Kumekuwepo na ushirikiano mkubwa miongoni mwa Makanisa katika kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwani uhamiaji ni dhana ambayo inajengeka katika matumaini ya maisha bora zaidi, ingawa mara nyingi imekumbana na majanga makubwa.
Wahamiaji wanabeba ndani mwao utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho na kitamaduni; kwa matumaini ya kuweza kuchangia katika ustawi na maendeleo ya wengi; maisha, utu na heshima yao kama binadamu vinapaswa kuheshimiwa. Kuna sababu nyingi ambazo zinapelekea watu kuzikimbia nchi zao pamoja na kutambua madhara wanayoweza kukumbana nayo njiani.
Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko Ijuamaa, tarehe 21 Novemba 2014, wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Kongamano la Saba la Kimataifa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji, ambao wanachambua vyanzo na sababu kuu zinazopelekea watu kuzikimbia nchi zao: ukosefu wa usawa kati ya watu; umaskini, ongezeko la idadi ya watu, upungufu wa fursa za ajira, majanga asilia, vita, dhuluma na nyanyaso za kidini. Lakini ushirikiano katika mchakato wa maendeleo unaweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu, kwa kuchangia maendeleo pamoja na kuziba pengo linalosababishwa na upungufu wa idadi ya watu katika baadhi ya maeneo. Ushirikiano huu ni muhimu katika maboresho ya maisha ya wahamiaji na familia zao na katika nchi walikotoka.
Baba Mtakatifu anakiri kwamba, wakati mwingine, nchi husika hupoteza watalaam waliofundwa wakafundika. Watoto wanapata malezi tenge, kwa kukuzwa na mzazi mmoja, jambo ambalo ni hatari kwa ustawi na maendeleo ya watoto; kuvunjika kwa ndoa. Nchi wahisani wakati mwingine zinakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwapokea, kuwahifadhi na kuwaingiza wahamiaji katika uhalisia wa maisha ya wenyeji wao kutokana na utofauti mkubwa wa kijamii na kitamaduni.
Kutokana na changamoto zote hizi, wafanyakazi wanaowahudumia wahamiaji na wakimbizi wana mchango mkubwa katika mchakato wa majadiliano, mapokezi, sheria na uwakilishi. Madhara ni makubwa zaidi kwa familia na vijana katika nchi walimotoka.
Baba Mtakatifu anasema kuna uhusiano mkubwa kati ya ushirikiano, maendeleo na wahamiaji, changamoto kwa Kanisa kuendelea kuwaonjesha ukarimu wahamiaji sanjari na kuwashirikisha karama mbali mbali ambazo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu, lakini zaidi zawadi ya imani, kwa kuwaingiza katika mpango wa Uinjilishaji mpya sanjari na kuwasindikiza wahamiaji katika hija ya maisha yao, hadi watakapofikia mwisho wa safari yao. Lengo ni kuhakikisha kwamba, wahamiaji wanahudumiwa kikamilifu katika maisha yao ya kiroho kwa njia ya Katekesi, Liturujia na Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa.
Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, wahamiaji wanaishi katika mazingira magumu, duni na pweke, kiasi hata kushindwa kupokelewa na wenyeji wao. Kanisa halina budi kuwa ni mahali pa matumaini, katika kulinda na kutetea haki msingi za wahamiaji; kwa kuwapatia msaada bila ubaguzi kwa kutambua karama walizo nazo wahamiaji badala ya kuangalia tu matatizo na changamoto wanazoleta katika nchi wahisani, mwaliko wa kuwashirikisha katika uhalisia wa maisha ya wenyeji wao. Ndani ya Kanisa hakuna mgeni, kila mtu anapaswa kukaribishwa na kusaidiwa.
Licha ya Kanisa kuwa ni Jumuiya ya Waamini, lakini waamini wanamtambua Yesu katika sura ya jirani zao na Mama alisiyekuwa na mipaka, anayewatamadunisha na kuwapokea wote, ili kuwaonjesha mshikamano wa upendo, kwani kila mtu anathamani kubwa machoni pa Mungu, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kumbe utu na heshima yao vinapaswa kulindwa na kudumishwa.
Wahamiaji kama binadamu, wenye tunu msingi za maisha ya kitamaduni wanakuza udugu kati ya watu, changamoto ya kung'oa kabisa mambo yanayosababisha ukosefu wa usawa, haki na udhalimu, ili kujenga utambulisho mpana zaidi na wenyeji wao, ili kukoleza mchakato wa maendeleo unaojikita katika kipaji cha ugunduzi na heshima kwa utu wa wote.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Lengo kuu ya jumuiya yetu ni kumtangaza Bwana YESU aliye alfa na omega katika historia ya wokovu wa binadamu wote hapa duniani.
Pages
- Home
- MALENGO YA JUMUIYA
- NGUVU YA ROZARI TAKATIFU
- PICHA ZA BWANA YESU
- AMRI ZA MUNGU
- AMRI ZA KANISA
- MFUMO WA UONGOZI
- SALA YA ASUBUHI
- SALA YA JIONI
- SALA MBALI MBALI
- MASOMO YA JUMAPILI NA TAFAKARI
- UMUHIMU WA SKAPULARI
- MAPAJI SABA YA ROHO MTAKATIFU
- KATEKISIMU KATOLIKI
- UFASIRI WA BIBLIA KATIKA KANISA
- “ROZARI YA BIKIRA MARIA”
- NANI MWABUDU SANAMU ?
- CONTACT US
- PICHA ZA BIKIRA MARIA
- HISTORIA NA UKUU WA BIKIRA MARIA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment