Saturday, May 3, 2014

Je wajua kuwa Kupalizwa kwa Bikira Maria mbinguni mwili na roho ni chemchem ya furaha kwa kanisa zima

Ilikuwa ni tarehe Mosi, Novemba, 1950, Baba Mtakatifu Pio wa Kumi na mbili, alipotangaza kwamba, Bikira Maria baada ya kuhitimisha hija ya maisha yake hapa duniani, alipalizwa mbinguni mwili na roho.

Huu ni ukweli wa kiimani ambao umejionesha katika Mapokeo na kuungwa mkono na Mababa wa Kanisa, kama njia ya kutoa heshima ya juu kabisa kwa Bikira Maria Mama wa Mungu. Mafundisho Tanzu ya Kanisa kuhusu Bikira Maria kupalizwa mbinguni ni utenzi wa sifa kwa ajili ya Bikira Maria aliyetukuzwa na Mwanaye Mpendwa Yesu, chemchemi ya furaha kwa Kanisa zima. Watu wa Mungu kadiri ya Mapokeo tayari walikwisha adhimisha tukio hili la sifa, kumbe kutangaza fundisho hili tanzu, ilikuwa ni njia ya kuimarisha imani ya waamini na tendo la imani ya kiliturjia.

Ndiyo maana Bikira Maria katika utenzi anasema, tangu sasa vizazi vyote wataniita mwenyeheri. Huu ni utenzi wa sifa na utukufu kwa Mama wa Mungu, aliyeungana kwa dhati na Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo, kwa ajili ya watu wa nyakati na tamaduni zote. Kanisa halina budi kutambua ukuu wa mwanamke kwa njia ya imani, inayowawezesha Waamini kuuona ukuu wa Bikira Maria na hatimaye, kupata fursa ya kumfahamu Mwenyezi Mungu.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni: mwili na roho, Jumatano, tarehe 15 Agosti 2012. Magnificat, anasema Baba Mtakatifu ni utenzi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu anayeendelea kutenda katika hija ya maisha na historia ya mwanadamu; ni utenzi wa imani na mapendo yanayobubujika kutoka katika Moyo Safi wa Bikira Maria.

Amebahatika kuwa mwaminifu pamoja na kumwilisha ujumbe na ahadi za Neno la Mungu walizopewa Mababa wa imani na katika maudhui ya utenzi huu, anayafanya kuwa ni sehemu yake ya Sala; mwanga katika mapito yake; tayari kumpokea Neno wa Mungu ambaye angefanyika mwili tumboni mwake. Hiki ni kielelezo endelevu cha uwepo wa Mungu katika historia na matukio mbali mbali ya maisha ya mwandamu.

Bikira Maria ni Sanduku la Agano, linalobeba ndani mwake, uwepo wa Mungu, chemchemi ya faraja na wingi wa furaha, kwani Mwenyezi Mungu ndiye asili ya furaha ya kweli katika maisha ya mwanadamu, kama ilivyojionesha katika Familia ya Mzee Zakaria, kutokana na uwepo wa Bikira Maria aliyekuwa amembeba Mwana wa Mungu, tumboni mwake.

Siku kuu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni anasema Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ni kielelezo kwamba, Mwenyezi Mungu anatoa nafasi kwa binadamu na nyumbani mwake kuna makao mengi, kama anavyobainisha Yesu mwenyewe katika sehemu nyingine za Injili. Mwenyezi Mungu ni makao ya binadamu, changamoto kwa mwanadamu kujitahidi kuwa karibu na Mwenyezi Mungu, kama alivyofanya Bikira Maria.

Ni Mama ambaye yuko karibu na binadamu, ana uwezo mkubwa wa kusikiliza na kusaidia, kwani yuko karibu sana na Mwenyezi Mungu. Ikumbukwe kwamba, hata katika moyo wa mwanadamu kuna nafasi ya Mungu, kama inavyojionesha kwa Bikira Maria Sanduku la Agano, linaloonesha uwepo wa Mungu, unaopania faraja mwanadamu kutokana na mahangaiko yake ya ndani na utimilifu wake unajionesha kwa namna ya pekee katika imani. Kwa njia hii, mwanadamu anapata fursa ya kumfungulia Mungu hazina ya maisha yake, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu, kama alivyofanya Bikira Maria kwa kusema, "Mimi ni mtumishi wa Bwana"

Baba Mtakatifu anasema, hapa: imani, matumaini na mapendo yanakumbatiana, ili kuleta mwelekeo bora zaidi katika ulimwengu mamboleo, kwani haya ndiyo matumaini ya binadamu, lakini kwa bahati mbaya, mwanadamu anaendelea kuwa mbali na uwepo wa Mwenyezi Mungu, kiasi kwamba, ulimwengu unaelekea pabaya zaidi. Mwenyezi Mungu bado anamsubiri mwanadamu, ili kumkirimia maisha mapya, furaha na matumaini yasiyodanganya kamwe!

Kwa mfano wa Bikira Maria, anasema Baba Mtakatifu, mwamini anaona ushindi dhidi ya kifo. Bikira Maria ni mwanga angavu wa ushindi wa Kanisa; mfariji na tumaini la Kanisa ambalo bado liko safarini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujiachilia mikononi mwa Bikira Maria ili aweze kuwaombea kwa Mwanaye mpendwa ili kuwaimarisha katika imani kwa maisha ya uzima wa milele; wakiendelea kuishi vyema kwa imani na matumaini ya kukutana na Mwenyezi Mungu, anayewaimarisha waamini katika ujasiri, nguvu ya kiimani na mapendo.




Habari kwa hisani kwa radio vatican

No comments:

Post a Comment