Mpendwa
msikilizaji wa kipindi tafakari masomo Dominika, Dominika iliyopita
tulimaliza kipindi na shamrashamra za Noeli na tulianza kipindi cha
kawaida cha mwaka wa Kanisa. Ndiyo kusema sasa tunatafakari masomo
Dominika ya II ya mwaka A.
Masomo
Dominika hii: Somo la kwanza tunalipata katika Kitabu cha Isaya 49:3,
5-6. Somo II 1Kor. 1:1-3 na Injili Yn. 1:29-34 Mwaliko ni kutafakari na
kuishi WITO WA KIKRISTO. Nabii Isaya yuko katika ndoto na anapokea wito
wa Mungu kwa ajili ya taifa lake la Israeli. Isaya anaalikwa kutegemea
nguvu za Mungu katika shughuli hiyo ya wito kwa ajili ya kuwarejeza watu
wa Israeli katika amani na usalama. Mungu anamwahidia kuwa atakuwa nuru
ya mataifa na hata miisho ya dunia. Tuko pia katika Juma la kuombea
Umoja wa Wakristo, linaloongozwa na kauli mbiu ”Je, Kristo
amegawanyika?”
Mpendwa mwana tafakari, ni vema na inafaa
kujiuliza huyu mtumishi wa Mungu ni nani? Katika Agano la Kale
tunakutana na sura ya mtumishi katika kitabu cha Nabii Yeremia 1:5 na
hapa tunaona Mungu akimwambia Nabii Yeremia yakuwa alimteua tangu
hajatungwa mimba na amemteua kuwa nabii kwa mataifa. Mwinjili Lk 1:15
anamtaja mtumishi ambaye hatakunywa divai wala kileo, na atajazwa Roho
Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake. Fundisho hili linakuja wakati
Waisraeli wako utumwani Babeli wanateseka na kwa njia ya nabii, Mungu
anatangaza uhuru watakaoupata kwa njia ya mtumishi wa Mungu.
Kwa
hakika aguo hili linakamilika katika Masiha, Yesu Mnazareti aliyezaliwa
katika kipindi cha Noeli. Hawa manabii waliotangulia ambao walikuwa
vyombo vyake wanatoa picha ya Masiha ambaye atatenda kadiri ya mpango wa
Baba yake. Mpendwa msikilizaji kazi yako hivi leo pamoja na jumuiya na
familia ni kuwa mtumishi mwaminifu kwa ajili ya kupeleka habari njema ya
wokovu kwa mataifa.
Mtume Paulo akiwaandikia Wakorinto
anawakumbusha juu ya wito wake na wito wa Sosthene na hasa ule wito
mkuu wa kuwa watakatifu. Katika barua yake hiyo anaonesha kazi ya wito
ikiwa ni kwa ajili ya kuwatakia wengine yaani taifa la Mungu mema yote
ya mbinguni. Ndiyo kusema mpendwa msikilizaji wito ni kwa ajili ya
kufariji na kushona mahali ambapo pamechanika katika harakati ya
kuuendea uhuru kamili wa wana wa Mungu. Yafaa kukumbua kuwa wakati Paulo
anawaandikia Wakorinto walikuwa katika ugomvi na ukosefu wa utulivu
katika jumuiya yao. Akitangaza kwanza mamlaka aliyokabidhiwa na Kristo
anawakemea na kuwambia nini maana ya kuwa mkristu. Kwa hakika ni
kutumikia kwa furaha na kutenda kadiri ya matakwa ya Injili. Umoja
kamili unajikita katika mafundisho ya Kristo ndiyo msingi wa maisha ya
wito wetu.
Katika Injili nabii Yohane Mbatizaji anakiri ukuu wa
Masiha akisema yeye ndiye aliyenipeleka na hivi ni kabla yangu na kabla
ya yote. Ndiyo kusema Yohane Mbatizaji yuko tayari kushuka kwa maana
wito ni ule wa kuonesha kwa mataifa yakwamba Kristu ni Mwanakondoo wa
Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu. Kwa hakika ile sifa yakwamba
nilikuchagua kabla ya kutunga mimba haimwangukii Masiha kama wale
manabii wa Agano la Kale, ndiyo maana basi Yohane anamtambulisha kama
Mwanakondoo wa Mungu, ambaye utume wake ni kuondoa dhambi za dunia,
dhambi zetu sote.
Kwa kutumia Mwanakondoo wa Mungu, anataka
kuturudisha nyuma kutafakari ule usiku mtakatifu Waisraeli walipotoka
Misri. Tunakumbuka kila familia ilichinja mwanakondoo na ilitumia damu
kupaka milango na ikawa ni alama kwa wokovu wao. Ni kwa mantiki hiyo
basi Yohane mwinjili anaweka mbele yetu Yesu atakaye toa maisha yake kwa
njia ya kumwaga damu yake takatifu. Mtumishi huyu atateswa lakini kwa
njia ya mateso yake atauokoa ulimwengu.
Mpendwa msikilizaji
Yohane Mbatizaji analo jambo la kutuambia yakwamba hakumfahamu Masiha,
hii ni hatua nzuri ambayo hivi leo wakatekumeni wanaanza nayo. Hawajui
chochote lakini Mungu huwaita na polepole humtambua Bwana. Kama ambavyo
nabii alibadilisha mwono wake kwa Masiha ndivyo ambavyo mkatekumeni
anavyoalikwa kusafiri polepole katika njia ya utambuzi mpaka kilima
kitakatifu. Mpendwa msikilizaji, twaweza kuzama katika ukatekumeni na
kusahau kwamba hata sisi tunao wajibu wa kuendelea kutafuta maana ya
wito wetu na hasa kutambua Masiha wetu si yule mfalme mkandamizaji bali
mwenye huruma na hasa akiwatumikia wengine. Ndiyo kusema wito wetu
tukimfuata yeye ni kuwa watumishi waaminifu wa Injili yake.
Mtazame
Yohane Mbatizaji anakiri yakwamba, yeye mwenyewe hakumfahamu na ndiyo
maana alitumwa akamshuhudie mbele ya mataifa kabla na katika udogo wake
huo alitumwa akawabatize watu kwa maji ili kujiandaa kumpokea Masiha.
Tena zaidi ya hilo anasema anapokuja habatizi kwa maji bali kwa moto na
Roho Mtakatifu. Hii ni alama ya Masiha alama ambayo yamtofautisha toka
Yohane Mbatizaji. Huyu kadiri ya Yohane Mbatizaji ni Mwana wa Mungu.
Basi kukiri kwa nabii kutusaidie kuwa wanyenyekevu katika maisha yetu na
hapo itakuwa rahisi kuhubiri habari njema.
Nikutakie furaha na amani katika kuwa mtumishi wa Mungu na hivi kuwa chombo cha mapatano na wokovu. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.
Lengo kuu ya jumuiya yetu ni kumtangaza Bwana YESU aliye alfa na omega katika historia ya wokovu wa binadamu wote hapa duniani.
Pages
- Home
- MALENGO YA JUMUIYA
- NGUVU YA ROZARI TAKATIFU
- PICHA ZA BWANA YESU
- AMRI ZA MUNGU
- AMRI ZA KANISA
- MFUMO WA UONGOZI
- SALA YA ASUBUHI
- SALA YA JIONI
- SALA MBALI MBALI
- MASOMO YA JUMAPILI NA TAFAKARI
- UMUHIMU WA SKAPULARI
- MAPAJI SABA YA ROHO MTAKATIFU
- KATEKISIMU KATOLIKI
- UFASIRI WA BIBLIA KATIKA KANISA
- “ROZARI YA BIKIRA MARIA”
- NANI MWABUDU SANAMU ?
- CONTACT US
- PICHA ZA BIKIRA MARIA
- HISTORIA NA UKUU WA BIKIRA MARIA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment