Tuesday, November 11, 2014

Rais wa Ghana akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 10 Novemba 2014 amekutana na kuzungumza na Rais John Dramani Mahama wa Ghana pamoja na ujumbe wake, waliomtembelea mjini Vatican. Rais Mahama baadaye amekutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Dominique Mamberti, aliyekuwa Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko na mgeni wake katika mazungumzo yao, wamesifia mahusiano mazuri yaliyopo kati ya pande hizi mbili sanjari na mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ghana, hususan katika sekta ya elimu, afya pamoja na kuendeleza mchakato wa majadiliano kati ya makundi mbali mbali nchini Ghana.

Viongozi hawa kwa namna ya pekee, wamekazia umuhimu wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Baadaye wamegusia pia masuala ya kimataifa na hasa kuhusiana na maafa makubwa ambayo yamesababishwa na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, Afrika Magharibi.

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment