Wednesday, April 30, 2014

Maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 yaanza kushika kasi! Krakovia utakuwa ni moto wa kuotea mbali!



Wakurugenzi wakuu wa utume wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia katika mkutano wao wanasema kwamba, kuna haja ya kuwa na tafiti endelevu zitakazoliwezesha Kanisa kuwa na njia mpya za kuweza kukutana na kuzungumza na vijana, sanjari na kuwa na lugha pamoja na mbinu mpya za mawasiliano, ili kuwafikia vijana ambao wengi wao wanaogelea kwenye mitandao ya kijamii.

Siku ya kwanza ya mkutano huu, wajumbe wamepembua kwa kina na mapana matunda yaliyopatikana kutokana na maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Rio di Janeiro, Brazil, pamoja na kuangalia shughuli za kuratibu na huduma kwa mamillioni ya vijana waliokuwa wamekusanyika mjini Rio de Janeiro.

Kardinali Oran Joao Tempesta, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Rio de Janeiro anasema, katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Brazil, wameshuhudia mkono wa Mungu ukitenda maajabu na matunda yake yameonekana. Matukio makubwa ya imani yanapaswa kumwilishwa kila siku katika uhalisia wa maisha ya vijana wenyewe.

Katika maadhimisho ya Juma la Kimissionari nchini Brazil, vijana walitembeza Msalaba na Sanamu ya Bikira Maria, muda mfupi kabla ya kuanza maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Hili ni tukio ambalo liliwashirikisha waamini na watu wenye mapenzi mema nchini Brazil na hivyo kuacha chapa ya kudumu katika mipango na mikakati ya shughuli za kichungaji miongoni mwa vijana. Kanisa Katoliki nchini Brazil, limepata uzoefu na mang'amuzi makubwa katika utekelezaji wa utume wake miongoni mwa vijana.

Wajumbe kimsingi wanasema, kila mahali ambapo vijana wameshiriki kikamilifu katika maandalizi, maadhimisho na tathmini yake, kumekuwepo na ukuaji mkubwa wa miito mitakatifu ndani ya Kanisa na kwamba, vijana wengi wanaendelea kujiimarisha katika hija ya imani na mapendo.

Kwa upande wake, Kardinali Stansislaw Rylko, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya walei anasema, ukitaka kumfahamu kwa undani Mwenyeheri Yohane Paulo II tembelea Jimbo kuu la Krakovia, Poland. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yalianzishwa kunako Mwaka 1984 kwa mwaliko kutoka kwa Baba Mtakatifu Yohane Paulo II na tangu wakati huo, utume wa Mama Kanisa miongoni mwa vijana ukaanza kuzamisha mizizi yake.

Kinzani na madhulumu ya kisiasa yalisababisha vijana wengi kukosa dira na mwelekeo wa maisha ya kiroho. Mwenyeheri Yohane Paulo II akaliona hilo na kuanza kukuza sera makini katika kuwahudumia vijana ndani na nje ya Kanisa. Vijana wakampenda na kumthamini kama Baba, Rafiki na Mwalimu kiasi hata cha kuthubutu kumsindikiza katika safari yake ya mwisho hapa duniani: Waliposikia kwamba amefariki dunia, wakapiga kelele, "Santo Subito", yaani atangazwe mara moja kuwa Mtakatifu.

Kardinali Stanislaw Dziwisz, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Krakovia, Poland, mwemyeji wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 anasema, maadhimisho haya yamekuwa kweli ni tukio la kiimani ambao limekoleza ari, moyo na mwamko wa kimissionari, chemchemi ya miito na utakatifu wa maisha. Maadhimisho haya yamekuwa ni changamoto endelevu kwa Mama Kanisa kuibua mbinu na mikakati ya utume miongoni mwa vijana.

Baraza la Maaskofu Katoliki Poland linasema, maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Poland yanapania kuwa ni uwanja wa huruma "Campus Misericordiae" kwa mahujaji vijana watakaobahatika na kuthubutu kutembelea Poland kunako mwaka 2016. Wajumbe wa mkutano huu unaohitimishwa Jumapili ya Matawi, umekuwa ni fursa ya kubadilishana, uzoefu, mang'amuzi na changamoto katika maisha na utume wa Mama Kanisa miongoni mwa vijana.

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment