Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake, Jumatano tarehe Mosi Mei, 2013 ameitolea kwa heshima ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi pamoja na Bikira Maria Mama wa Yesu ambaye Mwezi Mei, Kanisa linafanya Ibada maalum kwa ajili yake changamoto ya kumtafakari Yesu Kristo katika hija ya maisha ya kila siku.
Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, Mtakatifu Yosefu ambaye kitaaluma alikuwani Seremala, ni mtu anayewakumbusha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema dhamana na umuhimu wa kazi. Anasema, kazi ni sehemu ya mpango wa Mungu kwa ulimwengu, mwaliko wa kuitekeleza kwa juhudi, maarifa na kuwajibika zaidi kwa ajili ya mafao ya kazi ya uumbaji na utu wa mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, ukosefu wa fursa za ajira ni tatizo na changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi kwa kuzingatia mshikamano wa kijamii pamoja na sera makini. Anawataka vijana kuendelea kutafuta fursa za ajira kwa matumaini bila ya kukata tamaa, kwa kuwekeza zaidi katika elimu, kazi na mahusiano bora na wengine.
Mtakatifu Yosefu ni mfano wa mtu aliye sali katika ukimya, akawa karibu zaidi na Yesu, changamoto ya kuangalia ni kiasi gani cha muda ambao waamini wanatenga kwa ajili ya kusali na kulitafakari Neno la Mungu. Mwezi Mei ni mwezi wa Rozari Takatifu unaowapatia waamini nafasi ya kutafakari Fumbo la Maisha ya Kristo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu ili waweze kuwasaidia kuwa waaminifu katika utekelezaji wa majukumu ya kazi zao za kila siku pamoja na kuinua akili na mioyo yao kwa Yesu katika sala.
Baba Mtakatifu Francisko ametambua uwepo wa: waamini, mahujaji na wageni wanaozungumza lugha ya Kiingereza, wote hawa amewatakia kheri, baraka na amani ya kutoka kwa Kristo Mfufuka. Anawaalika waamini kusali kama Familia pamoja na Familia kwani familia inayosali pamoja hiyo itadumu na kuimarika. Anawataka vijana kujikita zaidi katika masomo, kazi, matendo ya upendo pamoja na kujenga urafiki wenye tija!
Kwa waamini na mahujaji wanaozungumza lugha ya Kiarabu, Baba Mtakatifu anawataka kuwa na ujasiri katika utekelezaji wa majukumu yao kwa njia ya sadaka, daima wakiwa na matumaini hai bila kukata tamaa.
Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko amesema, Mei Mosi ya Mwaka huu, Kanisa linafanya kumbu kumbu ya miaka miwili tangu Papa Yohane Paulo wa pili alipotangazwa kuwa Mwenyeheri, changamoto kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, maisha yake yanafumbatwa katika imani, upendo na ujasiri wa kitume kama ule uliooneshwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili.
Baba Mtakatifu ametambua pia uwepo wa Mapadre kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Paulo, Roma; Watawa wa mashirika mbali mbali wanaoadhimisha mikutano yao mikuu hapa Roma, waamini kutoka Parokia mbali mbali na vyama vya kitume, kila mmoja anachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa mwaminifu kwa wito wake kwa njia ya ushuhuda makini.
Vijana wajitahidi kumpenda na kumfuasa Kristo kwa uaminifu; wagonjwa watolee shida na mahangaiko yao katika Fumbo la Upendo wa Yesu aliyemwaga Damu yake Azizi; wanandoa wapya wawe waaminifu katika maagano yao na waoneshe upendo wa Kristo kwa Kanisa lake.
Mara baada ya katekesi, Baba Mtakatifu Francisko ametumia muda mrefu kwa ajili ya kusalimia na kuzungumza na waamini na mahujaji waliokuwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Baadhi ya watu wameshangazwa walipomwona Baba Mtakatifu akibadilishana Kikofia cha Kipapa na Padre, akakivaa hapo hapo bila hata ya kufikiri mara mbili! Matendo makuu ya Mungu kwa watu wake!
source : http://sw.radiovaticana.va/news/2013/05/01/umuhimu_wa_kazi_na_tafakari_kuhusu_fumbo_la_maisha_ya_yesu_kristo!/kws-687948
No comments:
Post a Comment