Wednesday, March 18, 2015

Ni mjumbe wa matumaini!

Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei, Jumamosi, tarehe 21 Machi 2015, tukio ambalo linatarajiwa kuwajaza furaha na matumaini waamini na watu wenye mapenzi mema huko Pompei, mlango wa sala na makutano kati ya Familia ya Mungu na Baba Mtakatifu Francisko wakati akiwa njiani kuelekea Jimbo kuu la Napoli.
Ni hija ya muda mfupi, lakini Baba Mtakatifu anapenda kuitumia kama hujaji anayekwenda kujikabidhi kwa Bikira Maria, kielelezo makini cha hija ambazo zimefanywa na waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu ameonesha nia ya kwenda kusali kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu wa Pompei, kielelezo cha Ibada kwa Bikira Maria, hali ambayo ameionesha tangu siku ile ya kwanza alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Baba Mtakatifu Francisko kwa mara kadhaa amewataka waamini kujenga na kukuza Ibada ya Rozari Takatifu, kwani huu ni muhtasari wa Injili na kwamba, kwake, Rozari imekuwa ni mwenzi wa hija ya maisha ya kiroho. Hii ni sala ya waamini wa kawaida, sala ambayo imekuwa ni chemchemi ya utakatifu kwa Watakatifu wengi ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, hii ni sala inayobubujika kutoka katika moyo wake!
Hii ni sehemu ya barua ya kichungaji iliyoandikwa na Askofu mkuu Tommaso Caputo, Mwakilishi wa Papa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu wa Pompei, wakati huu wanapojiandaa kwa ajili ya ujio wa Baba Mtakatifu Madhabahuni hapo. Baba Mtakatifu anapenda kujionea mwenyewe jinsi ambavyo Ibada kwa Bikira Maria inamwilishwa katika matendo ya huruma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, changamoto kwa waamini kuendelea kujikita katika ushuhuda wa imani tendaji.
Askofu mkuu Tommaso Caputo anasema, kwamba, waamini na watu wenye mapenzi mema, wangependa kumwona, kumsalimia, kusali na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwa karibu, jambo ambalo pengine si rahisi, lakini waamini watapaswa kuridhika na uwepo wa Baba Mtakatifu miongoni mwao. Hii inatokana na ukweli kwamba, Baba Mtakatifu ameamua kuingiza katika ratiba yake kuelekea Jimbo kuu la Napoli, ili kupita na kusali na waamini kwenye Madhabahu ya Pompei. Waamini wanaalikwa kuendelea kumsindikiza Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kwa sala na sadaka yao!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 

Habari kwa hisani ya radio vatican




















No comments:

Post a Comment