Sunday, December 29, 2013

Familia: Mke na mume; Baba na Mama: ni kielelezo cha neema na upendeleo wa Mungu kwa mwanadamu!



Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika Maadhimisho ya Sherehe ya Familia Takatifu, hapo tarehe 29 Desemba 2013 linasema, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinaheshimiwa na watoto wanapewa haki ya malezi ya wazazi wa pande zote mbili, kuliko mbio za kutaka kuwa na ndoa za watu wa jinsia moja. RealAudioMP3
Waamini na watu wenye mapenzi mema, wazoeshwe tena kusikia kuhusu: Bwana na Bibi; Mke na Mume ili kuonja tofauti zilizopo na jinsi watu hawa wanavyotegemezana na kukamilishana kadiri ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu.
Maaskofu wanasema, “Mke na Mume”, Bwana na Bibi, Baba na Mama ni kielelezo cha neema na upendeleo ambao Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu kwa kumshirikisha katika dhamana ya uumbaji, ili kuzaa na kuijaza dunia. Maaskofu wanasikitishwa na mabadiliko yaliyofanywa na Serikali katika sheria ya ndoa ya mwaka 2005 na kwamba, kwa sasa lugha inayotumika ni ya jumla wala hakuna tofauti. Maaskofu wanasema, upendo wa kweli kadiri ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu unajengwa kati ya Bwana na Bibi; vinginevyo; Jamii inataka kutema Injili ya Uhai na kukumbatia Utamaduni wa Kifo.
Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa, hasa wakati huu wa utandawazi na athari za myumbo wa uchumi kimataifa na kwamba, familia itaendelea kubaki kuwa ni chemchemi ya furaha na matumaini katika maisha ya mwanadamu.
Familia inayojengeka katika msingi wa upendo kati ya Bwana na Bibi inaonesha mwendelezo wa agano kati ya Mungu na mwanadamu. Waamini na watu wenye mapenzi mema wanapaswa kulitambua hili. Familia ijifunze pia kuwaenzi wazee kwani hawa ni kisima cha hekima na busara; maadili na utu wema.


habari : radio vatican

No comments:

Post a Comment