NANI MWABUDU SANAMU ?

NANI MWABUDU SANAMU ?


SWALA LA SANAMU
 
Kati ya maswala yanayowakera sana wenzetu Waislamu, na hata baadhi ya Wakristo wa madhehebu mbalimbali, mojawapo ni lile la sanamu na picha takatifu zinazotumiwa na Wakatoliki na Wakristo wengine toka karne za kwanza za Kanisa. Tunawapa pole kwa kero hizo, lakini wasiwe na wasiwasi: hatumlazimishi mtu yeyote afanye hivyo. Lakini upande wetu tunawaomba wasituhukumu harakaharaka wakisema, eti, tunaabudu sanamu; sisi tunajua sababu tulizonazo za kutumia vitu hivyo bila ya kuviabudu, na tuna hakika ya kumpendeza Mwenyezi Mungu. Ukipenda, nitakueleza kidogo kuhusu jambo hilo, ingawa si la kwanza katika dini yetu. Yaliyo muhimu kwetu ni imani kwa Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, halafu tumaini na upendo kwake na kwa jirani yeyote.
Tukizungumzia sanamu ni kwa sababu tunashambuliwa sana kuhusu jambo hilo, ambalo wengi wanaliona kuwa ni thibitisho kuwa, eti, Kanisa Katoliki limepotoka kabisa; hivyo, eti, ni lazima kuliacha na kufuata dini au madhehebu tofauti. Kumbe kuliasi hilo Kanisa pekee la Yesu Kristo ni kupotea kabisa kwa kutoroka kundi lake na wachungaji aliowakabidhi kondoo zake.
Toka mwanzo wa maelezo yetu haya tunatamka juu ya imani yetu yale aliyoyasema mtume Paulo alipolaumiwa kwa kula nyama iliyotolewa kwanza sadaka kwa miungu ya bandia; jibu lake na letu ni hili, “Kwa habari ya kuvila vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; twajua ya kuwa sanamu si kitu katika ulimwengu, na ya kuwa hakuna Mungu ila mmoja tu” (1Kor. 8:4). Tunawaomba wote wapokee tamko letu hilo; sisi sio wajinga kiasi hicho, hata tukamlinganisha Mungu pekee na kiumbe chake chochote, hasa kama tulikitengeneza wenyewe.
Wengi wanaotushambulia wanatumia Biblia, hasa kitabu cha Kutoka (20:3-6), tunaposoma: “Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia. Kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu: nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu”. Baada ya kusoma maneno hayo, watu hao wanaanza kusisitiza: “ Umesikia? Hilo ni neno la Mungu! Nyinyi Wakatoliki mmepotoka kabisa! Mapadri wenu wanawadanganya”.
Kweli, mtu asiyejua Biblia na namna ya kuitumia anaweza akashtushwa sana na maneno hayo hata akadhani kwamba eti, Kanisa linapotosha watu. Lakini anayejua Biblia vizuri hawezi kamwe kuridhika na dondoo lake moja, kama kwamba lingekuwa neno pekee la Mungu kuhusu jambo fulani. Biblia imejaa maneno ya kila aina, na mengine yanaonekana kupingana yenyewe kwa yenyewe. Kanisa tu, ambalo ndilo “nguzo na msingi wa kweli” (1Tim. 3:15), linaweza kutueleza maneno ya Biblia yana maana gani, na kati ya hayo lipi ni muhimu zaidi kuhusu swala fulani, kwa mfano swala la sanamu.
 
 
KATAZO LA SANAMU LILIVYOTUNZWA CHINI YA SANAMU
 
Ni afadhali jue kwamba maneno hayo ya Kutoka pamoja na ya amri nyingine za Mungu yaliandikwa juu ya mbao mbili za mawe ambazo ziliitwa Ushuhuda na kuwekwa ndani ya sanduku maalumu lililoitwa sanduku la Agano na lililofunikwa kwa dhahabu. Bila ya shaka hilo si ajabu. Lakini nadhani utashangaa kusoma katika kitabu hichohicho cha Kutoka (25:16-22) kwamba Mungu mwenyewe aliagiza zichongwe sanamu juu ya hilo sanduku la Agano: “Kisha tia ndani ya sanduku huo Ushuhuda nitakaokupa. Nawe fanya kiti cha rehema cha dhahabu safi; urefu wake utakuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu. Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu: uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili. Fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku. Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema. Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku; kisha utie huo Ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku. Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la Ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli”.
Ukiwa umesikiliza vizuri, ni kwamba hilo katazo la sanamu lilitunzwa chini ya sanamu mbili zilizoagizwa na Mungu mwenyewe! Tena, ni kwamba Mwenyezi Mungu aliahidi kuwa ndipo atakapowatokea Waisraeli na kuzidi kusema nao. Ndiyo sababu kwa Waisraeli kiti hicho kati ya makerubi kilikuwa mahali patakatifu kuliko popote duniani. Kumbe hayo makerubi yalikuwa miungu ya makabila ya jirani, hasa ya Babeli, huko Iraq! Lakini aliyeagiza hayo makerubi yachongwe ni Mwenyezi Mungu, si binadamu. Hivyo ni dhahiri kuwa katazo la sanamu si la moja kwa moja, la sivyo Mungu angekuwa anajipinga kwa kuamuru kitu alichokikataza. Lakini sisi sote tunajua Mwenyezi Mungu hawezi kamwe akajipinga. Kwa hiyo katazo la sanamu alilotoa, maana yake ni hiyo inayofundishwa na Kanisa Katoliki.
Zaidi ya makerubi hayo yaliyochongwa juu ya sanduku la agano, mengine mengi yalikuwemo mwenye mapazia ya hekalu, kutokana na agizo la Mungu: “Kisha fanya hiyo Maskani iwe na mapazia kumi: ifanye ya nguo ya kitani nzuri ya kusokota, pamoja na nyuzi za rangi ya samawi, na ya zambarau, na nyekundu, pamoja na makerubi; kazi ya fundi stadi…”(Kut. 26:1-31).
Kutokana na agizo hilo, Bezaleli “akafanya kiti cha rehema cha dhahabu safi: urefu wake ulikuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake ulikuwa dhiraa moja na nusu. Kisha akafanya makerubi mawili ya dhahabu: akayafanya ya kazi ya kufua, yawe katika miisho miwili ya kiti cha rehema; kerubi moja mwisho huu, na kerubi moja mwisho huu; alifanya hayo makerubi mawili ya kitu kimoja na hicho kiti cha rehema katika miisho yake miwili. Na hayo makerubi yakanyosha mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zilikuwa zaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zilikuwa zikielekea kiti cha rehema” (Kut. 37:7-9).
Hapo baadaye Solomoni pia alipamba patakatifu pa patakatifu, yaani undani wa hekalu, kwa makerubi na mengineyo, tunavyosoma katika kitabu cha kwanza cha Wafalme (6:23-35): “Akafanya ndani ya chumba cha ndani makerubi mawili ya mzeituni, kwenda juu mikono kumi… Akayaweka hayo makerubi katika nyumba ya ndani; na mabawa ya makerubi yakanyoshwa… Akayafunika makerubi kwa dhahabu. Akazinakshi kuta zote za nyumba kwa nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, pande za ndani na nje… Akafanya milango miwili ya mzeituni; akanakshi juu yake nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, akaifunika kwa dhahabu; akatia dhahabu juu ya makerubi, na juu ya mitende. Ndivyo alivyoyafanyia maingilio ya hekalu miimo ya mzeituni… akanakshi juu yake makerubi…”.
Hivyo ni wazi kwamba tangu mwanzo katazo la sanamu halikuwa la moja kwa moja. Hata manabii waliopinga vikali ibada za sanamu za kipagani hawakusema lolote dhidi ya hayo makerubi na michoro ya kupamba hekalu la Mungu wa kweli.
 
 
KUABUDU MIUNGU KATIKA AGANO JIPYA
 
Sasa tuingie katika Agano Jipya. Injili haituletei neno lolote la Yesu dhidi ya sanamu. Kinyume chake, katika kueleza atakavyowaokoa watu, alijifananisha na sanamu ya nyoka ya shaba. Musa aliinua sanamu hiyo jangwani kwa ajili ya watu walioumwa na nyoka hai kusudi wakiitazama wapone tu; basi, Yesu alisema: “Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa, ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye” (Yoh. 3:l4-15).
Hata alipotaja amri za Mungu, Yesu hakuzitaja zile za kwanza zikiwa ni pamoja na katazo la sanamu, bali alianza na Usiue: “Wazijua amri: Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako” (Mk. 10:19). Ni kwamba mkazo wa Yesu ni mwingine, yaani amri kuu ya upendo. Mtume Paulo alieleza mkazo huo katika barua yake kwa Waroma (13:8-10): “Msiwiwe na mtu chochote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria. Maana kule kusema: Usizini, usiue, usiibe, usitamani, na ikiwapo amri nyingine yoyote, inajumlishwa katika neno hili, ya kwamba: Mpende jirani yako kama nafsi yako. Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria”.
Siku nyingine Yesu alionyeshwa pesa yenye picha na jina la mtawala, kama ilivyo desturi hata leo, akauliza, “Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii?” (Math. 22:20); akajibiwa kuwa ni ya mfalme Kaisari. Basi, Yesu alituangalisha tusiabudu sanamu za namna hiyo akisema, “Hamwezi kumtumikia Mungu na mali” (Lk. 16:13). Yaani mali zinaweza zikashika nafasi ya Mungu katika maisha yetu hata tukaziabudu. Unaweza ukamkuta mtu ambaye anapinga sana sanamu na picha takatifu, kumbe anatamani sana pesa! Kadiri ya Biblia huyo anaabudu sanamu, yaani pesa. Anajali twiga zake kuliko binadamu mwenzake anayeweza kuhitaji msaada.
Kwa msingi huo mtume Paulo alisema wazi kufanya hivyo ndio kuabudu sanamu: “Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati, wala mchafu, wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu” (Ef. 5:5). Ndiyo sababu alionya: “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi: uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu” (Kol. 3:5). Barua ya kwanza kwa Timotheo (6:9-10) inafafanua: “Hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na imani, na kujichoma kwa maumivu mengi”.
Kadiri ya mtume Paulo, wengine tena wanaabudu tumbo lao, tunavyosoma katika Wafilipi (3:19): “mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani”. Wataalamu wanaeleza kwa namna mbalimbali maana ya maneno hayo, wengine wakidai kuwa tumbo linamaanisha ulafi, wengine wanasema linamaanisha tamaa zote za mwili kama vile uzinzi, wengine tena wanaeleza kuwa maneno hayo ya mtume Paulo yanazidi kuwapinga wale waliosisitiza masharti ya Kiyahudi kuhusu vyakula, wakifanya maswala ya tumbo kuwa ndiyo dini. Kwa vyovyote ni kwamba watu hao walijali mno mambo ya mwili, hata kuliko Mungu mwenyewe. Bila ya shaka watu wa namna hiyo wapo leo pia. Kulaumu picha takatifu hakutawasaidia kitu. Afadhali waache kuabudu tumbo.
Mfano mwingine ni ule wa mtume Yohane ambaye mwishoni mwa maisha yake alisumbuliwa sana na baadhi ya wanafunzi wake ambao walileta matata na hatimaye mafarakano katika jumuia za Kikristo. Barua zote tatu alizoziandika zinakabili watu hao kwa ukali. Ya kwanza inamalizika kwa maneno yafuatayo: “Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu” (1Yoh. 5:21). Ukisoma barua nzima utatambua kwamba haizungumzii kamwe sanamu, ila mafundisho ya kizushi na utovu wa upendo katika jumuia. Kwa hiyo ni wazi kuwa maneno hayo ya mwisho hayalengi sanamu zenyewe, ila yanasisitiza yale yaliyotangulia (1Yoh. 5:20): “Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupatia akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli. Nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele”. Kwa sababu hiyo kupotosha ukweli wa imani hata kusambaratisha Kanisa ni sawa na kuasi kabisa dini ya Kikristo na kuabudu miungu mingine. Hata hilo ni la kuzingatiwa sana: unaweza ukamkuta mtu anapinga sana sanamu na picha takatifu, kumbe analeta mafarakano katika Kanisa akidai wengine wafuate msimamo wake! Mtu wa namna hiyo anayaamini maoni yake tu, hawezi kusikiliza wengine, wala hajali umoja wa Kanisa . Kadiri ya Biblia huyo anaabudu sanamu, yaani anajiabudu pamoja na akili yake. Anajali kiburi chake kuliko ustawi wa Mwili wa Kristo.
Kabla ya Yohane, Mtume Paulo alionya wanafunzi wake hasa wa Korintho kuhusu shida hiyohiyo: “Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja. Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu. Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu husema, ‘Mimi ni wa Paulo’, na, ‘Mimi ni wa Apolo’, na, ‘Mimi ni wa Kefa’, na, ‘Mimi ni wa Kristo’. Je, Kristo amegawanyika? Je, Paulo alisulubiwa kwa ajili yenu? Au je, mlibatizwa kwa jina la Paulo?” (1Kor. 1:10-13). Mwelekeo huo wa kujivunia mhubiri huyu au huyu unajitokeza siku hizi katika kusambaza picha zake katika kuwaalika watu wahudhurie mikutano ya Injili: pengine walewale wanaokataa picha za Yesu na za watakatifu wake wanaeneza kila mahali zile za mhubiri wanayempenda. Barua hiyo ya Paulo inaendelea kutuuliza: “Je, Paulo alisulubiwa kwa ajili yenu? Au je, mlibatizwa kwa jina la Paulo?”. Nasi tunajiuliza, Je, hao Wakristo wanajiona wameokolewa na mhubiri huyo hata wapendelee picha yake kuliko ya Yesu? Kuna msingi fulani wa kujiuliza hivyo, yaani kwamba mara nyingi hao wanajali mhubiri wao kuliko umoja wa Kanisa, lililo Mwili wa Kristo: “Je, Kristo amegawanyika?”. Si ajabu kwamba katika madhehebu hayo yanayopinga sanamu mafarakano hayana mwisho kamwe. Kila kikundi kinang’ang’ania misimamo ya fulani dhidi ya ile ya wengine wowote hata kusababisha farakano. Hiyo inaweza kutokea ingawa wahusika wanajidai kuwa hawamfuati Paulo wala Apolo wala Kefa, ila Kristo, wakisema, “Mimi ni wa Kristo”.
Hata upande wa siasa mtu anaweza akajikuta akiabudu miungu mingine. Hasa kitabu cha Ufunuo kinatuangalisha na ibada kwa mtawala wa nchi anayedai kushika nafasi ya Mungu na kutoa sheria kinyume cha Mungu. Yohane aliandika kitabu hicho akiwa uhamishoni katika kisiwa cha Patmos, kinachokabili nchi ambayo siku hizi inaitwa Uturuki. Zamani zake sehemu hiyo ilikuwa tu mkoa wa Dola la Roma. Ndio mkoa wa Asia ambapo ibada kwa mfalme mkuu wa Roma ilistawi mapema na kwa nguvu zaidi kuanzia kipindi cha utawala wa Augustus, ambaye chini yake Yesu alizaliwa. Katika Ufunuo sura ya 2 na ya 3 tunasoma barua saba kwa kanisa la Efeso, mji mkuu wa mkoa, na kwa makanisa ya miji sita ya kandokando. Miji hiyo yote, isipokuwa Thiatira, ilikuwa na mahekalu ya kumuabudia mfalme. Hasa huko Efeso mfalme Domitianus (aliyetawala miaka 81-96 B.K., yaani miaka hiyohiyo Ufunuo ulipoandikwa) alijijengea hekalu kubwa akidai kuabudiwa na raia zake. Vilevile alisimamisha sanamu zake katika sehemu zote za Dola la Roma. Kutokana na hali hiyo ya hatari kwa imani ya Wakristo wanaomwamini Mungu mmoja tu, na Bwana mmoja, Yesu Kristo, basi Yohane aliandika kitabu cha Ufunuo ili kuwahimiza waamini wapinge madai ya serikali ya kuwataka raia sio tu watii sheria halali, bali pia wawape viongozi wake heshima ile anayostahili Mungu tu. Vilevile Yohane aliwahimiza wapinge dini inayotetea ibada za namna hiyo. Hao ndio wanyama wale wawili wanaozungumziwa katika sura ya 13: yaani serikali ovu na dini inayoitetea.
Ingawa siku hizi hakuna mfalme wala rais anayedai kujengewa mahekalu ili aabudiwe, ni kishawishi cha watawala wengi kutaka kushika nafasi ya Mungu kwa kupanga wenyewe maadili ya wananchi, hata kuwalazimisha watende kinyume cha dhamiri na dini zao. Matokeo yake ni kwamba waamini wengi wanadhulumiwa, kuteswa na hata kuuawa. Vilevile ni kishawishi cha viongozi wengi wa dini kutetea watawala hata wanapotenda maovu. Viongozi hao wanaweza wakawadai waumini wao watii bila ya kujiuliza kama ni sawa au sivyo. Vilevile ni kishawishi cha wananchi wengi kufuata mkondo na hivyo kushika sheria za serikali hata zikipingana na zile za Mungu; na pia kuheshimu nchi yao kuliko inavyofaa, hata kudharau nchi nyingine; tena kuwaamini mno viongozi wao na vyama vyao hata kufumba macho mbele ya makosa wanayoyafanya. Hizo zote ni namna za kuabudu viumbe badala ya Mungu tu.
 
 
UJENZI WA MAKANISA NA MATUMIZI YA SANAMU
 
Tukirudia sanamu zenyewe, Agano Jipya halisemi kuwa Wakristo wa kwanza walizitumia, lakini hiyo si hoja, kwa sababu vilevile hawakuwa na mahali maalumu pa ibada. Hata hivyo siku hizi hakuna anayepinga ujenzi wa makanisa kwa ajili hiyo akitoa hoja ya kwamba Biblia haizungumzii mahali pa namna hiyo, bali inasema Mitume na wanafunzi wao walikuwa wakisali pamoja na Wayahudi katika hekalu pekee la Yerusalemu na katika masinagogi ya kila mji na kijiji, halafu walikutana kuadhimisha ekaristi katika nyumba za kawaida. Kwa mfano, Matendo ya Mitume (2:46) yanasema: “Sikuzote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe”.
Kumbe ukirudi nyuma, unakuta kwamba Wakristo waliopinga sanamu katika karne ya pili, kwa mfano Minucius Felix kule Afrika Kaskazini, waliweza kupinga pia ujenzi wa makanisa wakitumia maneno ya Yesu kwa mwanamke Msamaria (Yoh. 4:21): “Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu”. Walisahau kuwa Yesu alikuwa akihiji mara nyingi Yerusalemu hekaluni. Kama kawaida, hata katika swala hilo kutegemea mstari mmoja tu wa Biblia ni hatari kubwa ya kuipotosha yote.
Mmojawapo kati ya hao waliopinga majengo ya ibada kwa msingi huo ni Origenes. Huyohuyo anakumbukwa sana katika historia ya Kanisa kwa utaalamu wake wa Biblia, lakini pia kwa tendo alilofanya la kujihasi ili atimize namna yake neno la Yesu kuhusu matowashi, yaani wanaume wasioweza kuungana na wanawake: “Wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee” (Math. 19:12). Basi, huyo Origenes alijikata sehemu za siri ili kulipokea neno hilo alivyolielewa; ila baadaye akajilaumu. Hata hivyo, mpaka leo kuna watu wanaoendelea kusoma Biblia namna hiyo kwa kuzingatia dondoo hili au hili linavyoonekana mara moja, wakipuuzia mapokeo ya Kanisa, na hivyo wanaingia hasara kubwa.
Basi, upinzani wa watu hao tuliowataja na wa serikali pia haukufaulu kuzuia Wakristo wasiendelee kujenga na kupamba makanisa waliyoyahitaji. Kuanzia mwaka 205 tuna ushahidi wa maandishi kuhusu mahali pa namna hiyo. Ni vilevile kuhusu picha takatifu. Tunazikuta katika mahandaki ya Roma ambapo Wakristo mashujaa wa karne tatu za kwanza walikusanyika kwa ibada ili kukwepa askari wasiwakamate na kuwatesa. Humo tunakuta kwa mfano mchoro wa njiwa kwa maana ya Roho Mtakatifu, na wa mchungaji mwenye kubeba kondoo mabegani kwa maana ya Yesu Mchungaji Mwema. Matumizi ya picha yanashuhudiwa vilevile na kitabu cha mwaka 150 hivi kuhusu maisha ya mtume Yohane, na maandishi ya Tertullianus aliyeishi Afrika Kaskazini kwenye mwaka 200, halafu na historia ya Kanisa iliyoandikwa na Eusebius wa Caesarea mara baada ya uhuru wa dini kutangazwa na Dola la Roma (313). Wakristo wakaendelea kutumia hizo picha za Yesu na za watakatifu bila ya upinzani wowote mpaka Mohamed alipoanzisha Uislamu. Baada tu ya umma wake kuenea na kuja kutawala nchi mbalimbali za Kikristo, wakazuka Wakristo walioanza kuzionea aibu picha hizo kutokana na lawama na hoja za Waislamu. Ulikuwa mwaka 724 hivi; mara hata mfalme Leo III aliyetawala Dola la Roma la Mashariki akaanza kuzipinga na kuzikataza na kuziteketeza. Ndio mwanzo wa mabishano makali yaliyosababisha hata umwagaji damu hadi mwaka 843 ambapo Wakristo waliotetea picha takatifu walipata ushindi wa kudumu na kuruhusiwa na serikali.
 
 
 
 
MUNGU AMEONEKANA KWETU
 
Hapo katikati ulifanyika Mtaguso Mkuu wa Pili wa Nisea (787) ambapo maaskofu walichukua uamuzi wa moja kwa moja kuhusu swala hilo wakieleza sababu gani kuanzia Agano Jipya sanamu zinakubalika. Kwa kifupi ni kwamba Yesu sio tu Neno wa Baba bali ni pia sura yake: katika yeye Mungu ametutokea wazi, tofauti na ilivyokuwa katika Agano la Kale, ambapo Musa aliwaambia Waisraeli: “Bwana alisema nanyi kutoka kati ya moto; mkasikia sauti ya maneno, lakini hamkuona umbo lolote; sauti tu” (Kumb. 4:12). Ndiyo sababu hao walikatazwa wasiwe na sanamu: kwa kuwa zamani hizo hawakujaliwa kumuona Mungu.
Kumbe mtume Yohane aliweza kuanza kwa kishindo barua yake ya kwanza kwa kushuhudia juu ya Neno la uzima “lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa” (1Yoh. 1:1). Yesu ni “mng’ao wa utukufu” wa Mungu “na chapa ya nafsi yake” (Eb. 1:2), “ni mfano wa Mungu asiyeonekana” (Kol. 1:15); “katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili” (Kol. 2:9), hata aliweza kusema: “Aliyeniona mimi amemwona Baba” (Yoh. 14:9). Ukristo ni ufunuo wa Neno na wa sura ya Mungu katika Kristo. Mwenyewe ni picha ya Mungu isiyofanywa na mikono ya binadamu na iliyoonyeshwa katika hekalu la mwili wake.
Kuanzia hapo imani inatokezwa na kutangazwa si kwa maneno tu, bali pia kwa picha ambazo ni mafundisho kwa njia ya macho na ushahidi wa ukweli wa umwilisho wa Mwana wa Mungu. Bila ya shaka ni lazima tuangalie kwamba picha tunazozichora zilete ujumbe sahihi kadiri ya imani, kama vile ni lazima tuwe macho ili mahubiri na mafundisho tunayoyatoa yasipotoshe ukweli wa ufunuo wa Mungu. Mtaguso wa Pili wa Vatikano umeagiza: “Maaskofu wasikubali kamwe matumizi ya sanaa yanayopingana na imani na maadili na uchaji wa Kikristo katika nyumba ya Mungu na mahali pengine patakatifu. Pia wakatae yale yanayovunja heshima halisi ya kidini kwa sababu ni batili au kwa sababu hayatoi vielelezo halisi vya mambo matakatifu”.
Tunapaswa kuchambua picha, si kuzikataa jumla kama kitu kiovu. Hasa kwa wasiojua kusoma zinachangia sana imani na upendo kwa Bwana Yesu wakitambua upendo wake katika madonda na damu yake wanavyoona vimechorwa kwa usanii mkubwa. Mbele ya msalaba wengi wanaongoka na kuachana na dhambi zao. Wengine wanaponywa kimwili pia, kutokana na imani yao kwa Yesu iliyochochewa na picha yake. Bila ya shaka picha si mwenyewe, lakini inamwakilisha na kumfanya akumbukwe: hiyo ni kweli sio tu kuhusu picha zinazopigwa na kamera, bali pia kuhusu michoro na sanaa nyingine inayofaulu kutufikirisha juu ya mtu fulani.
 
                       
VIWAKILISHI VYA MTU
 
Agano Jipya linatusimulia jinsi watu wadogo walivyoweza kufaidika kiroho na kimwili na vitu vilivyosaidia imani yao, kama vile vazi la Yesu, kivuli cha Petro na leso na nguo za Paulo. Vitu hivyo vilipata nguvu kwa sababu ya kumwakilisha mmiliki wao. Tusome habari hizo za ajabu: “Tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema moyoni mwake, ‘Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona’. Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, ‘Jipe moyo mkuu, binti yangu, imani yako imekuponya’. Yule mwanamke akapona tangu saa ile” (Math. 9:20-22). Kilichomponya ni imani yake, lakini hiyo ilisaidiwa na tendo la kugusa pindo la vazi la Yesu. Ilitokea vilevile kwa wengine wengi walioletwa kwake hawawezi; “nao wakamsihi waguse hata pindo la vazi lake tu. Na wote waliogusa wakaponywa kabisa” (Math 14:36). Ilitokea vilevile kwa mitume wake: “hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao… nao wote wakaponywa” (Mdo. 5:15-16). “Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka” (Mdo. 19:11-12). Bila ya shaka vitu hivyo vyote havikuwa Yesu wala mitume wake wenyewe, lakini viliwawakilisha na kuwasaidia hao wagonjwa wawe na imani kwao. Si tofauti kwa picha na sanamu zetu: si Yesu wala si watakatifu wake wenyewe, lakini zinaweza kutusaidia tuwakumbuke na kujisikia tunaungana nao kwa njia hiyo. Sisi tunadhani kwamba waamini, baada ya kuelezwa vizuri na wachungaji wao, wana akili na imani ya kutosha hata waweze kuhusianisha picha na mtu bila ya kuwachanganya wala kudhani eti picha ndio mtu mwenyewe!
Kwa vile ufunuo umekusudiwa kwa watu wote bila ya kujali uwezo wa akili yao, Mwenyezi Mungu alipojifunua alitumia alama na njia za kila aina, kama vile moto, njiwa pamoja na sauti. Naye Yesu alitumia vitu kama vile mate, matope n.k. katika kuwaponya watu akatuachia sakramenti saba ambazo zote ni alama wazi ambazo kwa kuonekana na kusilikana kwao zinamaanisha na kutuletea neema za fumbo. Basi, ni dhahiri kuwa anatutaka sisi pia tutumie njia zote za maarifa: kusikia, kuona, kugusa n.k. ili yeye ajulikane na kutukuzwa. Upande mmoja tusidhani kwamba tutamjua na kumjulisha kwa njia za maarifa na vionjo vyetu tu: muhimu zaidi ni akili na hasa imani. Upande mwingine tusiingie kosa la kudhani tunatakiwa kutumia akili au imani tu, hata kukataa matumizi ya vitu na milango ya fahamu. Yesu alisifu imani ya yule mwanamke ingawa yeye aliona haimtoshi kumuamini bila ya kugusa pia pindo la vazi lake. Anayetakiwa kumjua na kumkaribia Mungu katika ibada na maisha ni binadamu nafsi nzima: yaani mwili kwa kutumia vionjo vyake na njia zake za maarifa, akili kwa kuchanganua, kuchambua na hata kusanii taarifa zinazomfikia, ikiongozwa daima na imani kwa ujumbe wa Mungu.           
Ni mang’amuzi ya siku nyingi kwamba ibada kadhaa zinavutia sana waamini kwa vile zina kielelezo cha sanamu na picha zinazowasaidia kutafakari mafumbo ya wokovu, kwa mfano ibada ya Ijumaa Kuu. Tazama pia upendo na huruma ambavyo vinaamshwa na ibada ya Njia ya Msalaba! Na tazama vinavyozidi kuongezeka kila kituo hadi msalabani na kaburini. Kweli, unaweza ukawasimulia watu mateso ya Yesu na kusababisha uchungu na majuto. Lakini wakiona picha za filamu juu ya mateso hayohayo, zikiwachorea mazingira yale yalivyokuwa, wengi wataguswa zaidi hata kulia machozi, hata kama wanajua kuwa ni igizo tu. Kumuona Yesu amefungwa kamba nene akiwa mikononi mwa wakatili ambao wanampiga mijeledi na kutiririsha damu yake: ni picha ambazo hazisahauliki kwa urahisi na zinasaidia kufikiria tukio ambalo hawakulishuhudia wenyewe. Pasipo msaada huo, kila mmoja anajichorea akilini kadiri ya ujuzi na uwezo wake. Kumbe wasanii wamejaliwa na Mungu kipaji cha kutuchorea kwa ufanisi mkubwa mambo yoyote, hata ya imani, na kama talanta nyingine zozote wanapaswa kukifanyia kazi kwa faida ya wote. Biblia inasifu ufundi waliojaliwa wale waliochaguliwa kuchonga makerubi : “Basi, Bezaleli na Oholiabu watatenda kazi, na kila mtu mwenye moyo wa hekima, ambaye Bwana amemtia akili na hekima ili ajue kufanya kazi hiyo yote kwa huo utumishi wa mahali patakatifu, kama hayo yote Bwana aliyoyaagiza” (Kut. 36:1). Ukurasa wa kwanza wa Biblia unamfananisha Mungu na msanii ambaye anatazama kila kazi ya mikono yake na kuridhika nayo. Alipomuumba mtu, kiumbe chake bora duniani, alimshirikisha usanii wake kama kipaji cha pekee cha kutokeza zaidi uzuri wa viumbe vyake. Msanii anahisi uzuri kuliko watu wengine, na pia anaweza kuutokeza kwa kiasi fulani katika mashairi, michoro n.k. Kwa haki sanaa mbalimbali zinahesabika kati ya kazi za heshima zaidi kwa binadamu, kwa kuwa zinatokeza uwezo wake wa kufurahia uzuri. Kanisa pia toka zamani limeheshimu kipaji hicho na kukikaribisha katika ibada zake, kuanzia muziki mtakatifu. Katika historia yote, sehemu kubwa ya sanaa zote zinazohifadhiwa na Umoja wa Mataifa ni sanaa za Kikatoliki. Kanisa linaukabidhi usanii kazi ya kufanya ulimwengu wa roho uvutie zaidi kwa kutokeza uzuri wa mafumbo ya imani pia katika rangi, sauti na kadhalika. Lakini watu wote jumla wanahitaji daima kuchota katika sanaa mwanga fulani kuhusu maisha yao ambao unaelekeza kwa Mungu. Uzuri unatia pia tumaini kati ya mabaya mengi yanayokera duniani.
Ushirikiano wa imani na sanaa uliwahi na bado unaweza kutokeza uzuri wa kazi ya Mungu unaong’aa hasa katika Yesu na watakatifu wake. Kwa watu wote uzuri wa namna hiyo ni njia ya kupenya mafumbo ya imani na ni mvuto wa kuinuka juu kuliko mambo ya dunia hii. Tufikirie tu uzuri wa muziki wa dini unaotokeza kwa namna bora yaliyomo katika maneno ya Zaburi fulani hata kutufanya tuyaonje na kuyafurahia kwa dhati kabisa. Vilevile hatuwezi kuikataa amani inayotuingia moyoni mahali penye picha nzuri za imani, tofauti kabisa na karaha na vishawishi vinavyotupata kwenye picha zisizofaa.         
Katika ulimwengu wa leo tunapatwa na mafuriko ya picha za kila aina, nyingi zikiwa chafu na katili, nazo zinavuta hasa watoto na vijana kutenda vile walivyoona. Ikiwa shetani anazitumia sana hizo picha kwa kutupotosha, kwa nini sisi tusitumie njia hiyohiyo kuenezea usafi na wema? Tunapovaa au kubandika mahali picha takatifu huwa tunaungama na pia kutangaza imani yetu kwa njia yake. Wafanyabiashara wanajua vizuri jambo hilo, hata wakamwaga pesa nyingi ili picha ya bidhaa yao ionekane popote pamoja na jina lake. Na kweli wateja wanakimbilia hasa bidhaa zilizotangazwa zaidi. Basi, nasi tutangaze popote imani yetu hata kwa njia hiyo.
Tena, hizo ishara za imani zinatudai tuishi kwa uadilifu tusije tukaaibisha dini yetu na kujiaibisha mbele ya wale wanaoziona tumezivaa au kuzibandika kwetu. Hivyo pia zinachangia utume wetu kwa kutuhimiza tuwe na mwenendo mwema. Lakini hata kabla ya hiyo, picha takatifu zinaamsha ndani mwetu hamu ya kulingana na Yesu au mfuasi wake aliyechorwa ndani yake. Ni kama unapoona picha ya baba wa taifa, marehemu mwalimu Nyerere, na papohapo unakumbuka uaminifu wake na ujumbe wake wa amani na haki ambao unakudai usipotoke.
 
 
HESHIMA KWA SANAMU NA PICHA TAKATIFU
 
Pamoja na kukataa jumla matumizi ya picha takatifu katika makanisa, wengi wanasema linawakwaza hasa tendo la kuziheshimu. Kumbe labda hawashangai jinsi kinavyoheshimika kitabu cha Neno la Mungu, kwa kukijaladia vizuri, kukishika kwa uangalifu mkubwa, kukishangilia, kukibusu na hata kukifukizia ubani. Kwetu ni wazi kabisa kwamba heshima tunayoitoa hailengi ubao, madini au chochote kile kilichotumika kutengenezea picha au sanamu, wala karatasi na wino vilivyotumika kuandikia kitabu hicho, bali yule aliyechorwa au anayesema nasi kwa vitu hivyo. Hilo ni jambo la kawaida katika maisha ya binadamu, ambaye anatunza kwa makini picha za watu anaowapenda, na vitu vyao, si kutokana na thamani ya vitu hivyo, bali kutokana na jinsi anavyothamini watu hao. Ukichukua picha ya marehemu wake, kwa mfano, na kuichana kwa dharau, utaona atakavyosikitika. Ni vilevile ukichana kitambaa chenye rangi za taifa: utalaumiwa na kuhukumiwa kwa kuikosea heshima nchi na watu wake. Tunasoma historia ya mtawa Stefano ambaye alithubutu kumuendea huyo mfalme Leo mwanzilishi wa mapambano dhidi ya picha takatifu akamuonyesha pesa yenye sura yake, akimuuliza: “Sura hii ni ya nani?”. Mfalme akamjibu: “Mbona ni sura yangu!” Hapo mtawa akaitupa ile pesa chini akaikanyagakanyaga. Mara akakamatwa akahukumiwa kifo kwa sababu ya kukanyaga sura ya mfalme. Lakini wakati wa kupelekwa akamuambia mfalme: “Tazama! Kama mimi nitaadhibiwa hivi kwa sababu tu sikuheshimu sura yako katika pesa, na wewe ni kiumbe tu utakayekufa, watastahili adhabu gani watu kama wewe wanaoteketeza picha za Yesu, Mwana wa Mungu?”. Ingawa huyo mtawa shujaa akauawa, ukweli alioutoa kwa maneno yake unabaki palepale hata leo.
Heshima inaweza kutolewa kwa namna mbalimbali, kadiri ya utamaduni wa mahali: sehemu nyingine watu wanaheshimiana kwa kupiga goti, kwingine kwa kuinama au kuinamisha kichwa, kwingine kwa kubusiana mikono au nyuso, na kadhalika. Ni kweli kwamba baadhi ya heshima hizo tunazitumia kwa Mungu pia, lakini nadhani kila mtu anaelewa kuwa tukimpa Mungu ni kwa dhati kuliko tunapompa kiumbe chake. Hata katika Biblia tunaona matendo hayo yalivyotumika kwa watu wa Mungu, kwa mfano mfalme Daudi: “Ahimaasi aliinua sauti yake, akamwambia mfalme, ‘Amani!’ Akainama mbele ya mfalme kifudifudi, akasema, ‘Ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyewatoa watu hao walioiinua mikono yao juu ya bwana wangu, mfalme’” (2 Samweli 18:28). Mfalme Daudi hakukataa kusujudiwa, kwa sababu huyo Ahimaasi alipofanya hivyo alimhimidi Mungu aliyemuokoa, na hivyo alimkiri Mungu wake kuwa mkuu kabisa. Hata nabii Nathani alimuinamia mfalme Daudi: “Walimwambia mfalme wakasema, ‘Tazama, Nathani, nabii’. Naye alipoingia ndani mbele ya mfalme, akamsujudia kifudifudi” (1Fal. 1:23). Nabii wa Mungu hakuona ni kosa kumsujudia mfalme aliyeteuliwa na Mungu aongoze kwa niaba yake taifa la Israeli.
Tukiendelea kusoma tunakuta nabii Eliya alivyopokea kwa wema wajumbe wa mfalme Ahazia waliomuinamia, tofauti na waliotangulia kumuendea ambao hawakumheshimu vya kutosha wakateketezwa kwa moto kutoka mbinguni: “Yule akida wa hamsini wa tatu akapanda, akaenda akapiga magoti mbele ya Eliya, akamsihi sana, akamwambia, ‘Ee mtu wa Mungu, nakusihi, roho yangu na roho za watumishi wako hawa hamsini ziwe na thamani machoni pako’” (2 Fal. 1:13). Eliya, mtetezi mkuu wa upekee wa Mungu, hakulaumu hilo tendo la kumpigia magoti na kumsihi yeye binadamu, kwa msingi wa kuwa aliitwa mtu wa Mungu, yaani akida alimtofautisha na Mungu na kumheshimu kwa kuwa ni nabii wake.
Ni kweli kwamba watu wengine wa Mungu na malaika walikataa kupigiwa magoti, lakini Biblia inaonyesha wazi ni kwa sababu gani, yaani kwa kuwa waliopiga magoti walitaka kuwaabudu kama Mungu au miungu. Kwa mfano, tunasoma katika Matendo 14:11-15: “Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, ‘Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu’. Wakamwita Barnaba, Zeu, na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji. Kuhani wa Zeu ambaye hekalu lake lilikuwa mbele ya mji, akaleta ng’ombe na taji za maua hata malangoni, akitaka kutoa dhabihu pamoja na makutano. Walakini mitume Barnaba na Paulo, walipopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika makutano, wakipiga kelele, wakisema, ‘Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi’”. Kwa msingi huohuo Yesu alikataa kumsujudia shetani: “Ibilisi alimchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia, ‘Hata yote nitakupa, ukianguka kunisujudia’. Ndipo Yesu alipomwambia, ‘Nenda zako, shetani! Kwa maana imeandikwa: Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake’” (Math. 4:8-10). Lakini Yesu hakusita kupiga magoti mbele ya mitume wake, wakiwa ni pamoja na Yuda msaliti, ili awaoshe miguu kama kwamba ni mtumwa wao: “Alitia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga” (Yoh. 13:5). Tendo lilelile moja linaweza kuwa na maana mbili, moja mbaya moja bora kabisa. Inategemea nia ya mtu.
Ndivyo ilivyo pia kuhusu vitendo vyetu vya heshima kwa picha na sanamu takatifu: sisi hatuna nia yoyote ya kuziabudu. Ila tunamuabudu Yesu aliyechorwa kwa kuwa ni Mwana wa Mungu, na tunawaheshimu kiasi chao watakatifu wake kwa sababu ni watu wa Mungu na kwa sababu Mungu mwenyewe anawaheshimu, alivyosema Yesu: “Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu” (Yoh. 12:26).
Zingatia kuwa picha zetu zote ni za viumbe halisi, sio za miungu ya bandia kama ilivyokuwa kwa wapagani wa zamani za Agano la Kale na za Agano Jipya walioabudu sanamu za wanyama na za vingine visivyowahi kuwepo nje ya ubunifu wao. Sisi tunamchora Yesu na watakatifu wake, hasa mama yake: hao wote waliishi kweli duniani wakatuachia mifano bora ya uadilifu, nasi tunawaheshimu kwa sababu hiyohiyo tu, yaani kwa jinsi walivyompenda na kumtumikia Mungu. Ni watu halisi, tena bora, walio hai kwa Mungu na wanaostahili heshima zote.
Kumhusu Yesu tumeandikiwa na mtume Paulo: “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu, ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba” (Fil. 2:5-11). Amina: kwa jina la Yesu kila goti lipigwe! Lakini, ebu, jina ni kitu gani? Ni kiwakilishi tu cha mtu mwenyewe. Ukiliheshimu jina la Yesu, heshima inamuendea yeye, si herufi zinazounda jina hilo. Basi, hata picha yake inaweza kuwa kiwakilishi chake, hivi kwamba heshima unayokipatia inamuendea Yesu mwenyewe. Ndiyo sababu jina hilo linaweza likatamkwa kwa namna mbalimbali kadiri ya lugha, bila ya kupotewa na maana yake ya kumwakilisha mwana wa Maria wa Nazareti: unaweza kumuita Jesus kwa Kiingereza, Isa kwa Kiarabu, n.k., mradi umkiri kuwa ndiye Bwana wa vyote. Kumbe unaweza ukamkuta mtu anayesisitiza kwamba si sahihi kumuita Yesu “Kristu”, wakidai matamshi ya kufaa ni “Kristo”. Yaani kuishia na o badala ya u! Tukitaka kuzingatia matamshi asili ya Kigiriki tunatakiwa kutamka Kristos, au sanasana Kristosi. Na tukifanya hivyo, kwa nini tusitamke vizuri pia jina la Yesu, kwa Kiyahudi Yeshuah ? Ni afadhali tukubaliane kwamba matamshi si muhimu zaidi, yanaweza kubadilika kadiri ya mahali. Nikitamka Kristu siendi motoni kwa hiyo, na nikitamka Kristo siendi mbinguni kwa hiyo.
Unajua, katika maisha ya Yesu wengi hawakumuelewa, hasa wale wasiotaka kumuelewa. Hivyo si ajabu kukuta hata leo wabishi waliojipa kazi ya kukosoa wote na kusahihisha yote, hata kuhusu mambo madogomadogo. Mtu akipenda anaweza akatusahihisha wote tunaposema kuwa jua limezuka au limepanda au limetua, akisisitiza kwamba jua halisogei popote, bali dunia inazunguka kandokando yake. Lakini atasaidia nini? Mbona siku hizi karibu wote wanajua kuwa ndivyo ilivyo? Tuachane na kiburi! Tusidhani kuwa sisi peke yetu tunaelewa jografia, na wengine wote ni wajinga kiasi hicho.
 
 

KUABUDU MSALABA

 
Haya tuliyoyasema yanafaa kuhusu neno moja la liturujia ya Ijumaa Kuu ambalo linaeleweka vibaya na kupingwa sana na baadhi ya wenzetu, yaani ‘kuabudu msalaba’. Wanalielewa kama kwamba ni ibada kwa mbao zake. Basi, tunaposema “kuabudu msalaba”, tunaomba wenzetu hao watuelewe tunataka kusema nini. Nichukue mfano wa mtume Paulo aliyeandika: “Yeye aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana” (1Kor. 1:31), yaani asionee fahari kitu kingine chochote. Hata hivyo alipowaandikia Wagalatia mwenyewe alitamka (6:14): “Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu chochote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulubishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu”.
Ni wazi kuwa Paulo hakutaka kusema anazionea fahari mbao za msalaba tu, bali fumbo la msalaba ambalo tumekombolewa. Fumbo hilo limebadilisha kabisa ulimwengu, likidai tubadili pia mawazo na matendo yetu yote tukabebe misalaba yetu nyuma ya Yesu: “Mtu yeyote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate” (Mk. 8:34). Tukimzungumzia Kristo jumla tu, tunaweza tukamuelewa kama mtukufu tu, mbali na ulimwengu na mateso yake, na hivyo kutufanya tukwepe hali halisi ya ulimwengu huu wa mateso. Ndiyo sababu Paulo alisisitiza kwamba “sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulubiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu” (1Kor. 1:23-24). Kwa hiyo tunapaswa kukubali kwanza mpango wa Mungu aliyetaka Mwanae ateswe msalabani ili abebe laana ya dhambi zetu na kuifutilia mbali, halafu sisi tufuate nyayo zake. Mtume alilionea fahari fumbo hilo, ingawa alijua fika kuwa Kumbukumbu la Torati (21:22-23) linasema: “Akiwa mtu ametenda dhambi ipasayo kufa, akauawa, nawe utamtundika juu ya mti, mzoga wake usikae usiku kucha juu ya mti; lazima utamzika siku iyo hiyo, kwani aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu”.
Sisi pia tusione msalaba kama adhabu ya aibu, bali tuupende na kuuonea fahari. Si mbao za msalaba ambazo hatujui zilikwenda kwishia wapi, bali fumbo hilo la upendo wa Mungu lililotukomboa, na hasa yule aliyesulubiwa kwa ajili yetu. “Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu” (1 Kor. 1:18). Ndiye tunayemuabudu. Kama tulivyokwishaeleza, tunapopiga goti mbele ya sanamu ya Yesu msulubiwa na kuibusu, heshima hizo zinamuendea yeye kama shukrani ndogo kwa upendo wake mkuu. Naye anazipokea kama alivyozipokea heshima alizopewa na watu wa zamani zake, ingawa wengine walinung’unika. Tunasoma, kwa mfano, habari za mwanamke ambaye alimpaka mafuta Yesu akasifiwa naye kwa kumuonyesha hivyo heshima yake: “Amin, nawaambieni: Kila patakapohubiriwa Injili hii katika ulimwengu wote, tendo hilo alilolitenda huyu litatajwa pia kwa kumbukumbu lake” (Math. 26:13). Kumbe baadhi ya wanafunzi na wengineo walinung’unika sana, hata ilimpasa Yesu kuwakemea: “Mwacheni; mbona mnamtaabisha? Amenitendea kazi njema” (Mk. 14:6). Angalia usirudie leo kosa walilolifanya hao kwa kumlaumu bure huyo mwanamke kwa jinsi alivyomheshimu Yesu tofauti na mitazamo yao. Unaweza ukamlaumu mtu anayemheshimu Yesu kwa kubusu sanamu yake kwa imani na upendo, ukijidai wewe tu una imani na unajua namna ya kufaa ya kumheshimu. Kumbe Yesu ameridhika kabisa na heshima zake.
Hata siku nyingine wanafunzi walionywa na Yesu alipoona wanataka kuwazuia watu wasimheshimu walivyotumwa na moyo wao, yaani kwa kumuomba awabariki watoto waliomletea. “Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, ‘Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni: Yeyote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa’” (Mk. 10:14-15). Ndio, ndugu, tunahitaji kuongoka na kuwa kama watoto ili tuingie katika ufalme wa Mungu. Badala ya kuwahukumu watu wenye moyo wa kitoto mbele ya picha takatifu, tujitahidi kuachana na kiburi na tabia ya kuhukumu bure. Mungu tu anajua mioyo ya watu. Tusiwapime kulingana na namna ambayo sisi tunajua Biblia. Hata zamani za Yesu waliojidai waadilifu kwa kujua na kushika sheria ya Musa walidharau sana wenzao wasiokuwa na elimu hiyo. Kumbe ndio walioshindwa kumuamini na kumfuata Yesu. Sikiliza maneno yao: “Ni nani katika wakuu amwaminiye, au katika Mafarisayo? Lakini makutano hawa wasioifahamu torati wamelaaniwa” (Yoh. 7:48-49). Yesu aliwahi kuwaonya: “Mwayachunguza Maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima” (Yoh. 5:39-40). Namna yao ya kuelewa Biblia, pamoja na kuwafanya wahukumu wenzao, iliwasogeza mbali na Yesu mwenyewe, hasa baada ya kumuona amefia msalabani! “Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu tunaookolewa ni nguvu ya Mungu” (1Kor. 1:18).

No comments:

Post a Comment