Wednesday, April 30, 2014

Watakatifu wapya, miamba ya huruma ya Mungu kukumbukwa kila mwaka ifikapo Mwezi Oktoba



Baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu, Jumapili tarehe 27 Aprili 2014 katika Ibada iliyohudhuriwa na maelfu ya watu waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican pamoja na viunga vyake, watakatifu hawa wapya watakumbukwa kila mwaka mwezi Oktoba kadiri ya Kalenda ya Liturujia ya Kanisa.

Kadiri ya Kalenda ya Liturujia ya Kanisa kwa ajili ya kumbu kumbu ya Watakatifu, Yohane XXIII atakumbukwa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Oktoba. Hii ni siku maalum ambayo, kwa takribani miaka hamsini iliyopita, Yohane XXIII alikuwa anafungua rasmi maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, tukio ambalo limeleta mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Hili ni tukio la kishujaa lililomstahilisha Papa Yohane XXIII kuitwa Mtakatifu.

Mtakatifu Yohane Paulo II atakumbukwa kila mwaka ifikapo tarehe 22 Oktoba. Hii ni siku ambayo Papa Yohane Paulo II alipoanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, akaendeleza maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na kukazia umuhimu wa Mama Kanisa kujikita katika mchakato wa Umissionari na Uinjilishaji Mpya. Mwezi Oktoba ni mwezi wa shughuli na mikakati ya kimissionari ndani ya Kanisa.

Tangu sasa waamini na watu wenye mapenzi mema wanaweza kuwaenzi watakatifu hawa wapya kwa maadhimisho ya: Ibada, Liturujia pamoja na kuwaweka kuwa walinzi na wasimamizi wa shughuli mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II atakuwa ni msimamizi wa Siku za Vijana Duniani. 

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment