Friday, November 21, 2014

Jifunzeni kutoka kwa Bikira Maria!

Mwenyeheri Paulo VI kunako mwaka 1974 aliandika Waraka wa Kichungaji kuhusu Ibada kwa Bikira Maria unaojulikana kama Marialis cultus, ulionesha Ibada ambayo Papa Paulo VI alikuwa nayo kwa Bikira Maria, kama ambavyo pia inajionesha katika nyaraka zake mbali mbali zinazomtaja Bikira Maria kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa; Nyaraka ambazo zimekumbukwa na Taasisi za Kipapa katika kikao chake cha hadhara, Alhamisi, tarehe 20 Novemba 2014, tukio ambalo limehudhuriwa na Kardinali Pietro Parolin,Katibu mkuu wa Vatican aliyewakabidhi wajumbe hao ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Bikira Maria ni Mama mnyenyekevu, mwenye uso mpole, changamoto na mwaliko kwa waamini kukuza ndani mwao Ibada ya kina kwa Bikira Maria, kama kielelezo makini cha uzuri na ukuu wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Ni Mama mwombezi ambaye Mwenyeheri Paulo VI alipenda kumkimbilia wakati wa shida na mahangaiko ya Kanisa, kwani ni Mama aliyeonja shida na mahangaiko ya kibinadamu. 

Bikira Maria ni Malkia wa amani, watu wamkimbilie ili kuomba amani kwa ajili ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake; awasaidie watunga sera na sheria, kutunga sheria kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi, awasaidie na kuwaepusha watu na majanga mbali mbali, ili kukuza na kudumisha haki na upendo. 

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hata yeye katika mapambazuko ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya amelikabidhi Kanisa kwa Bikira Maria, ili kulisaidia Kanisa katika utume wake wa Uinjilishaji mpya ili kupata nguvu na ujasiri wa kusonga mbele kwa imani na matumaini, daima katia fadhila ya unyenyekevu na kiasi. Waamini kamwe wasichoke kuiga mfano wa Bikira Maria na kukimbilia katika maombezi yake, ili aweze kuwaongoza na kuwasimamia, kama Mama wa Mungu na Kanisa.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wale wote wanaojitaabisha kufanya tafiti mbali mbali kuhusiana na Bikira Maria ndani na nje ya Italia, anawataka waendelee na juhudi hizi, kwa kutambua mchango unaotolewa na Watumishi wa Bikira Maria nchini Mexico ambao amewapatia tuzo la Bikira Maria kutokana na mchango wao kwa Ibada ya Bikira Maria. 


Habari kwa hisani ya Radio vatican

No comments:

Post a Comment