Monday, February 1, 2016

Baraza la Makanisa Ulimwenguni na UN kushirikiana kutoa huduma kwa wahamiaji
Katika mkutano wa ngazi ya juu kati ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni na Umoja wa Mataifa uliofanyika hivi karibuni, huko Geneva, Uswiss, kwa pamoja viongozi wakuu wa taasisi hizi mbili za Kimataifa wamekubaliana kimsingi kwamba, kuna haja ya kuratibu kwa umakini mkubwa suala la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi ya maisha na usalama Barani Ulaya, ili kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji zaidi ya millioni sitini walioenea sehemu mbali mbali za dunia.
Katika Tamko la pamoja, viongozi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni na Umoja wa Mataifa wamekubaliana kimsingi kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuzama zaidi katika mchakato wa kutafuta suluhu ya kudumu kwa changamoto na matatizo yanayoendelea kuzalisha makundi makubwa makubwa ya wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Suluhu inayojikita katika utashi wa kisiasa ili kupata ufumbuzi wa mgogoro wa kivita huko Mashariki ya Kati, hususan nchini Syria ni muhimu sana katika kukabiliana na wimbi na wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria.
Ukosefu wa misingi ya haki, amani, usawa, ustawi na maridhiano kati ya watu ni sababu kubwa inayoendelea kuzalisha wakimbizi na wahamiaji katika miaka ya hivi karibuni. Jumuiya ya Ulaya kwa upande wake, inapaswa kuibua sera na mikakati makini ya kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi Barani Ulaya, kuliko walikotoka. Haki msingi za wakimbizi na wahamiaji hazina budi kulindwa na kuendelezwa.
Unyanyasaji wa kijinsia udhibitiwe ili kulinda utu na heshima ya wakimbizi. Watoto wa wakimbizi na wahamiaji wapatiwe elimu itakayowawezesha kwa siku za usoni kupambana na mazingira ili hatimaye, kupata maisha bora zaidi. Huduma hizi hazina budi kwenda sanjari na huduma ya afya na chakula bora. Mchakato wa kuwapatia hifadhi wakimbizi wa kisiasa hauna budi kuzingatia misingi ya haki na usawa pasi na upendeleo au ubaguzi ambao umejionesha katika baadhi ya nchi za Jumuiya ya Ulaya.
Kuna baadhi ya watu wametengwa na kubaguliwa kutokana na utaifa, kabila na mahali wanapotoka baadhi ya wakimbizi na wahamiaji kwa hofu ya mashambulizi ya kigaidi. Wadau mbali mbali wanapaswa kushirikiana kikamilifu ili kukabiliana na tatizo la ubaguzi wa rangi na hofu isiyokuwa na msingi. Viongozi wakuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, katika tamko lao la pamoja wamekazia pamoja na mambo mengine, umuhimu wa kuwashirikisha wakimbizi na wahamiaji katika maisha ya nchi husika, sanjari na kusikiliza sauti za wakimbizi na wahamiaji, ili kutekeleza sera na mikakati ya huduma kwa muda uliopangwa.
Wadau na mashirika mbali mbali yanayotoa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji yanapaswa kushirikiana na Serikali husika katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji. Ili kupembua kwa kina na mapana: mafanikio na changamoto zilizopo, viongozi wakuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni na Mashirika ya Umoja wa Mataifa, wameamua kufanya mikutano ya pamoja kila baada ya miezi mitatu, ili kupanga na hatimaye, kutekeleza sera na mikakati kwa ajili ya huduma bora zaidi kwa wakimbizi na wahamiaji Barani Ulaya.
.Habari kwa hisani ya  Radio Vatican.

Shuhudieni utajiri unaofumbatwa katika Ekaristi Takatifu!Askofu Cletus Chandrasiri Perera, mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Sri Lanka anasema, maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa Jimbo kuu la Cebu, Ufilippini ni fursa ya kuadhimisha, kuabudu, kutafakari na kuzama katika katekesi za kina zinazotolewa wakati huu wa kongamano, ili kuwawezesha waamini kuonja na hatimaye, kushuhudia utajiri mkubwa unaofumbatwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Waamini wanapaswa kutambua umuhimu wa Fumbo la Ekaristi katika maisha yao, tayari kulipatia kipaumbele cha kwanza katika maisha yao ya kila siku, ili kuweza kuipokea na kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao, ili kushuhudia huruma, upendo na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Wakati huu, Kanisa Katoliki linaungana kwa pamoja kusali, kutafakari na kumwabudu Yesu Kristo ambaye daima yuko kati kati ya watu wake kwa njia ya Neno na Sakramenti, lakini zaidi kwa njia ya maskini, ambao kimsingi ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu.
Maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu kimataifa yanajikita katika Ibada ya Misa takatifu,Sala, Katekesi, Tafakari, Ibada ya Kuabudu na Maandamano la Ekaristi Takatifu ushuhuda wa imani ya Kanisa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo kati ya waja wake pamoja na mikutano mbali mbali ya kiimani. Inafurahisha kuona kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia maadhimisho ya Kongamano hili yafanyike nchini Ufilippini, nchi ambayo ina idadi kubwa ya waamini wa Kanisa Katoliki, watu ambao wako moto moto katika ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, ikilinganishwa na nchi nyingine kutoka Barani Asia.
Maadhimisho haya ni mkusanyiko wa waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaoshuhudia umoja na utofauti wao katika imani na upendo. Wote hawa wanaungana kwa pamoja ili kumwomba Kristo Yesu awaongoze na kuwaimarisha katika imani inayoshuhudiwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ekaristi takatifu ni kiini na hitimisho la maisha na utume wa Kanisa, kama ambavyo wanakaza kusema Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Maadhimisho haya ni wakati muafaka kwa Wakristo kutoka Sri Lanka waliohamia nchini Ufilippini kuweza kukutana na kusali kwa pamoja, ili kushuhudia imani yao katika Fumbo la Ekaristi Takatifu anasema Askofu Cletus Chadrasiri Perera, mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Sri Lanka kwenye maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa linaloendelea huko Jimbo kuu la Cebu, Ufilippini.

Habari kwa hisani ya Radio Vaticani


UTATU MTAKATIFU