakramenti ya Baba. Kwa kuwa Mungu
hakuna anayemjua; ila Yesu, aliye ufunuo wa Baba au aliye Sakramenti ya
Baba, anatufanya nasi tuwe sakramenti yake kama Kanisa ni sakramenti
yake kweli. Ndiyo Mafundisho ya Mtaguso wa Pili wa Vatikani kuwa “Katika
Kristo Kanisa ni kama sakramenti au ishara na chombo cha kuwaunganisha
watu kiundani na Mungu na kuleta umoja kati ya wanadamu wote”. Yesu ni
Sakramenti ya Baba kwa mantiki hii, “anayemuona Yesu anamuona Baba kwani
Baba yu ndani yake, naye yu ndani ya Baba” (Yoh 14:9.38). Yaani Yesu ni
Sura ya Mungu asiyeoonekana (Kol 1:15). Mwanadamu huwa Sakramenti ya
Yesu wakati asikiapo sauti yake na kumfuata (Yoh 10:27), kwani Yesu
husema, “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi yangu. Adumuye ndani yangu,
nami ndani yake, huyo huzaa matunda mengi, kwa maana pasipo mimi
hamuwezi kufanya lolote” (Yoh 15:5). Kanisa ni Sakramenti ya Yesu kwani
“Mtu hawezi kuwa na Mungu kama Baba, asipokuwa na Kanisa kama Mama”,
anasema Mtakatifu Sipriano. Hii inatukumbusha jinsi Yesu alivyobadilisha
maisha ya Sauli alipokuwa njiani kwenda kulitesa Kanisa la Mungu, kwa
kujifananisha na Kanisa, “Sauli, Sauli, mbona unanitesa ?” (Mdo 9 :
1-43). Mwandishi ni Padri na Paroko Msaidizi wa Parokia ya St. Maurus
Kurasini, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
Habari kwa hisani ya gazeti la kiongozi
No comments:
Post a Comment