Tuesday, October 15, 2013

Ombeni Amani Afrika Kati: Mashahidi wa imani na Upendo

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mtandao wa Tweet siku ya Alhamisi (29.08.2013) alisema kwamba Mungu ana sura na jina: Yesu Kristo. Sura hii ilionekana hivi majuzi na masista wa Monasteri ya Mama wa Neno la Mungu kwenye kitongoji cha Boy-Rabe walipoonyesha ushujaa usio na kifani na kuifungua milango ya nyumba yao ili kuwakaribisha waathirika wa vita kati ya makundi ya waasi vinavyoendelea huko Afrika ya Kati.
 

Hata hivyo, katika tokeo jingine iliwalazimu wenzao mapadri na Masista wa Upendo waishio Bohong kutorokea Bouar ili kuyaokoa maisha yao kutokana na mashambulio ya waasi wa Seleka. Naye Askofu Mkuu wa Bangui Dieudoniè Nzapalainga amesema alibahatika kutoroka Boy- Rabe muda mfupi tu kabla wapiganaji wa Seleka kukizunguka kitongoji hicho. Askofu Mkuu Nzapalainga ambaye pia ni rais wa Baraza la Maaskofu na rais wa shirika la Caritas chini humo anasema kwamba wananchi wa Afrika ya Kati wanaendelea kukata tamaa na hivyo ameiomba serikali na jumuiya ya kimataifa kuingilia kati na kuyaokoa maisha ya wan’Afrika ya kati.

Kulingana na ripoti ya shirika la habari la Fidez iliyonukuliwa na jarida la L’Osservatore Romano (August 24, 2013) linalochapishwa mjini Vatikani, watu wa maeneo ya Bangui, Boeing, Bainville na kwingineko wanajisikia upweke bila mahali pa kukimbilia wanaposikia mitutu ya bunduki na kuwaona wenzao wakiuawa bila ya huruma kwenye mapigano hayo. 


Ni wakati wa kuiombea Afrika amani kutokana na migogoro na kinzani ya vita inayoshuhudiwa sehemu mbalimbali za bara hilo. Hayo yalijitokeza bayana siku ya Jumapili 25-08-2013, wakati wa sala ya Malaika wa Bwana pale Baba Mtakatifu Francisko alipoiomba jumuiya ya kimataifa kuingilia kati swala la mapigano yanayoendelea nchini Syria na kutafuta suluhisho la amani.
Ni changamoto kwa wenyeji wa Afrika kupiga magoti na kumwomba Mama Bikira Maria Malkia wa Amani kuliombea bara la Afrika na kuwaongoza viongozi wa dunia kuonesha upendo, umoja na mshikamano kuhusiana na changamoto nyingi zinazolikumba bara la Afrika na watu wake. Waafrika pia wanachangamotishwa kutafakari kwa kina siasa na utendaji kazi utakaosaidia maendeleo endelevu ya bara Afrika na mafaa ya watu wake kwa ujumla. 


Ikumbukwe kwamba vita na milio ya bunduki kamwe haviwezi kujenga ila vinaongeza mateso ya wana wapenzi wa Mungu wanaoishi barani Afrika. Makundi ya kisiasa yana wajibu wa kuchangia kuleta amani na sio vurugu miongoni mwa jamii. Ni mwaliko kwa makundi yanayozozana sio tu Afrika ya Kati, Syria na Misri, lakini pia kote barani Afrika, kuchunguza athari na uharibifu wa maneno na matendo yao na hivyo kukata shauri kuendeleza amani na majadiliano kama njia muafaka ya kutatua tofauti zinazojitokeza kwenye sera na mikakati yao.


Habari kwa hisani ya Radio Vatican.

No comments:

Post a Comment