Thursday, May 9, 2013

Shutuma za udini dhidi ya Mwl. J. K. Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania



Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania ni kati ya viongozi wa siasa wanaoheshimika sana Barani Afrika. Lakini kwa bahati mbaya, "Nabii hakosi heshima isipokuwa kwa watu wa nyumbani kwake". RealAudioMP3

Kwa miaka kadhaa, baadhi ya Waamini wa dini ya Kiislam nchini Tanzania amedai kwamba, wakati wa utawala wa Mwalimu Julius K. Nyerere, waamini hao walinyanyaswa kiasi kwamba, wamebaki nyuma kimaendeleo ikilinganishwa na waamini wa dini nyingine nchini Tanzania.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, katika mahojiano maalum na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, anakanusa uvumi huu kwa kusema kwamba, ni malalamiko ambayo yamezagaa nchini Tanzania kiasi kwamba, kuna baadhi ya watu wamediriki hata kutengeneza Kanda ili kueneza uvumi huu. Haya ni mawazo yaliyonunuliwa kutoka nje, ili kuvuruga misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa ambao watanzania kwa takribani miaka 50 iliyopita wamekuwa wakiufaidi.

Askofu Msonganzila anasema, hizi ni dalili za ukoloni mambokesho! Kinzani za kidini kwa madai kwamba, Serikali ya Tanzania inaongozwa na mfumo Kristo ni uzushi usiokuwa na msingi. Watanzania watakumbuka kwamba, wakati wa Azimio la Arusha, Serikali ilitaifisha shule zilizokuwa zinamilikiwa na kuendeshwa na Kanisa, ili kutoa fursa kwa watanzania wengi zaidi kupata fursa ya elimu.

Kanisa lilitambua na kuheshimu nia njema iliyooneshwa na Baba wa Taifa bila kunung'unika. Ikumbukwe kwamba, mikakati ya kichungaji katika sekta ya elimu ni sehemu ya Uinjilishaji wa kina unaofanywa na Kanisa Katoliki katika mchakato wa kukomboa mtu mzima: kiroho na kimwili, kumbe kumiliki na kuendesha shule katika viwango mbali mbali si jambo la nasibu bali ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa Katoliki.

Hata baada ya kutaifishwa shule, watanzania wengi waliokuwa na kiu ya elimu walipata bila ya ubaguzi wowote, kinyume kabisa cha madai yanayotolewa na baadhi ya waamini kwa sasa! Kuna watanzania wengi ambao baadhi yao ni viongozi waandamizi Serikali wamesoma katika shule zilizotaifishwa au zilizokuwa zinamilikiwa na Kanisa, bila shaka hawa ni mashahidi makini wa hali halisi ilivyokuwa katika shule hizi.

Askofu Michael Msonganzila anasema, hizi ni zama za ukweli na uwazi, watanzania wanapaswa kufungua macho, masikio, mioyo na akili zao ili kuuona ukweli. Huu si muda wa malumbano, bali watu wawekeze katika elimu inayomwangalia mtu mzima: kiroho na kimwili, ili kuweza kuwajengea watoto wa kitanzania, kesho iliyo bora zaidi.

Elimu ya dini na elimu dunia zina nafasi yake. Watanzania wasikubali kutumiwa na watu wasiowatakia mema kwa kufanya ghasia na malumbano yasiyokuwa na tija kwa maendeleo yao. Wakumbuke daima kwamba, vita na ghasia hazina macho, kwa kujiingiza katika migogoro ya kidini, watapoteza hata kile kidogo walicho nacho kwa sasa! Ni wakati wa kujenga na kuimarisha mshikamano na umoja wa kitaifa dhidi ya maadui walioko ndani na nje ya Tanzania wanaotaka kulitumbukiza Taifa katika maafa ya udini.


SOURCE: http://sw.radiovaticana.va/news/2013/01/30/shutuma_za_udini_dhidi_ya_mwl._j._k._nyerere,_baba_wa_taifa_l/kws-660219

No comments:

Post a Comment