BARUA YA KITUME
“ROZARI
YA BIKIRA MARIA”
YA
BABA MTAKATIFU YOHANE PAULO II
KWA
MAASKOFU, MAKLERI NA WAAMINI WOTE
KUHUSU
ROZARI TAKATIFU
UTANGULIZI
1. Rozari ya Bikira Maria, iliyostawi hatua kwa hatua katika
milenia ya pili kwa uvuvio wa Roho wa Mungu,
ni sala iliyopendwa na watakatifu wengi na kuhimizwa na Ualimu wa Kanisa.
Katika usahili na udhati wake inazidi kuwa sala muhimu sana, na kutarajiwa kuzaa
matunda ya utakatifu katika milenia hii ya tatu iliyoanza tu. Yenyewe inafaa
kuchangia safari ya Kiroho ya Ukristo ambao, baada ya miaka elfu mbili,
haujapotewa na uhai wa asili yake na unajisikia kusukumwa na Roho wa Mungu
kwenda kilindini ili kumtangaza tena kwa sauti kubwa Kristo kwa ulimwengu kuwa
ndiye Bwana na Mwokozi, "njia, ukweli na uzima" (Yoh 14:6), "lengo
la historia yote, kiini cha vipeo vya historia na cha ustaarabu wa binadamu".
Kwa kuwa Rozari, ingawa ina sura ya Kimaria, ni sala ambayo moyo wake ni Kristo.
Katika usahili wa sehemu zinazoiunda, inajumlisha ndani mwake udhati wa ujumbe
wote wa Injili, ambao Rozari ni kama muhtasari wake. Ndani mwake mna mwangwi wa
sala ya Maria, Magnificat, wimbo wake
usiopitwa na wakati kwa ajili ya umwilisho wenye kulenga ukombozi wa watu
ulioanza katika tumbo lake la kibikira. Kwa njia yake taifa la Wakristo linataka
kujifunza kwa Maria, ili liingizwe hata kuzama ndani ya uzuri wa uso wa Kristo
na kung'amua ukuu wa upendo wake. Kwa njia ya Rozari mwamini anachota wingi wa
neema, kama kwa kuupokea mikononi mwa Mama wa Mkombozi.
Maaskofu wa Roma na Rozari
2.
Sala hiyo ilitiwa maanani sana na watangulizi wangu wengi. Kuhusu jambo hilo
anastahili kukumbukwa kwa namna ya pekee Leo XIII ambaye tarehe 1 Septemba 1883
alitoa barua rasmi Supremi Apostolatus
Officio, tamko kuu ambalo lilifungua njia ya mengine mengi kuhusu sala hiyo
aliyoielekeza kama chombo cha Kiroho cha kufaa dhidi ya maovu mengi ya jamii.
Kati ya Baba Watakatifu wa mwishomwisho ambao wakati wa Mtaguso walijitokeza
kuhamasisha Rozari napenda kuwataja mwenye heri Yohane XXIII na hasa Paulo VI
ambaye katika himizo la kitume Marialis
Cultus, akifuata mwelekeo wa Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikano, alisisitiza
jinsi Rozari ilivyo na tabia ya Kiinjili na inavyomlenga Kristo. Halafu mimi
mwenyewe sijaacha nafasi ya kuhimiza kusali Rozari mara nyingi. Tangu ujana
wangu sala hiyo imeshika nafasi muhimu katika maisha yangu ya Kiroho. Safari
yangu ya mwisho huko Polandi, na hasa ziara yangu katika patakatifu pa Kalwaria,
imenikumbusha kwa nguvu jambo hilo. Rozari imenisindikiza katika furaha na
katika majaribu. Kwake nilikabidhi mahangaiko mengi, kwake nikapata daima faraja.
Miaka ishirini na minne iliyopita, tarehe 29 Oktoba 1978, wiki mbili tu baada ya
kuchaguliwa nikalie ukulu wa Petro, kama kwa kuifungua roho yangu nilisema hivi:
“Rozari ndiyo sala yangu pendevu kuliko zote. Sala nzuri ajabu! Ya ajabu
katika usahili wake na udhati wake… Tunaweza kusema kwa namna fulani Rozari ni
sala inayofafanua sura ya mwisho ya hati Lumen Gentium ya Mtaguso wa pili wa Vatikano, sura inayohusu uwepo
wa ajabu wa Mama wa Mungu katika fumbo la Kristo na la Kanisa. Kwa maana juu ya
maneno ya Salamu Maria yanapita mbele ya macho ya roho matukio makuu ya maisha
ya Yesu Kristo. Yenyewe yameunda umoja wa mafumbo ya furaha, uchungu na utukufu,
na kutuunganisha kwa namna hai na Kristo kupitia - tuseme - moyo wa Mama yake.
Wakati huohuo moyo wetu unaweza kujumlisha katika makumi hayo ya Rozari matukio
yote yanayounda maisha ya mtu binafsi, familia, taifa, Kanisa na binadamu kwa
jumla.
Matukio ya binafsi na ya jirani na hasa ya wale ambao tunahusiana nao zaidi na
kuwapenda zaidi. Hivyo sala sahili ya Rozari inalingana na madundo ya maisha ya
binadamu". Kwa maneno hayo, wapendwa ndugu zangu, niliingiza katika mwendo
wa kila siku wa Rozari mwaka wangu wa kwanza kama askofu wa Roma. Leo, mwanzoni
mwa mwaka wa ishirini na tano wa huduma hiyo kama mwandamizi wa Petro, nataka
kufanya vilevile. Jinsi zilivyo nyingi neema nilizozipokea miaka hiyo kwa Bikira
Maria kupitia Rozari: Magnificat anima mea
Dominum! Nataka kumuinulia Bwana shukrani zangu kwa maneno ya Mama yake
mtakatifu, ambaye chini ya ulinzi wake nimeweka huduma yangu ya Kipapa: Totus
tuus!
Oktoba 2002 - Oktoba 2003: mwaka wa Rozari
3.
Kwa hiyo, kufuatana na tafakuri niliyoitoa katika barua ya kitume Novo
Millennio Ineunte, ambamo nilialika taifa la Mungu "tuanze upya na
Kristo" baada ya mang'amuzi ya jubilei kuu, nimejisikia haja ya kuandika
tafakuri juu ya Rozari kama taji la Kimaria la barua hiyo, ili nihimize
tuutazame uso wa Kristo tukiwa na Mama yake mtakatifu na tukijifunza kwake. Kwa
sababu kusali Rozari ni hicho tu: kuutazama uso wa Kristo pamoja na Maria. Ili
nitie maanani mwaliko huo, nikichukua fursa ya kutimia hivi karibuni kwa miaka
120 tangu Leo XIII atoe hati hiyo, nataka sala hiyo ipendekezwe na kutumiwa kwa
namna ya pekee kwa muda wa mwaka mzima katika jumuia mbalimbali za Kikristo. Kwa
hiyo nautangaza mwaka unaoanza Oktoba ya mwaka huu hadi Oktoba ya mwaka 2003 uwe
mwaka wa Rozari. Nakabidhi elekezo hilo la kichungaji kwa bidii ya kila jumuia
ya Kanisa. Kwa kufanya hivi sitaki kuvuruga, bali kukamilisha na kuimarisha
mipango ya kichungaji ya Makanisa maalumu. Natumaini litapokewa kwa juhudi na
utayari. Rozari ikivumbuliwa tena katika maana yake yote inafikisha hadi kiini
chenyewe cha maisha ya Kikristo na kutoa nafasi ya kawaida yenye kuzaa matunda
ya Kiroho na ya kimalezi kwa sala hasa, kwa malezi ya taifa la Mungu na kwa
uinjilishaji mpya. Napenda kusisitiza hilo nikikumbuka kwa furaha tarehe
nyingine, yaani kutimia miaka arubaini tangu uanze Mtaguso Mkuu wa pili wa
Vatikano (11 Oktoba 1962), ambao ndio "neema kuu" iliyoandaliwa na
Roho wa Mungu kwa Kanisa la nyakati zetu.
Hoja dhidi ya Rozari
4.
Kwamba mwaka wa Rozari unafaa inatokana na kuzingatia mambo mbalimbali. La
kwanza linahusu haja ya haraka ya kupambana na tatizo la sala hiyo kupuuziwa
pasipo sababu katika hali ya sasa ya historia na ya teolojia na hivyo
kutopendekezwa vya kutosha kwa vizazi vipya. Baadhi wanadhani kwamba nafasi ya
kwanza inayoistahili liturujia, kama ilivyosisitizwa na Mtaguso Mkuu wa pili wa
Vatikano, inadai kupunguza umuhimu wa Rozari. Kumbe, alivyoeleza Paulo VI, sala
hiyo haipingani na liturujia, bali inaitegemeza, kwa kuwa inaiandaa na kuiitikia
vema, ikiwezesha kuishiriki kabisa kwa dhati na kuyachuma matunda yake katika
maisha ya kila siku.
Labda
kuna wengine pia ambao wanaogopa kwamba sala hiyo haisaidii ekumeni, kutokana na
tabia yake ya Kimaria hasa. Kumbe Rozari inajipanga katika mandhari safi zaidi
ya ibada kwa Mama wa Mungu kadiri Mtaguso ulivyoichora: yaani ibada inayomlenga
Kristo, kiini cha imani yetu, hivi kwamba "Mama anapoheshimiwa, Mwana
ajulikane na kupendwa na kutukuzwa ipasavyo". Rozari, ikieleweka upya
inavyofaa, ni msaada, sio kizuio kwa umoja wa Wakristo!
Njia ya sala hasa
5.
Lakini sababu muhimu zaidi inayonifanya nipendekeze tena kwa nguvu matumizi ya
Rozari ni kwamba yenyewe ni njia ya kufaa sana kwa kuwahamasisha waamini kuhusu
ile juhudi ya kuzama katika fumbo la Kristo niliyoipendekeza katika barua ya
kitume Novo Millennio Ineunte kama
njia halisi ya 'malezi ya utakatifu' : "Tunahitaji aina ya Ukristo ambayo
inajitokeza kwanza katika utaalamu wa kusali".
Wakati ambapo katika utamaduni wa kisasa, ingawa kati ya matata mengi,
inaelea haja mpya ya maisha ya Kiroho, inayochochewa hata na athari za dini
nyingine, kuna haja ya haraka kuliko siku za nyuma ya kuwa jumuia zetu za
Kikristo zigeuke "shule halisi za sala".
Rozari
inajipanga katika mapokeo bora na yenye mang'amuzi mengi zaidi ya sala hasa ya
Kikristo. Ikiwa imestawi huku Magharibi, ni sala yenye tabia ya
kutafakari hasa na inalingana kwa namna fulani na "sala ya moyo" au
"sala ya Yesu" iliyochipuka kwenye rutuba ya Mashariki ya Kikristo.
Sala kwa ajili ya amani na ya familia
6. Nafasi nyingine za historia ya leo
zinaongeza sababu za kueneza upya Rozari siku hizi. Ya kwanza ni haja ya haraka
ya kumsihi Mungu atujalie amani. Mara nyingi watangulizi wangu na mimi mwenyewe
tuliipendekeza Rozari kama sala kwa ajili ya amani. Mwanzoni mwa milenia mpya,
ambayo ilianza na matukio ya kutisha ya mauaji ya tarehe 11 Septemba 2001 na
ambayo inarekodi kila siku katika sehemu mbalimbali za dunia nafasi mpya za
umwagaji damu na ukatili, kuvumbua upya Rozari ni kuzama katika fumbo la yule
ambaye "ndiye amani yetu" kwa kuwa ametufanya "sisi sote
tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga" (Ef
2:14). Kwa hiyo haiwezekani kusali
Rozari bila ya kujisikia tunahusika na jukumu maalumu la kuhudumia amani, kwa
namna ya pekee kwa ajili ya nchi ya Yesu, ambayo inazidi kupatwa na majaribu
makali na inapendwa sana na moyo wa Wakristo.
Haraka
hiyohiyo ya kuwajibika na kusali inajitokeza upande mwingine wenye utata wa
wakati wetu, ule wa familia, seli ya jamii, inayozidi kushambuliwa na miundo
inayobomoa kinadharia na kimaisha, hata kutia wasiwasi kuhusu kesho ya muundo
huo wa msingi usiokanushika na kuhusu kesho ya jamii nzima pamoja nao. Kueneza
upya Rozari katika familia za Kikristo, kama sehemu ya mpango mpana zaidi wa
uchungaji wa familia, ni msaada wa kufaa ili kuzuia matokeo ya kuangamiza ya
matata ya nyakati zetu.
«Tazama,
mama yako! » (Yoh 19:27)
7.
Dalili mbalimbali zinaonyesha jinsi Bikira mtakatifu anavyotaka kutekeleza leo
pia, hasa kwa njia ya sala hiyo, juhudi za kimama ambazo Mkombozi alipokuwa
mahututi alizikabidhi wana wote wa Kanisa katika nafsi ya mwanafunzi mpendwa:
"Mama tazama mwanao" (Yoh 19:26). Zinajulikana nafasi
mbalimbali ambazo Mama wa Kristo, katika karne ya XIX na XX alijitokeza na
kusema ili kuhimiza taifa la Mungu kutumia aina hiyo ya sala ya kuzama katika
mafumbo.
Kwa
namna ya pekee napenda kukumbusha maono ya Lurdi na Fatima, kutokana na jinsi
yalivyoathiri mpaka leo maisha ya Wakristo na kuthibitishwa rasmi na Kanisa;
patakatifu hapo pawili ni shabaha za wahiji wengi wanaojitafutia faraja na
tumaini.
Kwenye nyayo za mashahidi
8.
Haiwezekani kutaja umati usiohesabika wa watakatifu walioiona katika Rozari njia
halisi ya utakatifu. Inatosha kukumbuka mtakatifu Alois Maria Grignion de
Montfort, mwandishi wa kitabu azizi kuhusu Rozari, na karibu nasi zaidi, padri
Pio wa Pietrelcina, ambaye hivi karibuni nimefurahi kumtangaza kuwa ni mtakatifu.
Halafu
karama maalumu ya kuwa mtume halisi wa Rozari alikuwa nayo mwenye heri Bartolo
Longo. Safari yake ndefu ya utakatifu ilitegemea mnong'ono aliousikia kilindini
mwa moyo wake: "Anayeeneza Rozari ataokoka!" Juu ya msingi huo
alijisikia kuitwa ajenge huko Pompei kanisa kwa heshima ya Bikira wa Rozari
takatifu katika mandhari ya mji wa zamani ambao ulifikiwa tu na ujumbe wa
Kikristo kabla haujateketezwa na mlipuko wa volkeno Vesuvio mwaka 79,
na ambao karne nyingi baadaye ulielea tena kutoka majivu yake kama
ushuhuda wa mianga na vivuli vya ustaarabu wa zamani.
Kwa
kazi yake yote, na hasa kwa "Sabato Kumi na Tano", Bartolo Longo
alistawisha kiini cha Kikristo na cha kuzama katika mafumbo cha Rozari, akitiwa
moyo na kutegemezwa kwa namna ya pekee na Leo XIII, « Papa wa Rozari ».
SURA YA KWANZA
KUMKAZIA
MACHO KRISTO PAMOJA NA MARIA
Uso mwangavu kama jua
9.
"Aligeuka sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua" (Math
17:2). Ukurasa wa Injili wa Kristo kugeuka sura, ambapo mitume watatu Petro,
Yakobo na Yohane wanaonekana kama wamechanganyikiwa na uzuri wa Mkombozi,
unaweza kuchukuliwa kama picha ya sala hasa ya Kikristo. Kuukazia macho uso wa
Kristo, kutambua fumbo lake katika safari ya kawaida na ya uchungu ya ubinadamu
wake, hadi kuhisi uangavu wa Kimungu uliodhihirika moja kwa moja katika Mfufuka
aliyetukuzwa kuumeni kwa Baba, ndiyo kazi ya kila mfuasi wa Kristo; kwa hiyo ni
kazi yetu pia. Tukiukazia macho uso huo tunajiweka tayari tuupokee fumbo la
uzima wa Utatu mtakatifu, ili kung'amua kwa namna mpya daima upendo wa Baba na
kujaa furaha ya Roho Mtakatifu. Hapo linatimia kwetu pia neno la mtume Paulo:
"Tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa
tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu
utokao kwa Bwana, aliye Roho" (2Kor 3:18).
Maria kielelezo cha sala hasa
10.
Maria ni kielelezo bora cha kumkazia macho Kristo. Sura ya Mwana ni ya kwake kwa
namna ya pekee. Alitungwa tumboni mwake, akichukua toka kwake sura ya kufanana
naye kibinadamu ambayo inadokeza ujirani wa Kiroho ambao kwa hakika ni mkubwa
zaidi. Hakuna aliyejitolea kuukazia macho uso wa Kristo kuliko alivyofanya Maria.
Kwa namna fulani macho ya moyo wake yalianza kumuelekea tangu apashwe habari,
alipomchukua mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu; miezi iliyofuata alianza kuhisi
uwemo wake tumboni na kutabiri sura yake. Hatimaye alipomzaa Bethlehemu macho ya
mwili wake pia yaliuelekea kwa hisani uso wa Mwana, huku akimvika nguo za kitoto
na kumlaza horini (taz. Lk 2:7).
Tangu
hapo mtazamo wake, uliojaa daima mshangao wa kiibada, haukubandukana naye tena.
Pengine ukawa mtazamo wa kuuliza swali, kama vile katika tukio la Yesu kupotea
hekaluni: «Mwanangu, mbona umetutenda hivi?» (Lk 2:48); kwa vyovyote ukawa
mtazamo wa kupenya, unaoweza kusoma moyoni mwa Yesu, hata kuhisi miguso
iliyofichika na kutabiri machaguo yake, kama alivyofanya Kana (taz. Yoh 2:5);
mara nyingine ukawa mtazamo wenye uchungu, hasa chini ya msalaba ambapo ukawa
tena, kwa namna fulani, mtazamo wa 'mwanamke anayejifungua', kwa kuwa Maria
hakushiriki tu mateso na kifo cha Mwana pekee, bali alimpokea mtoto mpya
aliyekabidhiwa katika mwanafunzi mpendwa (taz. Yoh 19:26-27); asubuhi ya Pasaka
ukawa mtazamo mwangavu kwa furaha ya ufufuko na hatimaye ukawa mtazamo motomoto
kwa ajili ya Roho kumiminwa siku ya Pentekoste (taz. Mdo 1:14).
Kumbukumbu za Maria
11.
Maria aliishi macho kwa Kristo na kutia maanani kila neno lake: «Aliyaweka
maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake» (Lk 2:19; taz. 2:51). Kumbukumbu za
Yesu, zilizochapika rohoni mwake, zilimfuata katika nafasi yoyote, zikimfanya
arudie kimawazo matukio mbalimbali ya maisha yake karibu na Mwana. Kumbukumbu
hizo ndizo zilizounda, kwa namna fulani, 'rozari' ambayo mwenyewe alisali
mfululizo siku zote za maisha yake duniani.
Pia
sasa, kati ya nyimbo za furaha za Yerusalemu wa mbinguni, sababu zake za
kushukuru na kusifu zinabaki zilezile. Ndizo zinazomuelekeza kulishughulikia
kimama Kanisa linalohiji, ambapo mwenyewe anaendelea kutekeleza tangazo lake
kama mwenezainjili. Maria anawapendekezea mfululizo waamini 'mafumbo' ya Mwanae,
akitamani yatazamwe yaweze kueneza uwezo wote wa kuokoa uliyo nayo. Jumuia ya
Kikristo inaposali Rozari inajilinganisha na kumbukumbu na mtazamo wa Maria.
Rozari, sala ya kuzamia mafumbo ya imani
12.
Rozari, kuanzia mang'amuzi yenyewe ya Maria, ni sala hasa ya kuzamia mafumbo ya
imani. Ingekosa sura hiyo isingekuwa yenyewe tena, kama alivyosisitiza Paulo VI:
«Pasipo kuzama katika mafumbo, Rozari ni kama mwili usio na roho, na inaingia
hatari ya kukariri maneno kimashine tu na hivyo kupinga onyo la Yesu: 'Mkiwa
katika kusali, msipayukepayuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa
watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi' (Math. 6:7). Kwa maumbile yake,
sala ya Rozari inadai mwendo mtulivu na kama kusimama kwa kuwaza, ambavyo
vimsaidie anayesali atafakari mafumbo ya maisha ya Bwana, ambayo yatazamwe
kupitia moyo wa Mama yule aliyekuwa karibu zaidi na Bwana, na vifunue utajiri
wake usiopimika».
Inafaa
tuzingatie wazo hilo la dhati la Paulo VI, ili kutokeza sura mbalimbali za
Rozari ambazo zinatia maanani sifa yake ya kuwa sala ya kumkazia macho Kristo.
Kumkumbuka Kristo pamoja na Maria
13.
Kwa Maria, kuzama katika mafumbo ni hasa kukumbuka. Lakini ni lazima tuelewe
hilo kwa maana ya Kibiblia ya neno (zakar), ambayo inafanya matendo aliyoyatenda
Mungu katika historia ya wokovu yawe ya leo. Biblia ni simulizi la matukio ya
wokovu, ambayo kilele chake ni Kristo mwenyewe. Matukio hayo siyo "jana"
tu, bali ni "leo" ya wokovu. Jambo hilo la kufanya tukio lililopita
liwe la leo pia linatendeka hasa katika liturujia: yale ambayo Mungu aliyatenda
karne kadhaa zilizopita hayawahusu tu wale walioyashuhudia kwa wakati wake, bali
yanamfikia kwa zawadi yake ya neema mtu wa wakati wowote. Kwa namna fulani hilo
ni kweli pia kwa njia nyingine za kujihusisha kwa imani na matukio hayo: «kuyakumbuka»
kwa msimamo wa imani na upendo, maana yake ni kujiweka wazi kupokea neema ambayo
Kristo ametupatia kwa mafumbo ya maisha, kifo na ufufuko wake.
Kwa
hiyo, wakati ni lazima tusisitize tena pamoja na Mtaguso wa pili wa Vatikano
kwamba liturujia, iliyo utekelezaji wa ukuhani wa Kristo na ibada rasmi ya
hadhara, ndiyo «kilele ambacho utendaji wote wa Kanisa unakilenga na papo hapo
chemchemi ambamo nguvu zake zote zinabubujika», ni lazima pia tukumbuke kwamba
maisha ya Kiroho «hayaishii katika kushiriki liturujia takatifu tu. Mkristo
ameitwa kusali pamoja na wenzake, hata hivyo anatakiwa pia kuingia katika chumba
chake cha ndani ili kumuomba Baba sirini (taz. Mt 6:6); tena anatakiwa kusali
bila ya kikomo, kama mtume Paulo alivyofundisha (taz. 1Ts 5:17)». Rozari
inaingia kwa namna yake maalumu katika
mandhari hiyo yote ya sala 'isiyokoma', na ikiwa liturujia, iliyo kazi ya Kristo
na ya Kanisa lake, ni kazi ya wokovu kwa namna bora, Rozari, iliyo tafakuri juu
ya Kristo pamoja na Maria, ni kuzama ndani ya mafumbo kunakoleta wokovu. Kwa
kuwa kuzama katika maisha ya Mkombozi, fumbo baada ya fumbo, kunasababisha
kwamba, yale ambayo mwenyewe aliyatenda na ambayo liturujia inafanya yawe ya leo,
yapokewe na mwamini kwa dhati na kuunda maisha yake.
Kufundishwa na Maria juu ya Kristo
14.
Kristo ndiye Mwalimu hasa, yeye aliye mfunuaji na ufunuo wenyewe. Si swala la
kujifunza tu maneno aliyoyafundisha, bali la 'kumsoma mwenyewe'. Lakini nani
mwalimu mzoefu kuliko Maria katika jambo hilo? Ikiwa upande wa Mungu Roho
Mtakatifu ndiye Mwalimu wa ndani anayetufikisha kwenye ukweli wote wa Kristo (taz.
Yoh 14:26; 15:26; 16:13), upande wa binadamu hakuna anayemfahamu Kristo vizuri
kuliko Maria, hakuna anayeweza kama Mama yake kutuingiza katika ujuzi wa dhati
wa fumbo lake.
'Ishara' ya kwanza iliyotendwa na Yesu
- kugeuza maji kuwa divai kwenye arusi ya Kana - inatuonyesha Maria katika
nafasi hiyo ya mwalimu, akiwahimiza watumishi watekeleze maagizo ya Kristo (taz.
Yoh 2:5). Na tunaweza kubuni kwa hakika kwamba, kazi hiyo mwenyewe aliifanya kwa
ajili ya wanafunzi baada ya Yesu kupaa mbinguni, ambao alibaki pamoja nao
wakimngojea Roho Mtakatifu, akawafariji katika mwanzo wa utume wao. Kupitia
pamoja na Maria mafumbo ya Rozari ni kama kuketi 'shuleni' pa Maria ili kumsoma
Kristo, ili kupenya siri zake, ili kuelewa ujumbe wake. Shule hiyo ya Maria
inaleta faida kubwa, hasa tukizingatia kwamba anafanya kazi hiyo kwa kutupatia
kwa wingi vipaji vya Roho Mtakatifu na papo hapo kwa kutupendekezea mfano wa ile
«hija ya imani», ambayo yeye ni mwalimu wake asiye na kifani. Mbele ya kila
fumbo la Mwanae, mwenyewe anatualika, kama alivyofanya siku aliyopashwa habari
na malaika, tuulize kwa unyenyekevu maswali yanayotufungulia mwanga, halafu
tumalizie daima kwa utiifu wa imani: «Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe
kwangu kama ulivyosema» (Lk 1:38).
Kujilinganisha na Kristo pamoja na Maria
15.
Maisha ya Kiroho ya Kikristo sifa yake kuu ni juhudi ya mwanafunzi
kujilinganisha na Mwalimu wake zaidi na zaidi (taz. Rom 8:29; Fil 3:10,21).
Miminiko la Roho katika ubatizo, linalomwingiza mwamini kama tawi ndani ya
mzabibu ambao ni Kristo (taz. Yoh 15:5), linamfanya kiungo cha mwili wake wa
fumbo (taz. 1Kor 12:12; Rom 12:5). Lakini umoja huo wa msingi unatakiwa kufuatwa
na safari ya kuungana naye zaidi na zaidi, ambayo ielekeze zaidi na zaidi
mwenendo wa mwanafunzi kadiri ya 'nia' ya Kristo: «Iweni na nia iyohiyo ndani
yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu » (Fil 2:5). Kadiri ya maneno ya
Mtume ni lazima «kumvaa Kristo» (taz. Rom 13:14; Gal 3:27).
Katika
safari ya Kiroho ya Rozari, ambayo msingi wake ni kuukazia macho mfululizo uso
wa Kristo pamoja na Maria, kipeo hicho kigumu cha kujilinganisha naye kinalengwa
kwa njia ya kumkaribia 'kirafiki'. Hiyo inatuingiza kwa urahisi katika maisha ya
Kristo na kutufanya 'tupumue' hisia zake. Kuhusu jambo hilo mwenye heri Bartolo
Longo alisema, «Kama vile marafiki wawili, wakishirikiana mara nyingi, huwa
wanafanana katika mwenendo pia, sisi tukiongea kidugu na Yesu na Bikira, katika
kutafakari mafumbo ya Rozari, na kuishi pamoja nao kwa Ekaristi, tunaweza
kufanana nao, kadiri unyonge wetu unavyoruhusu, na kujifunza kutoka kwa
vielelezo hivyo bora maisha ya unyenyekevu, ya ufukara, yaliyofichika, ya subira
na makamilifu».
Kwa
safari hiyo ya kujilinganisha na Kristo, katika Rozari tunajiaminisha kwa namna
ya pekee kwa kazi ya kimama ya Bikira mtakatifu. Yeye aliye mzazi wa Kristo,
huku akiwa mwenyewe kiungo cha
Kanisa, tena «kiungo bora na cha pekee kabisa», kwa wakati huohuo ni pia 'Mama
wa Kanisa'. Kulingana na hadhi hiyo anazidi 'kuzaa' wana kwa Mwili wa fumbo wa
Mwanae. Anafanya hivyo kwa njia ya dua, akiwaombea miminiko la Roho ambalo
halina mwisho. Maria ndiye picha kamili ya umama wa Kanisa.
Rozari
inatusogeza kifumbo karibu na Maria aliyewajibika kusaidia ustawi wa kibinadamu
wa Kristo katika nyumba ya Nazareti. Hiyo inamwezesha kutulea na kutuunda kwa
juhudi hizohizo hadi Kristo “aundwe” kikamilifu ndani mwetu (taz. Gal 4:19).
Kazi hiyo ya Maria, ambayo inategemea na kulenga kabisa ile ya Kristo,
“haizuii hata kidogo muungano wa moja kwa moja wa waamini na Kristo, bali
inausaidia”. Ndilo wazo angavu lililotokezwa na Mtaguso wa pili wa Vatikano,
ambalo nimeling'amua kwa nguvu sana maishani mwangu, nikilifanya msingi wa tamko
langu la kiaskofu: Totus tuus.
Inavyoeleweka, tamko hilo linatokana na mafundisho ya mtakatifu Alois Maria
Grignion de Montfort, ambaye alieleza ifuatavyo nafasi ya Maria katika safari ya
kila mmojawetu ya kujilinganisha na Kristo: «Ukamilifu wetu wote umo katika
kulingana, kuungana na kuwekwa wakfu kwa Yesu Kristo. Kwa hiyo bila ya shaka
ibada iliyo kamili kuliko zote ni ile ambayo inatulinganisha, inatuunganisha na
kutuweka wakfu kikamilifu zaidi kwa Yesu Kristo. Basi, kwa kuwa Maria ndiye
kiumbe aliyelingana zaidi na Yesu Kristo, kati ya ibada zote ile inayomweka
wakfu na kumlinganisha zaidi mtu kwa Bwana wetu ni ibada kwa Maria, Mama yake
mtakatifu, tena kadiri atakavyowekwa wakfu kwake atawekwa wakfu kwa Yesu Kristo».
Hakuna nafasi nyingine kuliko Rozari ambapo njia ya Kristo na ya Maria
zinaonekana kuwa ni moja kwa dhati. Maria anaishi ndani ya Kristo tu na kwa
ajili ya Kristo!
Kumuomba Kristo pamoja na Maria
16.
Kristo ametualika tumuelekee Mungu kwa udumifu na tumaini ili tusikilizwe: «Ombeni,
nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa» (Math 7:7).
Msingi wa uwezo huo wa sala ni wema wa Baba, lakini pia ushenga wa Kristo
mwenyewe mbele yake (taz. 1Yoh 2:1) na kazi ya Roho Mtakatifu ambaye «hutuombea»
kadiri ya mipango ya Mungu (taz. Rom 8:26-27). «Kwa maana hatujui kuomba jinsi
itupasavyo» (Rom 8:26) na pengine hatusikilizwi kwa sababu «tunaomba vibaya»
(taz. Yak 4:2-3).
Ili
kuchangia sala ambayo Kristo na Roho wanabubujisha moyoni mwetu, Maria anaingia
kati kwa maombezi yake ya kimama. «Sala ya Kanisa ni kama inategemezwa na sala
ya Maria». Kwa kweli, Yesu, mshenga pekee, akiwa ndiye njia ya sala yetu, Maria,
aliye picha yake angavu, anaionyesha hiyo njia na «kwa msingi wa ushirikiano
huo wa pekee wa Maria na kazi ya Roho Mtakatifu, Makanisa yamestawisha sala kwa
Mama mtakatifu wa Mungu, yakifanya ilenge kwenye nafsi ya Kristo
iliyodhihirishwa katika mafumbo yake». Kwenye arusi ya Kana Injili inaonyesha
hiyo nguvu ya maombezi ya Maria, aliyejifanya sauti ya shida za watu kwa Yesu:
«Hawana divai» (Yoh 2:3).
Rozari
ni tafakuri na dua kwa pamoja. Kumlilia kwa bidii Mama wa Mungu, msingi wake ni
tumaini la kwamba maombezi yake ya kimama yanaweza yote moyoni mwa Mwanae.
Alivyosema mwenye heri Bartolo Longo katika Dua kwa Bikira, akitumia neno la
kusisimua linalohitaji kueleweka vizuri, Maria ni «Mwenyezi kwa neema». Hakika
hiyo, ambayo chanzo chake ni Injili, imeimarishwa na mang'amuzi ya taifa la
Kristo. Mwanashairi bora Dante aliitafsiri vizuri ajabu, kufuatana na mtakatifu
Bernardo, akiimba: «Mama, wewe u mkuu na mwenye uwezo hivi kwamba, /
anayetaka neema asikukimbilie wewe, / hamu yake inataka kuruka pasipo
mabawa». Maria, patakatifu pa Roho Mtakatifu (taz. Lk 1:35), wakati anapoombwa
nasi katika Rozari, anatusimamia mbele ya Baba aliyemjaza neema na ya Mwana
aliyezaliwa kutoka tumboni mwake, akisali pamoja nasi na kwa ajili yetu.
Kumtangaza
Kristo pamoja na Maria
17.
Rozari ni pia safari ya kutangaza na kuchimba, ambamo fumbo la Kristo
linatokezwa upya mfululizo kwa ngazi mbalimbali za maisha ya Kikristo. Namna
yake ni ya kulitokeza upande wa sala na wa kuzama ndani ya mafumbo, ambayo
inalenga kumuunda mfuasi kadiri ya moyo wa Kristo. Kwa kweli katika kusali
Rozari, ikiwa sehemu zake zote zinazoweza kuchangia tafakuri ya nguvu zinatumika
ipasavyo, inapatikana nafasi muhimu ya katekesi, hasa katika adhimisho la
kijumuia kwenye parokia na patakatifu. Wachungaji wanatakiwa kuitumia nafasi
hiyo. Bikira wa Rozari anaendelea hivyo pia kazi yake ya kumtangaza Kristo.
Historia ya Rozari inaonyesha jinsi sala hiyo ilivyotumiwa hasa na Wadominiko,
katika kipindi kilichokuwa kigumu kwa Kanisa kutokana na uenezi wa uzushi. Leo
tuko mbele ya changamoto mpya. Kwa nini tusishike tena tasbihi mikononi kwa
imani ile waliyokuwa nayo waliotutangulia? Rozari inadumu kuwa na nguvu zake
zote na kuendelea kuwa silaha muhimu kati ya vifaa vya kichungaji vya kila
mwenezainjili halisi.
SURA YA PILI
MAFUMBO
YA KRISTO - MAFUMBO YA MAMA
Rozari «muhtasari wa Injili»
18.
Hatuwezi kuanza kuukazia macho uso wa Kristo bila ya kusikiliza, katika Roho,
sauti ya Baba, kwa sababu «hakuna amjuaye Mwana, ila Baba» (Math 11:27).
Karibu na Kaisarea Filipi, baada ya ungamo la Petro, Yesu alifafanua asili ya
hisi hiyo sahihi hivi ya undani wake mwenyewe: «Mwili na damu havikukufunulia
hili, bali Baba yangu aliye mbinguni» (Math 16:17). Kwa hiyo ni lazima
kufunuliwa kutoka juu. Lakini ili tuupokee ufunuo huo ni lazima kusikiliza.
Mang'amuzi ya kimya na ya sala tu yanatupatia upeo wa kufaa ambapo unaweza
kukomaa na kustawi ujuzi halisi zaidi wa fumbo hilo, ambao unaunganisha na kutia
uaminifu.
Rozari
ni njia mojawapo ya mapokeo ya sala ya Kikristo kwa ajili ya kuzama katika uso
wa Kristo. Papa Paulo VI aliifafanua hivi: « Rozari ikiwa sala ya Kiinjili,
ambayo kiini chake ni fumbo la umwilisho ulioleta ukombozi, basi ni sala
inayomlenga Kristo moja kwa moja. Kwa kuwa hata jambo lake maalumu zaidi
- yaani kukariri kilitania Salamu Maria - linakuwa sifa isiyokoma kwa
Kristo, lengo kuu la tangazo la malaika na la salamu ya mama wa Mbatizaji: 'Mzao
wa tumbo lako amebarikiwa' (Lk 1:42). Tuseme zaidi: kukariri Salamu Maria ni
kama kitambaa ambacho juu yake tunafuma tendo la kuzama katika mafumbo: Yesu
anayekumbushwa na kila Salamu Maria ni yuleyule ambaye mfululizo wa mafumbo
unatutolea mara kwa mara kama Mwana wa Mungu na wa Bikira».
Ukamilisho wa kufaa
19.
Kati ya mafumbo mengi ya maisha ya Kristo, Rozari, kwa jinsi ilivyoundika katika
desturi iliyopitishwa na mamlaka ya Kanisa, inayapendekeza machache tu. Chaguo
hilo lililazimishwa na mpango asili wa sala hiyo wa kulingana na idadi ya Zaburi
150.
Hata
hivyo naona kwamba, ili kuongeza uzito wa Kikristo wa Rozari, inafaa
kuikamilisha kwa namna ambayo, ingawa inaachwa ifanyiwe kazi kwa hiari na mtu
mmojammoja na jumuia nzima, iiwezeshe kukumbatia pia matendo ya maisha ya
hadhara ya Kristo kati ya ubatizo na mateso. Kwa kuwa katikati ya mafumbo hayo
tunakazia macho pande muhimu za nafsi ya Kristo kama yule aliyetufunulia Mungu
moja kwa moja. Ndiye yule ambaye, kisha kutambulishwa kama Mwana mpendwa wa Baba
kwenye ubatizo katika mto Yordani, aliutangaza ujio wa Ufalme, aliushuhudia kwa
matendo na kutangaza madai yake. Ni katika miaka ya maisha ya hadhara kwamba
fumbo la Kristo lilidhihirika kwa namna ya pekee kama fumbo la mwanga: «Muda
nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu» (Yoh 9:5).
Basi,
ili Rozari iweze kuitwa kwa haki zaidi 'muhtasari wa Injili', inafaa kwamba,
kisha kukumbuka umwilisho na maisha yaliyofichika ya Kristo (mafumbo ya furaha),
na kabla ya kuzingatia uchungu wa mateso (mafumbo ya uchungu) na ushindi wa
ufufuko (mafumbo ya utukufu), tafakuri ilenge pia nafasi kadhaa za maana zaidi
za maisha ya hadhara (mafumbo ya mwanga). Ongezeko hilo la mafumbo mapya, bila
ya kuhatarisha jambo lolote la msingi katika sura ya kimapokeo ya sala hiyo,
linakusudiwa kuifanya izingatiwe upya katika maisha ya Kiroho ya Wakristo, kama
namna halisi ya kuingizwa vilindini mwa moyo wa Kristo, ulio kina kirefu cha
furaha na mwanga, uchungu na utukufu.
Mafumbo
ya furaha
20.
Mfululizo wa kwanza, ule wa 'mafumbo ya furaha', kwa kweli
sifa yake maalumu ndiyo furaha iliyosambazwa na tukio la umwilisho. Hiyo
ni wazi tangu Kupasha Habari, ambapo salamu ya Gabrieli kwa Bikira wa Nazareti
inajilinganisha na mwaliko wa kuwa na furaha ya Kimasiha: «Furahi, Maria».
Tangazo hilo ni lengo la historia yote ya wokovu, tena la historia ya ulimwengu
pia. Kwa sababu, ikiwa mpango wa Baba ni kujumlisha vyote katika Kristo (taz. Ef
1:10), kwa namna fulani ulimwengu wote ndio uliofikiwa na fadhili ya Kimungu
ambayo Baba alimuinamia Maria ili kumfanya Mama wa Mwanae. Upande mwingine,
binadamu wote ni kama wanaingia ndani ya fiat
ambayo Maria aliyakubali mara matakwa ya Mungu.
Halafu tukio la kukutana na Elizabeti
limejaa shangwe, ambapo sauti yenyewe ya Maria na uwemo wa Kristo tumboni mwake
vilifanya Yohane «kikaruka kwa shangwe» (taz. Lk 1:44). Limejaa furaha
vilevile tukio la Bethlehemu, ambapo kuzaliwa kwa Mtoto wa Kimungu, Mwokozi wa
dunia, kuliimbwa na malaika na kutangazwa kwa wachungaji kama «furaha kuu» (Lk
2:10).
Lakini
mafumbo mawili ya mwisho, ingawa yanaendelea kuwa na ladha ya furaha, yanadokeza
tayari dalili za janga. Kwa kuwa Kutolewa hekaluni, huku kukitokeza furaha ya
kuwekwa wakfu na ya kumzamisha mzee Simeoni katika fumbo, kunaleta pia utabiri
juu ya «ishara itakayonenewa» ambayo huyo Mtoto atakuwa kwa Israeli, na juu ya
upanga utakaochoma moyo wa Mama (taz. Lk 2:34-35). Vilevile ni la furaha na la
kusikitisha kwa pamoja tukio la Yesu hekaluni akiwa na umri wa miaka kumi na
miwili. Hapo alitokea katika hekima yake ya Kimungu, huku akisikiliza na kuhoji,
akiwa kimsingi yule mwenye 'kufundisha'. Ufunuo wa fumbo lake kama Mwana
anayewajibika kabisa kwa mambo ya Baba ni tangazo la ile nia imara ya Kiinjili
ambayo mbele ya madai ya moja kwa moja ya Ufalme inatia shakani hata mafungamano
mapendevu zaidi kwa binadamu. Yosefu na Maria wenyewe, waliohangaika na
kufadhaika, «hawakuelewa na neno hilo alilowaambia» (Lk 2:50).
Hivyo
kutafakari mafumbo 'ya furaha' ni kuingia ndani ya sababu kuu na maana ya dhati
ya furaha ya Kikristo. Ni kukazia macho uhalisi wa fumbo la umwilisho na utabiri
usio wazi wa fumbo la uchungu wenye kuokoa. Maria anatuongoza tuelewe siri ya
furaha ya Kikristo, akitukumbusha kwamba Ukristo ni hasa euangelion,
'habari njema', ambayo kiini chake, tena yaliyomo yake yote ni nafsi ya Kristo,
Neno aliyefanyika mwili, Mwokozi pekee wa ulimwengu.
Mafumbo ya mwanga
21.
Sala hasa, ikivuka toka utoto na maisha ya Nazareti hadi maisha ya hadhara ya
Yesu, inatufikisha kwenye mafumbo ambayo yanaweza kuitwa kwa namna ya pekee 'mafumbo
ya mwanga'. Kwa kweli, fumbo lote la Kristo ni mwanga. Ndiye «nuru ya ulimwengu»
(Yoh 8:12). Lakini sifa hiyo inajitokeza hasa katika miaka ya maisha ya hadhara,
ambapo yeye alitangaza habari njema ya Ufalme. Nikitaka kuionyesha jumuia ya
Kikristo nafasi tano za maana - mafumbo 'ya mwanga' – za kipindi hicho cha
maisha ya Kristo, naona inafaa kuzibainisha kama ifuatavyo: 1. katika ubatizo
wake kwenye Yordani, 2. katika kujifunua kwake kwenye arusi ya Kana, 3. katika
kutangaza Ufalme wa Mungu pamoja na mwaliko wa kuongoka, 4. katika kung’aa
kwake alipogeuka sura, na, hatimaye, 5. katika kuweka ekaristi, sakramenti ya
fumbo la Pasaka.
Kati
ya mafumbo hayo kila mojawapo linafunua Ufalme uliokwishafika katika nafsi
yenyewe ya Yesu. Kwanza, ubatizo kwenye Yordani. Hapo, Kristo aliposhukia maji
ya mto, kama yule asiye na doa anayejifanya ‘dhambi’ kwa ajili yetu (taz.
2Kor 5:21), mbingu zilifunguka na sauti ya Baba ilimtangaza kuwa ni Mwanae
mpenzi (taz. Math 3:17 na aya sambamba), huku Roho akimshukia ili kumweka wakfu
kwa utume unaomkabili. Pili, mwanzo wa ishara huko Kana (taz. Yoh 2:1-12),
ambapo Kristo, akigeuza maji kuwa divai, aliifungua mioyo ya wanafunzi isadiki
kutokana na Maria kuingilia kati, yeye aliye wa kwanza kati ya waamini. Tatu,
mahubiri ambayo Yesu alitangaza ujio wa Ufalme wa Mungu na kualika watu watubu (taz.
Mk 1:15), akiondolea dhambi za wanaomkaribia kwa tumaini nyenyekevu (taz. Mk
2:3-13; Lk 7:47-48), mwanzo wa ile huduma ya huruma atakayoendelea kutoa hadi
mwisho wa dunia, hasa kwa njia ya sakramenti ya upatanisho aliyolikabidhi Kanisa
lake (taz. Yoh 20:22-23). Halafu kwa namna ya pekee tukio la kugeuka sura,
ambalo kadiri ya mapokeo lilitokea juu ya mlima Tabori. Utukufu wa umungu
uling’aa katika uso wa Kristo, huku Baba akimtambulisha kwa mitume
waliochanganyikiwa na uzuri huo akidai wamsikilize (taz. Lk 9:35 na aya sambamba)
na wajiandae kuishi pamoja naye nafasi chungu ya mateso, ili kufikia pamoja naye
furaha ya ufufuko na maisha yaliyogeuzwa sura na Roho Mtakatifu. Hatimaye, ni
fumbo la mwanga tendo la kuweka ekaristi, ambamo Kristo anajifanya chakula kwa
Mwili wake na Damu yake ndani ya maumbo ya mkate na divai, akishuhudia «upeo»
wa upendo wake kwa ajili ya ulimwengu (Yoh 13:1), ambao akajitoa sadaka kwa
wokovu wake.
Uwepo
wa Maria hauonekani katika mafumbo hayo, isipokuwa Kana. Injili zinadokeza tu
mara moja moja uwepo wake katika nafasi hii au hii ya mahubiri ya Yesu (taz. Mk
3:31-35; Yoh 2:12) na hazisemi kitu kuhusu uwezekano wa kuwepo kwake karamuni
wakati wa kuweka ekaristi. Lakini kazi aliyoifanya Kana inasindikiza, kwa namna
fulani, safari yote ya Kristo. Ufunuo ule ambao katika ubatizo kwenye Yordani
ulitolewa na Baba moja kwa moja ukarudiwa na Mbatizaji kama mwangwi wake, huko
Kana ulikuwemo kinywani mwa Maria, ulipogeuka kuwa onyo kuu la kimama ambalo
analitoa kwa Kanisa la nyakati zote: «Lolote atakalowaambia, fanyeni» (Yoh
2:5). Hilo ni onyo linalofaa kutangulia maneno na ishara ya Kristo katika maisha
ya hadhara, likiendelea kuonekana nyuma ya 'mafumbo yote ya mwanga' ili
tuyazingatie kadiri ya Maria.
Mafumbo ya uchungu
22.
Injili zinatia maanani sana mafumbo ya uchungu ya Kristo. Tangu zamani ibada ya
Kikristo, hasa wakati wa Kwaresima, kupitia Njia ya Msalaba, imezingatia kwa
makini kila tukio la mateso, ikihisi kwamba humo ndimo kilele cha ufunuo wa
upendo na ndimo chemchemi ya wokovu wetu. Rozari imechagua baadhi ya matukio ya
mateso, ikimhimiza anayeisali kuyakazia macho ya moyo na kuyaishi upya. Safari
ya tafakuri inaanza huko Getsemani, ambako Kristo aliishi nafasi ya uchungu wa
pekee mbele ya matakwa ya Baba, ambayo udhaifu wa mwili unashawishiwa kuyakaidi.
Huko Kristo alishika nafasi ya vishawishi vyote vya binadamu, na mbele ya dhambi
zote za binadamu, ili amuambie Baba: «Si mapenzi yangu, bali yako yatendeke» (Lk
22:42 na aya sambamba). ‘Ndiyo’ yake hiyo ilipindua 'hapana' ya wazazi wetu
wa kwanza bustanini mwa Edeni. Jinsi utiifu huo kwa matakwa ya Baba ulivyokuwa
mgumu kwake inajitokeza katika mafumbo yanayofuata ya kupanda hadi Kalivari,
kupigwa mijeledi, kutiwa taji la miba, kufa msalabani, ambapo alidhalilishwa
kupita kiasi: Ecce homo!
Katika
kudhalilishwa hivyo haufunuliwi tu upendo wa Mungu, bali pia maana yenyewe ya
binadamu. Ecce homo: anayetaka
kufahamu mtu alivyo, anapaswa kutambua maana, mzizi na utimilifu wake katika
Kristo, Mungu aliyejishusha kwa upendo «hata mauti, naam, mauti ya msalaba» (Fil
2:8). Mafumbo ya uchungu yanamuongoza mwamini kuishi upya kifo cha Yesu kwa
kujiweka chini ya msalaba karibu na Maria, ili kuzama pamoja na Mama katika
kilindi cha upendo wa Mungu kwa binadamu na kuhisi nguvu zake zote za kuletea
uhai mpya.
Mafumbo ya utukufu
23.
«Kuukazia macho uso wa Kristo hakuwezi kuishia kwenye picha yake kama msulubiwa.
Yeye yupo amefufuka!». Tangu zamani Rozari inatokeza hakika hiyo ya imani,
ikimualika mwamini avuke ng’ambo ya giza la mateso, ili kuukazia macho utukufu
wa Kristo katika ufufuko na katika Kupaa mbinguni. Mkristo akimkazia macho
Mfufuka anavumbua upya sababu za imani yake (taz. 1Kor 15:14), na kuishi upya
furaha sio tu ya wale ambao Kristo aliwatokea – mitume, Magdalena, wanafunzi
wa Emau -, bali pia furaha ya Maria, ambaye alitakiwa kuwa na mang’amuzi si
mapungufu ya uhai mpya wa Mwana aliyetukuzwa. Katika utukufu huo ambao, kwa
Kupaa kwake, ulimweka Kristo kuumeni kwa Baba, Maria mwenyewe akainuliwa kwa
Kupalizwa kwake, akifikia, kwa fadhili ya pekee kabisa, kutanguliza hali
waliyoandaliwa waadilifu wote kwa ufufuko wa mwili. Hatimaye, akitiwa taji la
utukufu – anavyoonekana katika fumbo la mwisho la utukufu – anang’aa kama
Malkia wa malaika na wa watakatifu, utangulizi na kilele cha hali ya milele ya
Kanisa.
Kama
kiini cha safari hiyo ya utukufu wa Mwana na wa Mama, Rozari inaipanga, katika
fumbo la tatu la utukufu, Pentekoste, inayoonyesha uso wa Kanisa kama familia
iliyounganika na Maria, iliyouhishwa na miminiko la nguvu la Roho, iliyo tayari
kwa utume wa uinjilishaji. Kuzama katika fumbo hilo, sawa na mafumbo mengine ya
utukufu, kunatakiwa kuwafanya waamini waelewe kwa namna hai zaidi na zaidi
maisha yao mapya katika Kristo, ndani ya ukweli wa Kanisa, maisha ambayo tukio
la Pentekoste ndiyo ‘picha' yake bora. Hivyo mafumbo ya utukufu yanalisha
ndani ya waamini tumaini la lengo la milele wanalolielekea kama viungo vya taifa
la Mungu linalohiji katika historia. Hiyo inatakiwa kuwasukuma washuhudie
kishujaa ile «habari njema» inayotia maanani maisha yao yote.
Toka 'mafumbo' hadi 'fumbo': njia ya Maria
24.
Bila ya shaka hiyo mifululizo ya tafakuri inayopendekezwa na Rozari takatifu
haimalizi yote, ila inakumbusha yaliyo ya lazima, ikiingiza roho ionje ule ujuzi
wa Kristo ambao unachota mfululizo kwenye chemchemi safi ya kitabu cha Injili.
Kila jambo la maisha ya Kristo, linavyosimuliwa na Wainjili, linang’aa kwa
fumbo lile lipitalo ujuzi wote (taz. Ef 3:19).
Ndilo fumbo la Neno aliyefanyika mwili, ambamo «unakaa utimilifu wote wa
Mungu, kwa jinsi ya kimwili» (Kol 2:9). Ndiyo sababu Katekisimu ya Kanisa
Katoliki inasisitiza sana mafumbo ya Kristo, ikikumbusha kwamba «katima maisha
ya Yesu yote ni ishara ya fumbo lake». Neno la «duc
in altum» la Kanisa katika milenia ya tatu linapimwa na uwezo wa Wakristo
wa «kujua kabisa siri ya Mungu, yaani, Kristo; ambaye ndani yake yeye hazina
zote za hekima na maarifa zimesitirika» (Kol 2:2-3). Matashi motomoto ya barua
kwa Waefeso (3:17-19) yanaelekea
kila aliyebatizwa: «Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na
msingi katika upendo; ili mpate [...] kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu
kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu».
Rozari
inataka kutumikia kipeo hicho, ikitolea 'siri' ya kujiweka wazi kwa urahisi
zaidi kumjua Kristo kwa dhati na kwa kuwajibika zaidi. Tunaweza kuiita njia ya
Maria. Ni njia ya kielelezo cha Bikira wa Nazareti, mwanamke wa imani, wa kimya
na wa usikivu. Ni pia njia ya ibada ya Kimaria inayohuishwa na hakika ya
fungamano la moja kwa moja kati ya Kristo na Mama yake mtakatifu sana: kwa namna
fulani, mafumbo ya Kristo ni pia mafumbo ya Mama, hata pale asipohusika moja kwa
moja, kutokana na kwamba Maria aliishi ndani ya Yesu na kwa ajili yake. Katika
Salamu Maria tukijitwalia maneno ya malaika Gabrieli na ya mtakatifu Elizabeti,
tunajisikia msukumo wa kumtafuta upya daima kwa Maria, katika mikono yake na
katika moyo wake, yule «mzao wa tumbo lake aliyebarikiwa» (taz. Lk 1:42).
Fumbo la Kristo, 'fumbo' la binadamu
25.
Katika ushuhuda niliokwishataja kwamba niliutoa mwaka 1978 kuwa Rozari ndiyo
sala yangu pendevu kuliko zote, nilitokeza wazo ambalo nataka kulisisitiza.
Hapo
nilisema kuwa «sala sahili ya Rozari inapiga madundo ya maisha ya binadamu».
Kwa mwanga wa tafakuri za hapa juu kuhusu mafumbo ya Kristo, si vigumu kuchimba
uhusiano huo wa Rozari na ubinadamu. Uhusiano huo ni wa msingi kuliko
unavyoonekana mara moja. Anayetulia katika kumkazia macho Kristo kwa kufuata
hatua za maisha yake, hawezi kukosa kukuta ndani mwake ukweli kuhusu binadamu
pia. Ndio tamko kuu la Mtaguso wa pili wa Vatikano, ambalo nimelifundisha mara
nyingi kuanzia barua rasmi Redemptor
Hominis: «Kwa kweli, fumbo la binadamu linaeleweka vizuri katika fumbo la
Neno aliyefanyika mwili tu». Rozari inasaidia kujiandaa kupokea mwanga huo. Kwa
kufuata safari ya Kristo, ambamo safari ya binadamu «imejumlishwa»,
imefunuliwa na kukombolewa, mwamini anajiweka mbele ya sura ya mtu halisi.
Akikazia macho kuzaliwa kwake anajifunza uhai ulivyo mtakatifu, akitazama nyumba
ya Nazareti anajifunza ukweli asili kuhusu familia kadiri ya mpango wa Mungu,
akimsikiliza Mwalimu katika mafumbo ya maisha ya hadhara anapokea mwanga ili
kuingia katika Ufalme wa Mungu na, akimfuata katika njia ya Kalivari, anajifunza
maana ya uchungu kwa wokovu. Hatimaye, akiwakazia macho Kristo na Mama yake
katika utukufu, anaona lengo ambalo kila mmoja ameitiwa, akikubali kuponywa na
kugeuzwa sura na Roho Mtakatifu. Hivyo tunaweza kusema kuhusu kila fumbo la
Rozari kwamba, likizingatiwa vizuri, linaangaza fumbo la binadamu.
Wakati
huohuo, inamtokea mtu, hata bila ya kukusudia, kuleta kwenye mkutano huo na utu
mtakatifu wa Mkombozi matatizo, mafadhaiko, kazi na mipango mingi ambayo
inaathiri maisha yetu. «Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza » (Zab
56:22). Kutafakari kwa njia ya Rozari ni kukabidhi mahangaiko yetu kwa mioyo
yenye huruma ya Kristo na Mama yake. Miaka ishirini na tano baadaye, nikikumbuka
majaribu ambayo sijayakosa katika kutimiza huduma ya Petro, najisikia kusisitiza,
kama mwaliko wa dhati kwa wote wa kujipatia mang’amuzi hayo, kwamba kweli
Rozari «inapiga madundo ya maisha ya binadamu», ili yalingane na madundo ya
maisha ya Mungu, katika ushirika mfurahivu na Utatu mtakatifu, lengo na shauku
ya maisha yetu.
SURA YA TATU
KWANGU
MIMI KUISHI NI KRISTO
Rozari, njia ya kulishiza fumbo
26.
Kutafakari mafumbo ya Kristo kunapendekezwa katika Rozari kwa mbinu maalumu,
ambayo kwa maumbile yake inafaa kusaidia kuyalishiza. Ni mbinu ambayo msingi
wake ni kukariri. Hiyo ni kweli kwanza kwa Salamu Maria, inayorudiwa mara kumi
kwa kila fumbo. Tukitazama kijujuu tendo hilo la kukariri, tunaweza
tukashawishika kuona Rozari ni kazi kavu na ya kukinaisha. Kumbe inawezekana
kuitathmini tasbihi tofauti sana tukiiona kama tokeo la upendo usiochoka
kumrudia mpenzi kwa maneno mengi yaliyojaa hisia ambayo, ingawa yanaonekana
kufanana, ni mapya daima kutokana na hizo hisia unaoyajaa.
Katika
Kristo, Mungu ametwaa kweli «moyo wa nyama». Yeye hana tu moyo wa Kimungu,
uliojaa huruma na msamaha, bali pia moyo wa kibinadamu, unaoweza kupata
mitikisiko yote ya mapendo. Tungehitaji ushuhuda wa Injili kuhusu jambo hilo,
isingekuwa vigumu kuukuta katika majibizano ya kugusa kati ya Kristo na Petro
baada ya ufufuko: «Je, Simoni wa Yohane, wewe wanipenda?». Swali hilo
liliulizwa hata mara tatu, na jibu vilevile lilitolewa hata mara tatu: «Naam,
Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda» (taz. Yoh 21:15-17). Mbali ya maana maalumu
ya ukurasa huo, ulio muhimu sana kwa utume wa Petro, hakuna anayekosa kuona
uzuri wa kuyarudia hayo mara tatu, ambapo sisitizo la swali na la jibu lake
linajitokeza kwa maneno yanayojulikana sana na mang’amuzi ya daima ya upendo
wa binadamu. Ili tuielewe Rozari, ni lazima tuingie katika mwendo wa saikolojia
maalumu ya upendo.
Jambo
moja ni wazi: ikiwa marudio ya Salamu Maria yanamlenga moja kwa moja Maria,
tendo la upendo linamuendea hasa Yesu, pamoja na Maria na kwa njia yake. Marudio
yanalishwa na hamu ya kujilinganisha na Kristo kikamilifu zaidi na zaidi, ambako
ndio 'mpango' halisi wa maisha ya Kikristo. Mtume Paolo alitamka mpango huo kwa
maneno ya moto: «Kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida» (Fil 1:21).
Tena: «Ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu» (Gal 2:20).
Rozari inatusaidia kukua katika kujilinganisha hivyo hadi lengo la utakatifu.
Mbinu
ya kufaa...
27.
Si ajabu kwamba fungamano na Kristo liweze kufaidika na msaada wa mbinu fulani
pia. Mungu anajishirikisha kwa binadamu akiheshimu maumbile yetu na mwendo wa
maisha. Ndiyo sababu maisha ya Kiroho ya Kikristo, ingawa yanaweza yakafikia
namna za juu zaidi za kimya cha kuzama katika mafumbo, ambapo picha zote, maneno
na matendo yote yanaachwa nyuma kutokana na nguvu ya muungano usiosemekana wa
mtu na Mungu, hata hivyo kwa kawaida ni sifa yake kumhusisha mtu mzima katika
maumbile yake changamano ya roho na mwili na katika mafungamano yake na wengine.
Hiyo
inaonekana wazi katika liturujia. Sakramenti na visakramenti vimeundwa na
mfululizo wa vitendo ambavyo vinahusisha pande mbalimbali za nafsi yetu. Hata
sala isiyo ya liturujia inatokeza haja hiyohiyo. Hiyo inathibitishwa na kwamba
huko Mashariki sala maalumu zaidi ya tafakuri ya Kikristo, ambayo kiini chake ni
maneno: «Yesu, Kristo, Mwana wa Mungu, Bwana, unihurumie mimi mkosefu»,
inaendana kimapokeo na mwendo wa kupumua, ambao, wakati unaposaidia kudumu
katika dua, unahakikisha uzito kama wa kimwili kwa hamu ya kumfanya Kristo awe
pumzi, roho na 'yote' ya maisha.
...
ambayo hata hivyo inaweza kuboreshwa
28.
Katika barua ya kitume Novo Millennio
Ineunte nilikumbusha kwamba leo, huku Magharibi pia, inasikika haja mpya ya
kutafakari, ambako pengine katika dini nyingine kuna namna za kuvutia. Hawakosekani Wakristo ambao, kwa kutojua vya kutosha mapokeo
ya Kikristo ya kuzama katika mafumbo, wanakubali kushawishiwa na mapendekezo
hayo. Lakini mara nyingi hayo kwa ndani msingi wake ni mawazo yasiyokubalika,
hata kama yana mambo mazuri ambayo yanaweza yakapatana na mang’amuzi ya
Kikristo. Katika mang’amuzi ya dini hizo pia zinatumika sana mbinu ambazo,
zikilenga roho ijikusanye kwa dhati, zinahusisha nafsi na mwili, zinakariri
maneno na kutumia ishara. Rozari inajipanga katika fremu hiyo ya kimataifa ya
mang’amuzi ya kidini, lakini inajibainisha kwa sifa za pekee zinazolingana na
madai maalumu ya Ukristo.
Kwa
kweli Rozari ni mbinu tu mojawapo ya kuzama katika mafumbo. Ikiwa ni mbinu
inatakiwa kutumika kuhusiana na lengo, isigeuke yenyewe kuwa lengo. Hata hivyo,
ikiwa ni tunda la mang’amuzi ya karne kadhaa, mbinu yenyewe inatakiwa
kuthaminiwa vya kutosha. Upande wake yanasimama mang’amuzi ya watakatifu wengi.
Lakini hayo hayamaanishi kwamba haiwezi kuboreshwa. Ndipo unapolenga ukamilisho
wa mifululizo ya mafumbo kwa mfululizo mpya wa mysteria
lucis, pamoja na mashauri kadhaa kuhusu namna ya kusali ambayo nayapendekeza
katika barua hii. Kwa njia yake sitaki kuvuruga muundo wa sala hiyo ulioimarika
sana, bali kusaidia waamini kuuelewa upande wa ishara kulingana na mahitaji ya
maisha ya kila siku. Pasipo hilo hatari siyo tu kwamba Rozari itashindwa kuzaa
matunda ya Kiroho yanayotarajiwa, bali pia kwamba tasbihi inayotumika kwa
kawaida kuisalia itakuja kutazamwa kama aina ya hirizi au chombo cha kishirikina
kwa kupotosha kabisa maana yake na kazi yake.
Kutaja fumbo
29.
Kutaja fumbo, na kwa wakati huohuo afadhali kupata nafasi ya kukazia macho picha
inayolionyesha, ni kama kuweka wazi mpangilio wa tukio la kulizingatia. Maneno
yanaongoza ubunifu na roho kwenye tukio maalumu au nafasi ya maisha ya Kristo.
Katika maisha ya Kiroho yaliyostawi ndani ya Kanisa, heshima kwa picha takatifu
na vilevile ibada mbalimbali zilizohusisha sana hizi za watu, tena na mbinu ile
iliyopendekezwa na mtakatifu Ignasi wa Loyola katika Mazoezi ya Kiroho,
zimetumia macho na ubunifu (compositio
loci), zikiviona kama msaada mkubwa kwa kukusanya roho katika fumbo. Tena
mbinu hiyo inalingana na mantiki yenyewe ya umwilisho: Mungu amependa kutwaa
katika Yesu sura ya binadamu. Ni kwa njia ya ukweli wa mwili wake kwamba sisi
tunaelekezwa kufungamana na fumbo lake la Kimungu.
Haja
hiyo ya mambo ya kushikika inaitikiwa pia na kule kutaja mafumbo mbalimbali ya
Rozari. Bila ya shaka hayo hayashiki nafasi ya Injili wala hayakumbushi kurasa
zake zote. Kwa hiyo Rozari haishiki nafasi ya lectio
divina, bali inaidai na kuistawisha. Lakini ikiwa mafumbo yanayozingatiwa
katika Rozari, yakiwa ni pamoja na ukamilisho wake kwa mysteria lucis, yanaishia katika mambo makuu ya maisha ya Kristo,
kutokana nayo roho inaweza kwa urahisi zaidi kuenea katika sehemu nyingine za
Injili, hasa Rozari inaposaliwa katika nafasi maalumu za kujikusanya kirefu
zaidi.
Kusikiliza Neno la Mungu
30.
Ili tafakuri ipewe msingi wa Kibiblia na udhati mkubwa zaidi, inafaa baada ya
kutaja fumbo kuwe na tangazo la dondoo la Biblia linalohusika ambalo linaweza
kuwa refu kadiri ya hali. Kwa kuwa maneno mengine hayafikii kamwe nguvu maalumu
ya Neno lililovuviwa na Mungu. Hilo linatakiwa kusikilizwa kwa hakika ya kwamba
ni Neno lake lililotamkwa kwa ajili ya leo na «kwa ajili yangu».
Likipokewa
hivyo, linaingia katika mbinu ya kukariri ya Rozari bila ya kusababisha ukinaifu
unaoweza ukatokana na kukumbusha tu habari inayojulikana sana. Hapana, kazi si
kukumbuka habari, bali kuacha Mungu ‘aseme’. Katika nafasi fulani ya fahari
na ya kijumuia inaweza ikafaa Neno hilo lifafanuliwe kifupi.
Kimya
31.
Usikivu na tafakuri vinajilisha kimya. Inafaa kwamba, baada ya kutaja fumbo na
kutangaza Neno, tutulie kwa muda wa kufaa ili kulikazia macho fumbo la
kufikiriwa, kabla hatujaanza sala ya midomo. Kuvumbua upya thamani ya kimya ni
siri mojawapo ya utekelezaji wa sala hasa na wa tafakuri. Kati ya kasoro za
jamii iliyotawaliwa na teknolojia na vyombo vya habari, mojawapo ni kwamba kimya
kinazidi kuwa kigumu. Kama vile katika liturujia zinapendekezwa nafasi za kimya,
hata katika kusali Rozari inafaa nafasi fupi ya kutulia baada ya kulisikiliza
Neno la Mungu, wakati roho inapolenga yaliyomo katika fumbo maalumu.
«Baba
Yetu»
32.
Baada ya kusikiliza Neno na kulenga fumbo, hakuna budi kujiinua kwa Baba. Yesu,
katika kila fumbo lake, anatufikisha daima kwa Baba, anayemuelekea mfululizo,
kwa kuwa ametulia 'kifuani' pake (taz. Yoh 1:18). Yeye anataka kutuingiza katika
urafiki wa dhati na Baba, ili tuseme pamoja naye «Aba!, Baba» (Rm 8:15; Gal
4:6). Ni katika uhusiano na Baba kwamba yeye anatufanya kuwa ndugu zake na ndugu
sisi kwa sisi, akitushirikisha Roho ambaye ni wa kwake na wa Baba kwa pamoja.
Sala ya Baba Yetu, ikiwekwa kama msingi fulani wa tafakuri juu ya Kristo na
Maria inayostawi kwa njia ya kukariri Salamu Maria, inafanya tafakuri hiyo ya
fumbo kuwa mang’amuzi ya Kikanisa hata inapofanyika upwekeni.
«Salamu
Maria» kumi
33. Ndiyo sehemu kubwa zaidi ya Rozari
na papohapo ndiyo inayoifanya iwe sala ya Kimaria kwa namna ya pekee. Lakini
ikieleweka vizuri Salamu Maria yenyewe inaonyesha wazi kwamba sifa hiyo ya
Kimaria haipingani na sifa ya Rozari kuwa sala ya Kikristo, bali inaisisitiza na
kuikuza. Kwa kuwa sehemu ya kwanza ya Salamu Maria, inayotokana na maneno ambayo
Maria aliambiwa na malaika Gabrieli na mtakatifu Elizabeti, ni kuzama kwa ibada
katika fumbo lililofanyika katika Bikira wa Nazareti. Tunaweza kusema yanatokeza
mshangao wa mbingu na dunia na kwa namna fulani yanadokeza furaha ya Mungu
mwenyewe akitazama uzuri wa kazi yake bora kuliko zote – umwilisho wa Mwana
katika tumbo la kibikira la Maria -, kufuatana na mtazamo mfurahivu wa kitabu
cha Mwanzo (taz. Mwa 1:31), na ile aina ya ono asili au «pathos
ambayo Mungu, mwanzoni mwa uumbaji, aliitazama kazi ya mikono yake». Katika
Rozari, kukariri Salamu Maria kunatushirikisha furaha hiyo ya Mungu: ni shangwe,
ni mshangao, ni uvumbuzi wa muujiza mkubwa kuliko yote iliyofanyika katika
historia. Ndivyo unavyotimia utabiri wa Maria: «Tokea sasa vizazi vyote
wataniita mbarikiwa» (Lk 1:48).
Kiini
cha Salamu Maria, na kama bawaba kati ya sehemu yake ya kwanza na ya pili, ni
jina la Yesu. Pengine, katika kukariri harakaharaka, kiini hicho kinasahauliwa
pamoja na uhusiano wake na fumbo la Kristo linalokaziwa macho. Lakini mkazo juu
ya jina la Yesu na juu ya fumbo lake ndio unaobainisha matumizi ya Rozari yenye
maana na ya kuzaa matunda. Paulo VI katika himizo la kitume Marialis
Cultus alikumbusha tayari desturi inayofuatwa sehemu fulanifulani ili kutia
maanani jina la Kristo, yaani kuliongezea maneno yanayodokeza fumbo
linalotafakariwa. Ni desturi inayostahili sifa, hasa katika sala ya pamoja.
Inatokeza kwa nguvu imani katika Kristo ikiihusisha na nafasi mbalimbali za
maisha ya Mkombozi. Ni ungamo la imani na, kwa wakati huohuo, inasaidia
kudumisha uzingatifu wa tafakuri, ikiwezesha kulishiza fumbo la Kristo kadiri ya
lengo la kukariri Salamu Maria. Kukariri jina la Yesu – jina pekee ambalo
linatunawezesha kutumaini wokovu (taz. Mdo 4:12) – pamoja na lile la Mama yake
mtakatifu sana, na kama kwa kuacha Maria awe ndiye anayelipendekeza kwetu, ni
safari ya kulishiza inayolenga kutuingiza kwa dhati zaidi na zaidi katika maisha
ya Kristo.
Kutokana
na fungamano lake la pekee kabisa na Kristo, linalomfanya Maria awe Mama wa
Mungu, Theotokos, inapata nguvu ile
dua ambayo tunamuelekea katika sehemu ya pili ya sala, tukiyakabidhi maombezi
yake ya kimama maisha yetu na saa ya kufa
kwetu.
«Atukuzwe»
34.
Kuutukuza Utatu ndio lengo la sala hasa ya Kikristo. Kwa kuwa Kristo ndiye njia
inayotufikisha kwa Baba katika Roho. Tukiifuata mpaka mwisho tunajikuta
mfululizo mbele ya fumbo la nafsi tatu za Kimungu ambazo tuzisifu, tuziabudu na
kuzishukuru. Ni muhimu kwamba Atukuzwe, kilele cha kuzama katika mafumbo, iwekwe
mahali pa pekee katika Rozari. Katika sala ya hadhara inaweza kuimbwa ili
kusisitiza kwa namna ya kufaa mtazamo huo wa msingi ulio maalumu wa kila sala ya
Kikristo.
Kadiri
tafakuri juu ya fumbo ilivyokuwa zingatifu, ya dhati na kuhuishwa na upendo kwa
Kristo na kwa Maria – Salamu baada ya Salamu – basi kuutukuza Utatu mwishoni
mwa makumi, badala ya kuwa hatima fupi tu, kunapata tuni yake halisi ya kuzama
katika fumbo, kama kwa kuinua roho hadi juu mbinguni na kutufanya kwa namna
fulani tupate sisi pia mang’amuzi ya Tabori, utangulizi wa kuzama kesho katika
fumbo: «Ni vizuri sisi kuwapo hapa» (Lk 9:33).
Sala ya mwisho
35.
Katika kawaida ya Rozari, baada ya kuutukuza Utatu inafuata antifona iliyo
tofauti kadiri ya desturi. Bila ya kupunguza thamani ya maombi hayo, inafaa
tuseme kuwa kuzama katika mafumbo kunaweza kutokeza vizuri zaidi uwezo wake wa
kuzaa matunda kukiwa na mbinu ya kumalizia kila fumbo kwa sala ambayo ilenge
kupata matunda maalumu ya tafakuri ya fumbo husika. Hivyo Rozari itaweza
kutokeza kwa nguvu zaidi uhusiano wake na maisha ya Kikristo. Kufanya hivyo
kunapendekezwa na sala nzuri ya liturujia inayotualika kuomba kwamba kwa
kutafakari mafumbo ya Rozari, tuweze «kuiga yaliyomo na kupata yanayoahidi».
Hiyo
sala ya mwisho inaweza kufuata namna tofauti halali, kama inavyotokea tayari.
Hivyo Rozari inapata pia sura ya kulingana zaidi na mapokeo mbalimbali ya Kiroho
na jumuia mbalimbali za Kikristo. Katika mtazamo huo, inatarajiwa kwamba yaenee
kadiri ya busara ya kichungaji mapendekezo ya maana zaidi, afadhali kisha
kujaribiwa katika vituo na patakatifu pa Maria ambapo sala ya Rozari
inazingatiwa zaidi, hivi kwamba Taifa la Mungu liweze kufaidika na utajiri
wowote halisi wa Kiroho, likiufanya uwe lishe kwa sala yake hasa.
Tasbihi
36.
Chombo cha mapokeo cha kusalia Rozari ni tasbihi. Katika matumizi ya kijuujuu
zaidi inaishia mara nyingi kuwa kifaa tu cha kuhesabia Salamu Maria
zinazofuatana. Lakini inafaa pia kutokeza ishara inayoweza kuchangia tena kuzama
katika mafumbo. Kuhusu jambo hilo, neno la kwanza la kusema ni kuwa tasbihi
inamuelekea Msulubiwa, ambaye kwa namna hiyo anafungua na kufunga njia yenyewe
ya sala. Maisha na sala ya waamini kiini chake ni Kristo. Yote yanatoka kwake,
yote yamamlenga yeye, yote kwa njia yake, katika Roho Mtakatifu, yanamfikia Baba.
Kama
chombo che kuhesabia, kinachoonyesha maendeleo ya sala, tasbihi inadokeza safari
isiyokwisha ya sala hasa na ya ukamilifu wa Kikristo. Mwenye heri Bartolo Longo
aliiona pia kama ‘mnyororo’ inayotuunganisha na Mungu. Naam, mnyororo,
lakini mtamu; ndivyo unavyojidhihirisha daima uhusiano na Mungu aliye Baba.
Mnyororo ‘wa kitoto’, unaotulinganisha na Maria, «mjakazi wa Bwana» (Lk
1:38), na, kimsingi zaidi, na Kristo mwenyewe ambaye, ingawa ni Mungu,
alijifanya «mtumishi» kwa kutupenda. (Fil 2:7).
Ni
vizuri pia kueneza maana ya kiishara ya tasbihi upande wa mafungamano kati yetu
wenyewe, tukikumbuka kwa njia yake uhusiano wa ushirika na udugu unaotuunganisha
wote na Kristo.
Mwanzo na mwisho
37.
Kwa sasa katika mazingira tofauti ya Kanisa kuna namna mbalimbali za kuanza
Rozari. Katika maeneo kadhaa kawaida ni kuanza na dua ya Zaburi 70: «Ee Mungu,
uniokoe, Ee Bwana, unisaidie hima», kama kwa kuchochea ndani ya anayesali
hakika nyenyekevu ya unyonge wake; kumbe pengine mwanzo unafanyika kwa kutamka
maneno ya Nasadiki, kama kwa kuweka ungamo la imani kuwa msingi wa safari ya
sala inayoanza. Namna hizo na nyinginezo ni halali vilevile kadiri zinavyoandaa
roho kuzama katika mafumbo. Halafu sala inafungwa na ombi kwa ajili ya nia za
Baba Mtakatifu, ili kupanua mtazamo wa anayesali hadi upeo mkubwa wa mahitaji ya
Kanisa. Ni kwa ajili ya kuhamasisha mtazamo huo wa Kikanisa wa Rozari, kwamba
Kanisa limeamua kuitajirisha kwa rehema takatifu kwa manufaa ya anayeisali kwa
misimamo yanayotakiwa.
Kwa
kweli, Rozari ikisaliwa hivyo inakuwa kwa hakika safari ya Kiroho ambamo Maria
anajifanya Mama, mwalimu, kiongozi na kumtegemeza mwamini kwa maombezi yake ya
nguvu. Haiwezekani kushangaa kwamba roho, mwishoni mwa sala hiyo, ambapo
imeng’amua kwa dhati umama wa Maria, inajisikia haja ya kumsifu Bikira
mtakatifu kwa sala nzuri ajabu ya Salamu Malkia na kwa Litania ya Loreto. Ni
kilele cha safari ya ndani iliyomleta mwamini karibu sana na fumbo la Kristo na
la Mama yake mtakatifu sana.
Mgawanyo
katika siku za wiki
38. Rozari inaweza kusaliwa nzima kila
siku, na wapo ambao wanafanya hivyo na kustahili sifa. Hivyo inakuja kujaza kwa
sala siku za waaamini wengi waliojitosa kusali tu, au inakuja kuongozana na
wagonjwa na wazee ambao wana muda mwingi usio na shughuli. Lakini ni wazi kwamba
– hasa ukiongezwa mfululizo mpya wa mysteria
lucis – wengi hawataweza kusali zaidi ya sehemu moja, kadiri ya mpangilio
fulani katika wiki. Mgawanyo huo katika juma unazipatia siku za wiki ‘rangi’
fulani ya Kiroho, kidogo kama liturujia inavyofanya na vipindi mbalimbali vya
mwaka wa Kanisa.
Kadiri
ya desturi ya sasa, Jumatatu na Alhamisi zinatumika kutafakari «mafumbo ya
furaha», Jumanne na Ijumaa «mafumbo ya uchungu», halafu Jumatano, Jumamosi na
Jumapili «mafumbo ya utukufu». Tuingize wapi «mafumbo ya mwanga»?
Tukizingatia kwamba mafumbo ya utukufu yanapendekezwa mfululizo Jumamosi na
Jumapili, na kwamba kimapokeo Jumamosi ni siku ya Maria hasa, inafaa kushauri
kuhamishia Jumamosi tafakuri ya pili ya wiki juu ya mafumbo ya furaha, ambamo
uwepo wa Maria unajitokeza. Hivyo Alhamisi inabaki na nafasi kwa kutafakari
mafumbo ya mwanga.
Hata
hivyo elekezo hilo halikusudii kuzuia uhuru wa kufaa katika kutafakari kwa mtu
mmojammoja au kijumuia, kadiri ya mahitaji ya Kiroho na ya kichungaji na hasa
kadiri ya kutukia siku za liturujia ambazo zinaweza zikashauri kurekebisha
mpangilio huo kwa namna ya kufaa. Kilicho muhimu kweli ni kwamba Rozari itazamwe
na kung’amuliwa zaidi na zaidi kama safari ya kuzama katika mafumbo. Kwa njia
yake na kwa kukamilishana na kazi ya liturujia, juma la Mkristo linalotegemea
Siku ya Bwana, siku ya ufufuko, linakuwa safari kupitia mafumbo ya maisha ya
Kristo, naye anajitokeza katika maisha ya wanafunzi wake kuwa ndiye Bwana wa
nyakati na wa historia.
HATIMA
«Rozari
mbarikiwa wa Maria, mnyororo mtamu unaotuunganisha na Mungu»
39.
Tuliyoyasema mpaka sasa yanatokeza sana utajiri wa sala hiyo ya kimapokeo ambayo
ina usahili wa sala ya watu wadogo, lakini pia udhati wa kiteolojia wa sala
inayowafaa wanaojisikia haja ya sala iliyokomaa zaidi.
Daima
Kanisa limekiri kwamba sala hiyo ina nguvu ya pekee, likiyakabidhi matumizi yake
ya pamoja na ya kudumu mambo magumu zaidi. Wakati ambapo Ukristo wenyewe ulikuwa
hatarini, Kanisa liliona kwamba nguvu ya sala hiyo ndiyo iliyoepusha janga, na
Bikira wa Rozari alisalimiwa kama mwombezi wa wokovu huo.
Leo
naikabidhi kwa radhi nguvu ya sala hiyo – kama nilivyodokeza mwanzoni –
kipeo cha amani duniani na kile cha familia.
Amani
40.
Matatizo yanayojitokeza katika upeo wa ulimwengu mwanzoni mwa milenia mpya
yanatufanya tufikirie kwamba kazi kutoka Juu tu, yenye uwezo wa kuelekeza mioyo
ya wanaoishi katika nafasi za kushindana na ya wanaoshika mikononi mwao kesho ya
mataifa, inaweza kutumainisha kwamba kesho hiyo haitakuwa na magiza makubwa kama
ya sasa.
Rozari
ni sala ambayo kwa maumbile yake inalenga amani, kwa sababu ni kumkazia macho
Kristo, Mfalme wa amani na «amani yetu» (Ef 2:14). Anayelifanya fumbo la
Kristo kuwa lake pia – na ndilo lengo hasa la Rozari -, anajifunza siri ya
amani na kuigeuza kuwa mpango wa maisha. Tena, kutokana na tabia yake kama
tafakuri, pamoja na mfuatano wake mtulivu wa Salamu Maria, Rozari inamtuliza
anayesali na kumuandaa kupokea na kung’amua ndani kabisa mwa nafsi yake,
halafu kueneza kandokando yake, ile amani halisi ambayo ni zawadi maalumu ya
Mfufuka (taz. Yoh 14:27; 20:21).
Pia
ni sala ya amani kutokana na matunda ya upendo inayoyazaa. Ikisaliwa vizuri kama
tafakuri halisi, Rozari, kwa kurahisisha mkutano na Kristo katika mafumbo yake,
inatambulisha pia uso wa Kristo katika ndugu, hasa wanaoteseka zaidi.
Inawezekanaje kulikazia macho, katika mafumbo ya furaha, fumbo la Mtoto
aliyezaliwa Bethlehemu bila ya kujisikia hamu ya kupokea, kutetea na kustawisha
uhai, kwa kubeba mateso ya watoto sehemu zote za dunia? Inawezekanaje kufuata
nyayo za Kristo mfunuaji wa ukweli, katika mafumbo ya mwanga, bila ya kuazimu
kutoa ushahidi wa Heri zake katika maisha ya kila siku? Tena inawezekanaje
kumkazia macho Kristo aliyelemewa na msalaba na kusulubiwa, bila ya kujisikia
haja ya kumsaidia kama «Wakirene» wake katika kila ndugu aliyevunjwa na
uchungu au kulemewa na hali ya kukata tamaa? Hatimaye, inawezekanaje kuukazia
macho utukufu wa Kristo mfufuka na wa Maria aliyetawazwa Malkia, bila ya
kujisikia hamu ya kufanya ulimwengu huu uwe mzuri zaidi, wenye haki zaidi na
kulingana zaidi na mpango wa Mungu?
Basi,
Rozari huku ikitufanya tumkazie macho Kristo, inatufanya pia wajenzi wa amani
duniani. Kwa sifa yake ya kuwa dua inayosisitizwa na ya pamoja, kulingana na
mwaliko wa Kristo wa kusali «sikuzote» bila ya kukata tamaa (Lk 18:1),
inatuwezesha kutumaini kwamba, leo pia 'pambano' gumu kama lile la amani
linaweza kupata ushindi. Mbali na kukimbia matatizo ya ulimwengu, Rozari
inatusukuma hivyo kuyatazama kwa macho ya uwajibikaji na ya ukarimu, na
inatupatia nguvu ya kuyakabili tukiwa na hakika ya kupata msaada wa Mungu na nia
imara ya kuushuhudia katika nafasi yoyote «upendo, ndio kifungo cha ukamilifu»
(Col 3:14).
Familia:
wazazi
41.
Rozari, pamoja na kuwa sala kwa ajili ya amani, tangu mwanzo ni pia sala ya
familia na kwa ajili ya familia. Zamani sala hiyo ilipendwa sana na familia za
Kikristo, na bila ya shaka ilichangia umoja wake. Ni lazima tusitapanye urithi
huo wa thamani. Ni lazima turudi kusali katika familia na kusali kwa ajili ya
familia, kwa kutumia tena namna hii ya kusali.
Ikiwa
katika barua ya kitume Novo Millennio
Ineunte nilihimiza Liturujia ya Vipindi liadhimishwe na walei pia katika
maisha ya kawaida ya jumuia za parokia na za vyama mbalimbali vya Kikristo,
nataka kufanya vilevile kuhusu Rozari. Ni njia mbili za sala hasa ya Kikristo,
si za kuchagua kati yake, bali za kukamilishana. Hivyo naomba wanaoshughulikia
uchungaji wa familia wahamasishe kwa moyo sala ya Rozari.
Familia
inayosali kwa umoja, inadumu kuwa na umoja. Kwa mapokeo ya muda mrefu, Rozari
takatifu inafaa kwa namna ya pekee kuwa sala inayokusanya familia. Wanafamilia,
kwa kumkazia macho Yesu, wanajipatia upya uwezo wa kutazamana daima usoni ili
kuelewana, ili kushikamana, ili kusameheana, ili kuanza upya kwa agano la upendo
lililofanywa upya na Roho wa Mungu.
Matatizo
mengi ya familia za kisasa, hasa katika jamii zilizoendelea kiuchumi, yanatokana
na kwamba inazidi kuwa vigumu kushirikishana. Kukaa pamoja kunashindikana, na
huenda nafasi chache za kukaa pamoja zikajazwa na picha za televisheni. Kuanza
upya kusali Rozari katika familia ni kuingiza katika maisha ya kila siku picha
tofauti sana, zile za fumbo linalookoa: picha ya Mkombozi, picha ya Mama yake
mtakatifu sana. Familia ambayo inasali pamoja Rozari inaiga kidogo mazingira ya
nyumba ya Nazareti: Yesu anawekwa katikati, kwa kushiriki pamoja naye furaha na
uchungu, kwa kumkabidhi mikononi mahitaji na matarajio, kwa kuchota kwake
tumaini na nguvu ya kuendelea na safari.
...
na watoto
42.
Ni pia jambo zuri na la kufaa kuikabidhi sala hiyo safari ya kukua kwa watoto.
Je, Rozari si safari ya maisha ya Kristo, tangu kutungwa mpaka kufa, hadi
kufufuka na utukufu? Leo inazidi kuwa vigumu kwa wazazi kuwafuata watoto katika
hatua mbalimbali za maisha. Katika jamii ya teknolojia iliyostawi, ya vyombo vya
upashanaji habari na ya utandawazi, yote yamekuwa yanakwenda haraka sana, na
umbali wa kiutamaduni kati ya vizazi unazidi kukua. Mapema aina yoyote ya ujumbe
na mang’amuzi yasiyotarajiwa yanapata nafasi katika maisha ya watoto na vijana,
hivi kwamba pengine wazazi wanafadhaika kuwaepusha na hatari wanazokabiliana
nazo. Si kwa nadra wanapatwa na hali ya kuvunjika moyo kabisa, wakiona wanao
walivyoshindwa na udanganyifu wa dawa za kulevya, na mivuto ya anasa isiyo na
mipaka, na vishawishi vya ukatili, na aina mbalimbali za matendo yanayotokeza
mtu asivyoona maana ya maisha na alivyokata tamaa.
Kusali
Rozari kwa ajili ya watoto, tena afadhali pamoja na watoto, kwa kuwalea tangu
utotoni kuwa na nafasi hiyo ya «kutulia kwa sala» kifamilia kila siku, bila ya
shaka si utatuzi wa matatizo yote, lakini ni msaada wa Kiroho wa thamani.
Inawezekana kupinga kwa kusema Rozari inaonekana ni sala isiyofaa kuwaridhisha
watoto na vijana wa leo. Lakini pengine hoja hiyo inategemea namna ya kusali
ambayo mara nyingi si sahihi. Zaidi ya hayo, bila ya kupotosha muundo wake wa
msingi, hakuna kinachozuia kwamba kwa watoto na vijana– katika familia kama
vile katika vikundi - sala ya Rozari isitajirishwe na ishara na vitendo vya
kufaa, ambavyo visaidie kuielewa na kufaidika nayo. Kwa nini tusijaribu? Kwa
msaada wa Mungu, uchungaji wa vijana usiokata tamaa bali wenye bidii na ubunifu
unaweza kufanya mambo ya maana kweli. Siku za Kimataifa za Vijana zimenionyesha
kiasi gani! Rozari ikipendekezwa vizuri, nina hakika kuwa vijana wenyewe
wataweza kuwashangaza tena wazee kwa kuifanya sala hiyo kuwa ya kwao na kuitumia
kwa umotomoto maalumu wa umri wao.
Rozari, hazina ambayo tuivumbue upya
43.
Wapendwa ndugu wa kiume na wa kike! Sala rahisi hivi, na kwa wakati huohuo
tajiri hivi, inastahili kweli kuvumbuliwa tena na jumuia ya Kikristo. Tufanye
hivyo hasa mwaka huu, tukipokea pendekezo hilo kama uimarishaji wa mpango
uliochorwa katika barua ya kitume Novo
Millennio Ineunte, ambayo programu za kichungaji za Makanisa maalumu mengi
zimeifuata katika kupanga juhudi kwa miaka ya jirani.
Kwa
namna ya pekee nawaelekea nyinyi, wapendwa ndugu katika uaskofu, mapadri na
mashemasi, nanyi watenda kazi wa kichungaji katika huduma mbalimbali, ili kwa
kung’amua wenyewe uzuri wa Rozari, muihamasishe kwa bidii.
Nawategemea nyinyi pia wanateolojia,
ili kwa masomo yenu makini na ya hekima kwa wakati mmoja, yenye mzizi katika
Neno la Mungu na usikivu kwa maisha halisi ya taifa la Wakristo, mtokeze misingi
ya Kibiblia, utajiri wa Kiroho na nguvu ya kichungaji ya sala hiyo ya kimapokeo.
Nawategemea
nyinyi, wanaume na wanawake mliowekwa wakfu, ambao mnaitwa kwa namna ya pekee
kuukazia macho uso wa Kristo mkijifunza kwa Maria.
Nawaangalia
nyinyi nyote, ndugu wa kiume na wa kike wa hali yoyote ya maisha, nyinyi,
familia za Kikristo, nanyi wagonjwa na wazee, nanyi vijana: mshike upya mikononi
kwa tumaini tasbihi ya Rozari, mkiivumbua upya katika mwanga wa Maandiko
matakatifu, kulingana na liturujia, katika hali halisi ya maisha ya kila siku.
Mwaliko
wangu huu usipotee bure! Mwanzoni mwa mwaka wa ishirini na tano wa upapa wangu,
nakabidhi barua hii ya kitume mikononi mwa Bikira Maria mwenye hekima,
nikisujudu Kiroho mbele ya picha yake iliyopo katika patakatifu pazuri ajabu
ambapo mwenye heri Bartolo Longo, mtume wa Rozari, alipajenga kwa heshima yake.
Najitwalia kwa radhi maneno yake ya kusisimua ambayo alifunga Dua maarufu kwa
Malkia wa Rozari takatifu: «Rozari mbarikiwa wa Maria, mnyororo mtamu
unaotuunganisha na Mungu, kiungo cha upendo kinachotuunganisha na Malaika, mnara
wa wokovu dhidi ya mashambulizi ya toka motoni, bandari salama katika dhoruba
iliyotupata sote, sisi hatutakuacha tena kamwe. Wewe utatufariji saa ya kufa.
Kwako tutatoa busu la mwisho uhai utakapozimika. Na sauti ya mwisho ya midomo
yetu itakuwa jina lako tamu, Malkia wa Rozari wa Pompei, Mama yetu mpendwa,
kimbilio la wakosefu, Mtawala mfariji wa wenye huzuni. Uhimidiwe popote, leo na
daima, duniani na mbinguni».
Kutoka
Vatikano, tarehe 16 Oktoba mwaka 2002, mwanzo wa mwaka wa ishirini na tano wa
Upapa wangu.
No comments:
Post a Comment