Kanisa Katoliki linapenda kuwa mstari wa mbele na mfano wa kuigwa katika kulinda na kutetea haki msingi za watoto sehemu mbali mbali za dunia, dhidi ya nyanyaso na mambo yanayokwamisha malezi na majiundo ya watoto: kiroho na kimwili.
Hivi ndivyo alivyobainisha Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican, kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva wakati alipokuwa anawasilisha taarifa ya utekelezaji wa haki za watoto kutoka Vatican kwenye mkutano wa sitini na tano wa Umoja wa Mataifa kuhusu utekelezaji wa itifaki ya ulinzi wa haki za watoto huko mjini Geneva, hapo tarehe 16 Januari 2014.
Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anasema, Vatican imejibu maswali yote yaliyoulizwa na Umoja wa Mataifa kwa njia ya maandishi kwa kufafanua sera na mikakati inayotekelezwa na Kanisa Katoliki katika kukabiliana na nyanyaso na dhuluma dhidi ya watoto wadogo. Vatican imekwisha toa kanuni elekezi kwa Makanisa mahalia jinsi ya kupambana na tabia hii chafu hasa katika taasisi zake za elimu na majiundo.
Askofu mkuu Tomasi amebainisha kwa kina na mapana, mikakati, sheria, kanuni na taratibu ambazo zimechukuliwa na Vatican kama sehemu ya mchakato wa kupambana na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, kashfa ambayo ililichafua Kanisa katika miaka ya hivi karibuni. Hizi ni juhudi ambazo zimevaliwa njuga kwa namna ya pekee na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI pamoja na Papa Francisko ambaye hivi karibuni aliunda Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto.
Askofu mkuu Tomasi anasema, hakuna sababu yoyote ile inayoweza kuhalalisha nyanyaso dhidi ya watoto wadogo, ndiyo maana Vatican inataka kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya watoto wadogo katika hatua mbali mbali za malezi na makuzi yao; yaani tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake.
Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kulinda na kutetea pia haki msingi za familia; kitovu cha malezi na makuzi ya mtoto. Wazazi wana haki na dhamana ya kutoa malezi na majiundo makini kwa watoto wao pamoja na kuheshimu uhuru wa kidini. Hizi ni haki msingi za familia katika malezi na makuzi ya watoto sehemu mbali mbali za dunia.
Ujumbe wa Vatican unasubiri kwa hamu kusikia ushauri utakaotolewa na Umoja wa Mataifa kuhusiana na jitiahada zake katika kulinda na kutetea utu na heshima ya watoto wadogo na kwamba, iko tayari kuufanyia kazi ushauri huu, mintarafu malengo ya itifaki ya kulinda watoto iliyoridhiwa na Jumuiya ya Kimataifa kunako Mwaka 1992.
Nukuu : radio vatcan
No comments:
Post a Comment